MIPAKA INAPINGUA UDUGU WA MWAFRIKA?

 





Adeladius Makwega – MBAGALA

Nakualika tena, msomaji wangu, katika makala ya katuni ya leo. Kumbuka, haya ni makala ya uchambuzi wa katuni kama zinavyochorwa katika vyombo mbalimbali vya habari na mitandaoni. Mtayarishaji wetu huchagua katuni nne; kwanza huzielezea zilivyo, kisha huzichambua kwa jicho lake makini, akizihusianisha na mazingira halisi yaliyomlenga mchoraji, na hatimaye kutoa maoni yake.

 

Leo, Mwanakwetu anafungua jalada kwa kuikamata katuni ya kwanza. Katuni hii inamuonesha baba anayekunywa chai kwa utulivu, huku mkewe akiwa pembeni na binti yao akimfundisha kusoma. Karibu nao, mtoto wa kiume anacheza kwa amani kabisa. Lakini kichwani mwa baba huyu—ndipo penye simulizi nzito—amebeba mawazo mengi: kodi, madeni, chakula, ada, umeme, nauli, na maji.

Katuni hii inabeba taswira ya mzigo mkubwa ambao wanaume na jamii kwa ujumla huubeba. Je, kweli, katika hali hiyo, hata chai au chakula kinaweza kupita kooni kwa amani?

Hilo ni swali ninalokuachia, msomaji wangu, kabla hatujahamia katuni ya pili.

 

Sasa, tunaikamata katuni ya pili. Hapa tunaona Mmasaai ambaye ameibiwa ng’ombe wake, na kwa bahati amemkamata mwizi huyo. Kesi inafikishwa kwa mwenyekiti wa kijiji. Mwenyekiti anasema kwa kujiamini: “Usiwe na wasiwasi, hapa ndipo haki yako itapatikana.” Lakini Mmasaai anajibu kwa msisitizo: “Mimi sitaki haki—nataka ng’ombe wangu!”

Hii ni katuni yenye mcheko wa kina—inatuchokoza kufikiria tofauti kati ya haki ya kisheria na haki ya vitendo.

Tunapoendelea, Mwanakwetu anaikamata katuni ya tatu, iliyotumiwa na DW Kiswahili katika mitandao ya kijamii, ikichorwa na Said wa Michael, maarufu kama Wakudata. Katuni hii inamuonesha mwanamke aliyevalia abaya nyeusi na hijabu nyekundu. Pembeni yake wapo viongozi watatu kutoka vyombo vya ulinzi—polisi, jeshi, na usalama—wakiwa na maumbo makubwa, mithili ya ngongoti wa ngoma za asili za Kimakonde. 

Wananchi wengi wanaonekana wakiwa ndani ya wigo, kama zizi lililofungwa kwa minyororo. Mnyororo huo umepewa jina: “Sheria.” Viongozi hawa wako nje ya zizi, kana kwamba wao ndiyo wanaomiliki mfumo huo.

Katika mazungumzo yao, mmoja wao anasema: “Mama anapiga mwingi,” huku wakidai kuwa ana tuhuma za kujibu. Lakini mama huyo anajibu kwa msisitizo: “Hakuna aliye juu ya sheria.”

Hata hivyo, taswira inaonesha kitu kingine—kwamba walioko nje ya zizi ndio wanaonekana kuwa juu ya sheria, huku mwananchi akiwa ndani ya mnyororo huo. Hapa, mchoro unazua mjadala mzito: je, kweli viongozi wako juu ya sheria?

Kwa uchambuzi wa Mwanakwetu, katuni hii inaonesha upinzani mkali dhidi ya dhana hiyo, huku DW Kiswahili ikiendeleza mjadala huo kwa sauti ya kimataifa. Kwa kuangalia kwa makini, sura ya mhusika mkuu inaonekana kumlenga Rais Samia Suluhu Hassan.

Swali linabaki palepale: Je, nchini Tanzania, viongozi wako juu ya sheria?

Hili ni swali zito linalohitaji tafakari ya kina.

 

Hatimaye, tunaifikia katuni ya nne na ya mwisho, pia kutoka kwa Said wa Michael na kusambazwa na DW. Katuni hii inamuonesha mwanasiasa maarufu kutoka Kenya, Bi Martha Karua, akishuka katika uwanja wa ndege wa Entebbe nchini Uganda, lakini akizuiwa kuingia. Askari anasema kwa ukali: “Hairuhusiwi hata kukanyaga ardhi.”

Ni kweli, Martha Karua hakuruhusiwa kuingia Uganda. Aliporudi Kenya, alipokelewa na umati wa watu, na akasema kwa huzuni:

“Jamani, kweli tumefikia hapa! Haya yanayofanyika Uganda na Tanzania? Ndugu zangu Wakenya, kuna haja ya kuingia katika hali ya dharura.”

Mtayarishaji wa makala haya anashangazwa na hali hii. Anakumbusha kuwa kabla ya mipaka ya kikoloni, tulikuwa kitu kimoja—hakukuwa na pasi wala vizuizi. Leo, kumtembelea ndugu yako kunahitaji masharti mazito.

Hali hii inahusishwa pia na tukio lililoripotiwa Tanzania, ambapo wanaharakati kutoka Kenya na Uganda—Boniface Mwangi na wakili Agather Atuhaire—walidai kukamatwa, kuteswa, na kunyanyaswa kingono walipokuwa wakifuatilia kesi ya kisiasa. Serikali ya Tanzania ilikanusha vikali madai hayo.

Wanaharakati hao walifungua kesi katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ), wakidai fidia ya dola milioni moja za Kimarekani kila mmoja. Ikiwa watashinda, Tanzania inaweza kulazimika kulipa kiasi kikubwa cha fedha—takribani shilingi bilioni tano—ambazo ni fedha za walipakodi.

Kwa kifupi, madhara ya kesi hii kwa Tanzania yanaweza kuwa makubwa katika nyanja za sheria, siasa, diplomasia, na taswira ya kimataifa. Hatima yake itategemea uamuzi wa mahakama na ushahidi utakaowasilishwa.Swali ni moja tu Je mipaka inapingua Udugu wa Mwafrika?

Mwanakwetu, upo?

Hadi hapo, nami nalifunga jalada la makala ya katuni ya leo. Tumepitia katuni nne: ile ya mzigo wa maisha kichwani kwa mzazi, ya Mmasaai na ng’ombe wake, ya viongozi na sheria, na hatimaye ya Martha Karua—ambayo ndiyo inayohitimisha makala yetu ya leo.

Kumbuka…

“Mipaka Inapingua Udugu wa Mwafrika.”

Nakutakia siku njema.

Adeladius Makwega


📧 makwadeladius@gmail.com


📞 0717649257

 

 

0/Post a Comment/Comments