Adeladius Makwega – Musoma, Mara, Tanzania
Tafakari ya Dominika ya 16 ya Mwaka A wa Kanisa, iliyoandaliwa na Padri Bonaventura Maro na kurushwa na Redio Vatican pamoja na mitandao yake ya kijamii, inasisitiza ukuu wa huruma na uvumilivu wa Mwenyezi Mungu. Licha ya udhaifu na dhambi zetu, Mungu hatuadhibu mara moja, bali hutupa nafasi ya kutubu na kupata wokovu ili tuweze kuishi maisha yenye maadili mema.
Ujumbe huu mkuu umejengwa juu ya misingi ya kimaandiko ifuatayo: Huruma ya Mungu:Mungu wetu ni wa rehema na neema, mvumilivu na mwingi wa fadhili kwa wale wanaomgeukia. Nafasi ya Toba:Katika Kitabu cha Hekima tunafundishwa kuwa Mungu hutupa nafasi ya kutubu dhambi zetu badala ya kutuangamiza. Wito kwa Waamini:Tunaalikwa kujenga utamaduni wa kujipatanisha na Mungu na jirani kupitia Sakramenti ya Kitubio, na kuishi kwa uvumilivu.
Makadinali walipofika madhabahuni mwa Bwana, walitoa tafakari ifuatayo:
“Tunaendelea kujifunza kupitia mifano ya Yesu Kristo kuhusu ufalme wa Mungu. Bado tuko katika sura ya 13 ya Injili ya Mtakatifu Mathayo. Yesu anaufananisha ufalme wa Mungu na mtu aliyepanda mbegu njema katika shamba lake; usiku, adui akaja akapanda magugu katikati ya ngano. Kisha mtu huyo akawaagiza watumishi wake wasubiri hadi wakati wa mavuno ili watenganishe magugu na ngano. Halafu Bwana anawaambia wanafunzi wake: ‘Ufalme wa mbinguni ni kama punje ya haradali, ambayo ingawa ni ndogo, ikikomaa huwa makao ya ndege wa angani. Pia ufalme wa Mungu unafanana na chachu, ambayo kiasi kidogo tu huumiza donge lote la unga wa mkate.’
Ndugu zangu, mifano hii inaonyesha uvumilivu wa Mungu na mwanzo wa ufalme wake. Atangoja hadi wakati wa mavuno, yaani wakati wa hukumu, ili kutofautisha magugu na ngano, mabaya na mema. Kwa sababu ukuaji wa ufalme wake hukamilika wakati wa mavuno.
Hawahukumu mapema mbegu; anatuacha tukue, tukitumaini tutazaa matunda mema. Haki na wema hukutana ndani ya Mungu.”
Haya ni maneno ya Kardinali Luis Antonio Tagle, Mkuu wa Baraza la Uinjilishaji wa Watu (Propaganda Fide) wa Kanisa Katoliki ulimwenguni.
Kwa upande wake, Mwanakwetu, katika Dominika ya Julai 19, 2026, alihudhuria Misa katika Kanisa la Mtakatifu Agustino, Parokia ya Mwisenge, Jimbo Katoliki la Musoma. Tafakari ya Dominika ilitolewa na Frateli Justine Mapesa, ambaye alianza kwa kisa cha ajali ya ndege:
“Ndege moja ya abiria iliruka kutoka mji mmoja kwenda mwingine. Ilipokuwa angani, gurudumu lake moja lilichomoka. Watu wa kiwanja cha kwanza walimjulisha rubani, naye akawaeleza abiria kuwa lolote linaweza kutokea, hivyo wawe tayari. Taarifa pia ilitumwa kiwanja cha pili ili kujiandaa kupokea ndege hiyo.
Ndani ya ndege kulikuwa na taharuki kubwa. Abiria walihisi kuwa kifo kiko karibu, na kila mmoja alianza kujitafakari na kutubu dhambi zake. Wakatoliki walimtafuta padri ili waungame. Hali ilikuwa ya hofu kubwa, lakini kwa neema ya Mungu, ndege ilitua salama katika kiwanja cha pili.”
Frateli Mapesa alieleza kuwa hofu hiyo ilitokana na ukweli kwamba wengi hawakuwa tayari kukutana na kifo. Hivyo, alisisitiza kuwa kila muumini anapaswa kuishi daima akiwa tayari, kwa kuzingatia sifa za ufalme wa Mungu. Ndiyo maana Yesu hutumia mifano kusema: “Ufalme wa Mungu unafanana na…” badala ya kutoa maelezo ya moja kwa moja.
Baada ya Misa, Mwanakwetu alianza safari ya kurejea nyumbani. Njiani alikutana na makundi matatu ya watoto waliokuwa wakielekea kanisani kusali misa ya pili.
Kundi la kwanza lilikuwa na mabinti wawili wenye umri wa takribani miaka 10 na 11. Walikuwa wakitaja methali za Kiswahili:“Siri ya maiti?”Mwenzake akajibu: “Aijuaye mwosha.” “Adhabu kaburini?”Mwenzake akajibu: “Aijuaye maiti.”
Kundi la pili lilikuwa kubwa, likijumuisha wavulana na wasichana. Waliokuwa mbele walimsalimia Mwanakwetu kwa heshima (“Shikamoo”), naye akaitikia “Marahaba.” Waliokuwa katikati hawakumsalimia, lakini waliokuwa nyuma walimsalimia. Kundi la tatu lilikuwa la wavulana pekee, wakionekana wenye haraka na nyuso zenye hasira. Waliokuwa mbele hawakusalimia, lakini mmoja aliyekuwa nyuma, licha ya kuonekana mwenye hasira zaidi, alimsalimia kwa heshima.
Swali: Je, kisa hiki kina maana gani katika mwanga wa masomo ya Dominika hii?
Tofauti za watoto – Ngano na magugu, Watoto hawa wanaonyesha hali tofauti: wapo wenye heshima, wapo wanaopuuza, na wapo wenye hasira. Hata hivyo, wote wanaenda kanisani. Hii inaakisi maisha ya waamini—ndani ya jamii moja kuna wema na udhaifu, lakini wote wako safarini kuelekea kwa Mungu.Kila mtu ana chembe ya wemaHata wale walioonekana wakali bado walionesha ishara ya heshima. Hii inaonyesha kuwa ndani ya kila mtu, hata akiwa na mapungufu, kuna wema fulani unaoweza kukua—kama punje ya haradali au chachu.
Tusiharakishe kuwahukumu watu kwa matendo yao ya nje. Kila mtu yuko katika safari ya imani, na Mungu anaendelea kufanya kazi ndani yake. Katika maisha ya imani, watu hutofautiana sana, lakini Mungu huvumilia wote na kuwapa nafasi ya kukua na kubadilika. Hukumu ya mwisho iko mikononi mwake, si yetu.
Mwanakwetu anatambua viongozi wa dini wanalo jukumu la kuturejesha katika njia kuu pale tunapokengeuka na hata hivyo makala haya yanatumika kama kengele ya kukumbushana mimi na wewe kuwakumbusha watoto wetu wawe wanakukumbuka kuheshimu wakubwa pale wanapokutana nao na isitohse Mwanakwetu njiani aliwakumbusha wale waliomnyima shikamoo kusalimu wakubwa kila wanapokutana nao.
Mwanakwetu upo? Kumbuka:
“Kutoka Magugu Hadi Ngano: Nafasi ya Toba na Mabadiliko.”
Nakutakia siku njema.
Mawasiliano:
Barua pepe: makwadeladius@gmail.com
Simu: 0717 649 257
.gif)









.gif)

Post a Comment