Julai 4, 2026, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba, alifanya mkutano wa hadhara katika eneo la Suguti, wilayani Musoma, mkoani Mara.
Katika mkutano huu, ambao ulikuwa pekee katika ziara ya Waziri Mkuu iliyofanyika mkoani Mara kuanzia Julai 1 hadi 4, malalamiko yalitolewa hadharani dhidi ya viongozi wanaopigiwa kura. Kwanza, alilalamikiwa diwani juu ya deni analodaiwa la shilingi milioni 10. Pili, alilalamikiwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Suguti kwa namna anavyoendesha ofisi.
Msomaji wangu, nakuomba ufahamu hili:
Kwa mujibu wa utaratibu wa uchaguzi nchini Tanzania, kura hupigwa kwa wenyeviti wa vijiji/mitaa na wajumbe wao, kisha diwani, halafu mbunge, na mwisho ni Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Japokuwa kura hizi hupigwa kwa vipindi tofauti, kwa kawaida huanza na wenyeviti wa vijiji na mitaa, kisha diwani, mbunge na Rais.
Katika mkutano huu, ndugu Kasamwila Halamba Kasamwila alitoa malalamiko dhidi ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Suguti, ndugu Sadiki Msembe Chibuda. Alidai kuwa mwenyekiti huyo anatumia vibaya madaraka yake.
Miongoni mwa malalamiko hayo ni tukio la kuzuia nyama iliyokwisha chinjwa, yenye uzito wa kilo 100, kuuzwa, jambo lililosababisha nyama hiyo kuoza.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Suguti, ndugu Chibuda, alipojitokeza mbele ya Waziri Mkuu, alijibu kuwa tukio hilo lilitokana na changamoto ya wizi wa mifugo. Alisema kuwa afisa mifugo alitoa maelekezo kuwa ng’ombe yeyote anayechinjwa lazima ijulikane ametoka wapi. Aidha, alidai kuwa ndugu Kasamwila ni mpinzani wake wa kisiasa anayatumia mazingira ya hadhara kumchafua, na kwamba nyama hiyo haikuoza.
Kwa upande wake, ndugu Kasamwila alieleza kuwa suala hilo lilifikishwa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya husika na baadaye kwa Mkuu wa Wilaya, lakini hadi Julai 4, 2026, hakuwa amelipwa fidia ya kilo 100 za nyama zinazodaiwa kuoza.
Maamuzi ya Waziri Mkuu yalikuwa yafuatayo: chombo cha usalama ngazi ya wilaya kifanye uchunguzi juu ya ukweli wa madai ya kuoza kwa nyama hiyo na kumpatia taarifa mara moja. Kuhusu malalamiko ya utendaji kazi wa Mwenyekiti wa Kijiji cha Suguti, alielekeza kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, afike kijijini hapo na kuitisha mkutano wa kijiji ili kubaini ukweli, kisha mkutano huo utoe maamuzi.
Mwanakwetu anasema nini leo?
Kufanya siasa vizuri kwa viongozi wanaopigiwa kura kunahitaji sana uungwaji mkono kutoka kwa wale wanaowaongoza. Japokuwa unapata uongozi kwa kura za wananchi, kufanya kazi kwa ufanisi kunategemea jinsi jamii husika—iwe kijiji, kata, jimbo au taifa—wanavyokuzungumzia.
Iwapo jamii itakuzungumzia vibaya, hiyo ni changamoto kubwa, na kufanya kazi kwa ufanisi kunakuwa kugumu.
Unaweza ukaongoza jamii, lakini ukifika mezani kula, hata tonge la ugali halishuki kooni. Hali hii inaweza kudhoofisha kabisa uwezo wako wa kukitendea haki kiti unachokikalia.
Mwanakwetu anaamini kuwa heshima ya kiti unachokalia huanza na kura za wananchi—hili halina ubishi. Hata hivyo, kuilinda heshima hiyo kunategemea namna jamii inavyokuunga mkono. Ikiwa jamii haikuungi mkono, inaweza kukuona kama sehemu ya tatizo, na wewe ukawa tatizo la ngazi ya juu zaidi kwa kuwa wewe ndiye unaonekana kwanza.
Hii ni tafakari ya Mwanakwetu juu ya kisa hiki cha Kijiji cha Suguti, ambapo alishuhudia tukio hili.
Kwa hakika mgogoro wa Kijiji cha Suguti unaweza pia kulinganishwa kwa ngazi yoyote ile ya uongozi inayopigiwa kura iwe Kata, Jimbo na hata Taifa.
Mwanakwetu upo?
Kumbuka:
“Kiongozi hushamiri kama jamii inamuunga mkono.”
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717 649 257











.gif)
Post a Comment