Mradi wa Chujio la Maji Nyandurumo Wafikia Hatua za Mwisho, Zaidi ya Wakazi 50,000 Kunufaika

  



Adeladius Makwega

Tarime, Mara TANZANIA.

 

Matumaini ya maelfu ya wakazi wa Wilaya ya Tarime ya kupata huduma ya maji safi na salama yanazidi kuimarika baada ya Mradi wa Ujenzi wa Chujio la Maji katika Chemchemi ya Nyandurumo kufikia hatua za mwisho za utekelezaji.

 

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, wakati alipofanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo wilayani Tarime Julai 20, 2026, akiambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.

 

Mbali na kukagua maendeleo ya miradi hiyo, Kanali Mtambi alisisitiza ushirikiano wa viongozi, wataalamu na wananchi ili kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa kwa fedha za Serikali inakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma iliyokusudiwa kwa wananchi.

 

Akizungumza katika eneo la mradi wa Chujio la Maji Nyandurumo, Kanali Mtambi alisema ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wake na kusisitiza kuwa hakuna sababu ya kuchelewesha kukamilika kwake.

 

"Najua mradi huu unagharimu takribani shilingi milioni 401. Hadi sasa shilingi milioni 379 tayari zimetolewa na kutumika, huku ikibaki nakisi ya shilingi milioni 22 pekee. Hii ni fedha ndogo. Tumeshakula ng'ombe mzima, sasa umebaki mkia tu. Nahitaji kuona mradi huu unakamilika mara moja," alisema Kanali Mtambi.

 

Alifafanua kuwa kukamilika kwa mradi huo kutakuwa suluhisho muhimu la changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wapatao 50,367 wa kata za Bomani, Tunwa na Nyandoto, hatua itakayochangia kuboresha afya, ustawi wa jamii na shughuli za kiuchumi.

 

Katika mkutano huo, baadhi ya wananchi wanaoishi jirani na eneo la mradi waliiomba Serikali kuwajumuisha katika huduma ya maji itakayotolewa kupitia chujio hilo. Akijibu ombi hilo, Kanali Mtambi alisema Serikali imelipokea na italifanyia kazi, huku akibainisha kuwa ipo mipango ya kutekeleza mradi mwingine mkubwa wa maji utakaowanufaisha wananchi wengi zaidi katika maeneo ya jirani.

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa MUWASA, Bi. Esther Gilyoma, alisema ujenzi wa chujio hilo ulianza rasmi Januari 26, 2024, na unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 31, 2026.

 

Alieleza kuwa mradi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha huduma za maji katika Mkoa wa Mara kwa kuhakikisha wananchi wanapata maji yenye ubora unaokidhi viwango vya afya.

 

Chujio la maji ni mfumo maalumu unaotumika kusafisha maji yanayotoka kwenye vyanzo mbalimbali, ikiwemo mito, chemchemi, mabwawa na visima, ili yawe salama kwa matumizi ya binadamu.

 

Mfumo huo huondoa uchafu, matope, chembechembe na, kulingana na teknolojia inayotumika, hupunguza au kuondoa bakteria pamoja na vijidudu vinavyoweza kusababisha magonjwa. Kutokana na uwezo huo, chujio la maji lina mchango mkubwa katika kuboresha ubora wa maji na kulinda afya za wananchi.

 

Kukamilika kwa Chujio la Maji Nyandurumo kunatarajiwa kuwa hatua muhimu katika kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama kwa maelfu ya wananchi wa Tarime, sambamba na kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha huduma bora za maji zinawafikia Watanzania wote.

 

makwadeladius@gmail.com

0717649257














 

 

 

 

 

 

0/Post a Comment/Comments