KUTOKA MADHABAHUNI HADI MTAANI

Adeladius Makwega, Musoma – Mara, Tanzania.

Tafakari ya Padri Bonaventura Maro imetumika na Vatican katika redio na kurasa zake za mitandao ya kijamii kuhusu Dominika ya 15 ya Mwaka A wa Kanisa, ikiambatanishwa na Maadhimisho ya Utume wa Bahari.

 

Padri Maro amesisitiza umuhimu wa mabaharia na wavuvi katika maisha ya watu, akihimiza jamii kuwathamini kwa kazi yao licha ya changamoto wanazokutana nazo wakiwa kazini.

 

Aidha, anaeleza kuwa Neno la Mungu lina nguvu kubwa na linaweza kubadilisha maisha ya mtu. Kama mbegu, Neno hilo linahitaji moyo ulio tayari ili likue na kuzaa matunda mema. Mfano wa Waisraeli unaonesha kuwa Mungu hutimiza ahadi zake hata wakati wa matatizo.

Zaidi ya hayo, Padri Maro ameeleza kuwa mateso ya sasa si ya kudumu, kwani kuna tumaini la maisha bora yajayo. Ameongeza kuwa katika Injili, mfano wa mpanzi unaonesha kuwa watu hulipokea Neno la Mungu kwa namna tofauti kulingana na hali ya mioyo yao. Hivyo, alihimiza kila mmoja kuwa na moyo mzuri unaopokea na kuishi Neno la Mungu ili kuzaa matunda mema kama upendo, amani na wema katika maisha ya kila siku.

Kwa upande mwingine, Makadinali nao hawakuwa mbali na tafakari ya Dominika hii:

 

“Yesu anaufananisha Ufalme wa Mungu na mtu aliyekwenda kupanda mbegu. Baadhi ya mbegu zilianguka njiani na kuliwa na ndege. Nyingine zilianguka kwenye udongo wa miamba, zikamea lakini zikanyauka kwa sababu ya joto. Zingine zilianguka katikati ya miiba ambayo ilizisonga chipukizi. Kisha mbegu zilizoanguka kwenye udongo mzuri zilikua na kuzaa matunda mara mia, sitini au thelathini.

Katika mfano huu, Mungu analitoa Neno lake kwa aina mbalimbali za udongo, yaani hali tofauti za mioyo yetu tunaposikia Neno la Mungu. Neno la Mungu ni kwa ajili ya wote. Tuombe neema ya kuwa udongo mzuri ili tuupokee Ufalme wa Mungu na kuzaa matunda mengi.”

Haya ni maneno ya Kardinali Luis Antonio Tagle, Kiranja wa Propaganda Fide ya Kanisa Katoliki ulimwenguni inayoshughulika na uinjilishaji wa watu.

 

Katika Dominika hii, ndugu yetu Mwanakwetu alisali katika Kanisa la Mtakatifu Agustino, Parokia ya Mwisenge, Jimbo Katoliki la Musoma, ambapo homilia ilitolewa na Frateli Mapesa. Katika mahubiri yake, alieleza jinsi Mtume Paulo alivyofika mji wa Athene na kuwafundisha watu waliokuwa na imani mbalimbali pamoja na dhana ya “Mungu Asiyejulikana.” Paulo alitumia dhana hiyo kuwafundisha, japokuwa muitikio wao ulikuwa mdogo. Frateli Mapesa pia alinukuu Kitabu cha Tenzi za Rohoni, utenzi namba 140, akihimiza Wakristo kuhesabu baraka za Mungu.

 

Alisisitiza kuwa, licha ya changamoto tunazokutana nazo, tunapaswa kuendelea kuhesabu baraka za Mungu. Alitoa mfano wa binti wa miaka 12 kutoka Venezuela aliyenusurika katika tetemeko la ardhi lililosababisha vifo vya watu 4,000, lakini aliendelea kuwa na tabasamu licha ya hali ngumu aliyopitia.

 

Haya yote yalijiri katika Dominika ya 15 ya Mwaka A wa Kanisa, tarehe 12 Julai 2026.

Baada ya ibada, Mwanakwetu alipokuwa anatoka kanisani, alikutana na makundi matatu tofauti: kundi la kwanza la kondoo na mbuzi wengi likiongozwa na kijana aliyekuwa akiwapeleka malishoni; kundi la pili la Wakristo waliokuwa wakielekea kusali misa ya pili; na kundi la tatu la mbuzi wachache na ng’ombe wengi waliokuwa wametawanyika ovyo, bila mchungaji kuonekana, huku magari yakipita kwa tabu yakipiga honi.

 

Karibu naye kulikuwa na ng’ombe jike mweusi, mzuri sana, aliyeonekana kuwa ananyonyesha kutokana na chuchu zake zilizojaa maziwa. Wazee wawili walipita karibu na kumtazama ng’ombe huyo. Mmoja alisema angekuwa dume angefaa sana kwa kupandisha, na mwenzake akasema hata jike linaweza kufaa, ingawa ni kazi kumhudumia hadi azae.

 

Mwanakwetu aliwasalimia wazee hao na kuendelea na safari yake, huku akiwaza kuwa mifugo inaweza kuwa mizuri, lakini bila mchungaji makini huweza kuzurura, kula vitu hatari, kugongwa na magari au kuibiwa.

 

Mbele kidogo alikutana na mama mmoja aliyebeba fimbo ya kuchungia, akizungumza na mwenzake kuhusu harusi. Ghafla alisema anahitaji kuwahi kwani mifugo yake ilikuwa inavuka barabara.

 

Mwanakwetu aliendelea na safari yake ya kurejea nyumbani.

 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Funzo kuu linalotokana na makundi haya matatu aliyokutana nayo Mwanakwetu lina uhusiano mkubwa sana na Injili ya Dominika hii (mfano wa mpanzi):

“Kundi la kwanza (kondoo na mbuzi wenye mchungaji makini):Hili linafanana na udongo mzuri katika Injili. Mifugo inaongozwa vizuri, inaelekea malishoni salama. Hii inaashiria watu wanaolisikia Neno la Mungu, wanaliweka moyoni na kulifuata kwa vitendo. Matokeo yake ni maisha yenye mwelekeo na matunda mema.

Kundi la pili (Wakristo wanaokwenda kusali):Hili linaweza kufanana na wale wanaopokea Neno lakini bado wako safarini kiimani. Wanajitahidi kusikia Neno la Mungu (kwenda misa), lakini bado wanahitaji kulikuza ndani yao ili lisizae matunda ya muda mfupi tu kama ilivyo kwa mbegu iliyoanguka kwenye miamba.

Kundi la tatu (mifugo mingi bila mchungaji, imetawanyika): Hili linafanana na mbegu zilizoanguka njiani au kwenye miiba. Bila uongozi, mifugo inakuwa hatarini—inaweza kupotea, kugongwa au kula vitu visivyofaa. Hii inaashiria watu wasio na mwelekeo wa kiroho; wanalisikia Neno lakini halikae ndani yao au linazongwa na mambo ya dunia.

Mwanakwetu anasema,Injili inatufundisha kuwa tatizo si mbegu (Neno la Mungu), bali ni hali ya udongo (moyo wa mtu). Vivyo hivyo katika maisha ya Mwanakwetu, tofauti haikuwa mifugo bali uwepo au ukosefu wa mchungaji.

Hivyo, tunaitwa kuwa kama kundi la kwanza: kuwa na “mchungaji” (yaani mwongozo wa Mungu), kuwa na moyo mzuri, ili Neno la Mungu lizae matunda katika maisha yetu.

Mwanakwetu upo? Kumbuka:

“Kutoka Madhabahuni Hadi Mtaani.”

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com
0717649257


















 

0/Post a Comment/Comments