Adeladius
Makwega
Butiama & Musoma, Mara, Tanzania.
Julai 3, 2026, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Lameck Mwigulu Nchemba, alifanya ziara katika Wilaya ya Butiama na Wilaya ya Musoma. Katika maeneo yote mawili, kiongozi huyu wa tatu katika uongozi wa taifa hili la Afrika Mashariki—baada ya Rais na Makamu wa Rais—ukiweka kando miradi aliyokagua, akaweka mawe ya msingi, akaifungua, na pia alizungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara.
Katika mikutano hiyo miwili ya hadhara, hasa ule wa Butiama, lilifanyika jambo moja zuri sana ambalo leo Mwanakwetu analihifadhi katika kumbukumbu zake za ziara hii.
Majira ya asubuhi, Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba aliwasili katika viwanja vya mkutano huo Butiama. Kabla ya shughuli kuanza, ilitolewa nafasi ya sala na dua kutoka kwa viongozi wa dini. Zoezi hili limekuwa likifanyika hata katika siku zilizotangulia, lakini siku hii ya Julai 3 hali ilikuwa hivi:
“Mhe. Waziri Mkuu, sasa viongozi wa kiroho waliopo hapa watuongoze katika sala na dua. Namualika Baba Mchungaji Baraka Ogina atuongoze kwa sala, akiwakilisha Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT).”
Mchungaji Ogina:
“Asante, tuombe! Kwa jina la Mungu Baba, Mungu Mwana na Roho Mtakatifu (Amina).
Ewe Mwenyezi Mungu Baba yetu uliye hai, tunakushukuru sana kwa ajili ya taifa letu Tanzania. Tunamuombea Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan; umpe hekima na busara katika kuiongoza nchi yetu. Kipekee, tunamleta mbele zako mpendwa wetu Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Waziri wetu Mkuu. Asante, Mungu, kwa utumishi uliomo ndani yake. Tunakuomba uendelee kumpa nuru kila anapokutana na changamoto za wananchi.
Kwa wana Butiama, tuna kila sababu ya kukushukuru, Baba yetu, kwa ajili ya viongozi wetu wanaochapa kazi: Mkuu wetu wa Wilaya, Tekla George Mkuchika; Mkuu wetu wa Mkoa, Kanali Evans Alfred Mtambi; na ndugu yetu Dkt. Charles Mahela, Mbunge wa Jimbo la Butiama, pamoja na watendaji wote wa Halmashauri ya Butiama.
Ewe Mwenyezi Mungu, wape viongozi wetu moyo wa kuitanguliza nchi yetu kwanza, ili waweze kutuongoza kwa haki, utu na upendo. Kwa jina la Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. Amina (Amina).”
Kisha akaalikwa kiongozi mwingine wa dini:
“Sasa, Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba nimualike Sheikh Salumu Mwisukwa, anayewakilisha Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA).”
Sheikh Mwisukwa:
“Bismillahi Rahmani Rahim. Alhamdulillahi Rabbil ‘Alamin. Wasalatu wasalam ‘ala
Rasulillah.
Ewe Mwenyezi Mungu, Mola wetu wa haki, tunanyanyua mikono yetu kukuomba. Tunakuomba umlinde kiongozi wetu, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba. Mkinge na kila aina ya uovu na umuepushe na kila shari.
Mola wetu, tunakuomba uilinde amani ya nchi yetu Tanzania. Pasipo amani hatuwezi hata kutoka majumbani mwetu kwenda kukuabudu wewe. Tunakuomba pia umlinde Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan; umuepushe na kila aina ya uovu na umkinge na vitimbwi vyote.
Ewe Mwenyezi Mungu, tunakuomba haya tukiwa na imani kwako. Amina.”
Baada ya hapo, aliitwa kiongozi mwingine wa dini kuhitimisha:
“Kwa kuhitimisha sala, naomba nimualike Padri Fidelis Busiga, anayewakilisha Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).”
Padri Busiga:
“Kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu (Amina). Tuombe.
Ewe Mwenyezi Mungu wa milele, Baba wa watu wote na mataifa yote, utuangalie kwa macho yako yenye huruma sisi Watanzania. Kwa baraka yako na uhuru wetu, utuwezeshe kuishi kadiri inavyowapasa wana wa Mungu.
Waongoze watawala wetu ili sheria wanazotunga ziwe za manufaa kwa watu wako. Wajalie watu wako wote paji la imani, ili tusishindwe kupambana na maovu yanayotukabili kutoka ndani au nje.
Utujalie hekima ya kutafuta ukweli na kuishi kwa uaminifu katika amri zako. Washa ndani ya mioyo yetu upendo wako wa Kimungu ili tushinde chuki, ukabila na ubaguzi, na utuunganishe katika umoja wa kweli.
Bariki taifa letu, liwe na amani na mataifa mengine. Waongoze watawala wetu watimize wajibu wao ipasavyo. Wasaidie raia wote kupata maisha bora hapa duniani na hatimaye uzima wa milele mbinguni. Amina (Amina).”
Haya yote ni dua na sala zilizofanyika ndani ya Wilaya ya Butiama.
Mwanakwetu anasema nini leo?
Hivi ndivyo hali ya dua na sala ilivyokuwa Julai 3, 2026, wilayani Butiama. Hata hivyo, hali ilikuwa tofauti kwa siku za Julai 1 na Julai 2, 2026, na hata Julai 3, 2026 wilayani Musoma, ambapo dua na sala zilifanyika lakini baadhi ya wahusika walionekana kuwa pungufu.
Kutokana na hali hiyo, ilizuka mjadala kati ya Mwanakwetu na mwanahabari mmoja aliyemuuliza:
“Mbona ndugu zako Mwanakwetu siwaoni?”
Mwanakwetu alijifanya hajamsikia. Mwanahabari huyo akaongeza:
“Huu ni mkutano wa nne, sijawaona.”
Walipoonekana katika mkutano wa tano, mwanahabari huyo alimchokoza tena Mwanakwetu akisema:
“Kwa kweli leo wapo.”
Walipofika mkutano wa Musoma Mjini, alisema:
“Kwa kweli hapa hawapo.”
Akaongeza kuwa, Waziri Mkuu anatarajiwa kufanya mikutano katika majimbo karibu yote ya Mkoa wa Mara. Tangu Julai 1 hadi Julai 5, 2026, mikutano sita ilifanyika katika majimbo sita, ambapo “Kweli Hapa Hawapo” ilijitokeza mara tano na “Kweli Hapa Wapo” mara moja tu.
Je, katika majimbo kumi hali itakuwaje? Kama katika majimbo manne yaliyosalia “Kweli Hapa Wapo” itajitokeza mara zote, basi itakuwa sare ya tano kwa tano.
Je, ndugu wa Mwanakwetu (“Kweli Hapa Wapo”) wataweza kuvunja rekodi hii? Watajidhihirisha kama ilivyokuwa Butiama?
Mwanakwetu anaamini kuwa hatupaswi kuandika kwa kubahatisha wakati ukweli bado unakusanywa. Tungoje mikutano hiyo ikamilike.
Katika makala haya, Mwanakwetu anaongeza kuwa lengo lake ni kutoa somo kwa wanahabari vijana: kwamba hata dua na sala katika ziara za viongozi zinaweza kuwa chanzo cha habari au makala yenye ujumbe kwa jamii—hasa pale panapohitaji kukazia nati na sukurubu kama kuna hisia kuwa kuna pahala pahala pamelegea Tanzania kama taifa lazima twende pamoja hakuna mkamilifu kama kuna ushauri umetolewa lazima tujitathimini sote twende pamoja maana Tanzania haiwezi kupata baraka kwa kusaliwa nusunusu.
Mwanakwetu upo? Je, kichwa cha makala kiitwaje?
“Kweli Hapa Wapo?” au “Kweli Hapa Hawapo?”
Vichwa vyote viwili Mwanakwetu amevipenda—kama mikwaju ya penalti tano kwa tano. Lakini kwa sasa, ni tano kwa moja.
Hawa ni nduguze Mwanakwetu:
KWELI HAPA HAWAPO.
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717 649 257
.gif)



.gif)
Post a Comment