Adeladius Makwega – MBAGALA
Ilikuwa majira ya jioni ya Julai 19, 2026. Mwanakwetu alipokea simu kutoka kwa jamaa yake mmoja akimweleza matokeo ya Kidato cha Sita ya mwanafunzi mmoja aliyepata Daraja la Kwanza lenye pointi nane.
"Yeye amesema anakwenda kusomea uhandisi wa madini."
Mwanakwetu alipokea taarifa hiyo vizuri sana na kumpongeza mwanafunzi huyo kwa ufaulu wake.
Jamaa yake akaongeza:
"Lakini wanasema ukisomea sekta ya madini, tatizo ni kupata kazi."
Mwanakwetu akajibu:
"Hapana. Jukumu la mwanafunzi ni kusoma. Mambo ya kupata kazi huja baada ya kuhitimu mafunzo, japokuwa ni muhimu kusoma taaluma ambayo una uhakika nayo katika soko la ajira."
Ndugu huyo akaendelea kusema kuwa sekta ya madini imekuwa na changamoto kwa muda mrefu, si Tanzania tu bali hata duniani kote.
Mwanakwetu akauliza:
"Kwa nini?"
Jamaa akajibu:
"Mathalani, taifa kama Kongo (Zaire) lina madini mengi, lakini utulivu bado ni bidhaa adimu sana."
Mwanakwetu akasema:
"Ndiyo, lakini hatuwezi kumwambia mtoto asiingie katika ndoa kwa sababu tu ndoa zina migogoro isiyokwisha."
Baada ya mazungumzo hayo, Mwanakwetu aliagana na ndugu yake, kisha akabaki peke yake akiwa katika tafakari kubwa kuhusu biashara ya madini duniani.
Akilini mwake alikubaliana kwamba changamoto za umaskini, vita, mauaji na migogoro ya wenyewe kwa wenyewe nchini Kongo, ambayo imeendelea kwa takribani miaka 100, zimekuwa zikiambatana na uwepo wa madini mengi. Madini hayo hayajaweza kuleta utulivu, amani wala maendeleo makubwa ya viwanda kwa wananchi wa maeneo husika, huku mataifa makubwa yakiendelea kunufaika na bidhaa hiyo.
Mwanakwetu alivuta picha kwamba hata madini yanapogunduliwa katika shamba la mtu mmoja, tamaa ya jamii inayomzunguka huongezeka. Hali hiyo inaweza kusababisha migogoro mingi kuliko ilivyokuwa kabla ya kugundulika kwa madini hayo.
Akilini mwake, Mwanakwetu aliyafananisha madini kama dhahabu na almasi na embe dodo upande; likiwa bichi huwa kali sana, likiiva nusu huwa tamu na nusu nyingine hubaki chungu.
"Dhahabu ni mithili ya embe dodo upande: nusu tamu, nusu chungu."
Kwa hakika, embe dodo upande hupatikana katika maeneo ya pwani ya Tanzania, kama Lindi, Pwani na Dar es Salaam. Hutofautiana na embe dodo la kawaida ambalo likiwa bichi si kali sana, na likiiva huwa tamu lote. Mwanakwetu alitamani madini kama dhahabu yangeleta faraja kwa wanadamu badala ya kuwa nusu neema na nusu shari.
Mwanakwetu alijiuliza:
"Kazi kubwa ya madini haya, hasa dhahabu, ni nini?"
Dhahabu ni metali adimu yenye thamani kubwa inayotumika katika nyanja kuu nne: kutengeneza vito vya thamani, kuhifadhi utajiri (akiba ya fedha za kigeni), utengenezaji wa vifaa vya kielektroniki kama simu na kompyuta, na katika sekta ya afya, hususan tiba za meno na baadhi ya magonjwa. Hata hivyo, matumizi makubwa zaidi yanakadiriwa kuwa ni kuhifadhi utajiri, yakichukua zaidi ya asilimia 50 ya matumizi yote.
Aidha, baadhi ya matumizi hayo yanaweza kufanywa kwa kutumia vifaa au mbinu nyingine.
Kwa hakika, ukiangalia maeneo mengi yenye dhahabu, mara nyingi hukutana na milio ya bunduki, ving'ora vya polisi, matukio ya mauaji na migogoro ya mara kwa mara. Hata pale panapokuwa na amani, wananchi wengi huvamia migodi kutafuta chembechembe za dhahabu ili waondokane na umaskini, kwa kuwa huamini kuwa kumiliki dhahabu ni njia ya kutoka kwenye umaskini na kuwa tajiri. Wengine hujilaumu kwa kuuza au kuachia maeneo yao kabla ya kugundulika kuwa yana madini.
Swali kuu la makala haya ni hili:
“Je, biashara ya madini ya vito kwa sasa ina tija ya kweli kwa binadamu? Je, tukilinganisha athari zake na zile za biashara ya utumwa, ulinganisho huo utakuwa si wa haki?”
Kwa hakika, biashara ya utumwa ilipigwa marufuku kwa sababu mbalimbali, ikiwemo misingi ya kidini, haki za binadamu, ushawishi wa kisheria na sababu za kiuchumi.
Mwanakwetu anaona kuwa baadhi ya hoja hizo zinafanana na hali ya biashara ya madini ilivyo leo.
Kwa upande wa sheria, maeneo mengi ya madini yamejaa kesi mahakamani, migogoro ya umiliki, malalamiko ya athari za mazingira, pamoja na matukio ya mauaji na matumizi ya nguvu.
Kwa upande wa haki za binadamu, hali kadhalika, kuna mazingira magumu ya kazi, malipo duni na unyonyaji, ilhali madini hayo huuzwa kwa thamani kubwa.
Kwa sababu za kiuchumi, sehemu kubwa ya madini ya vito hutumika kama akiba ya utajiri. Mwenye akiba kubwa ndiye mwenye nguvu zaidi kiuchumi. Mwanakwetu anaona kuwa, endapo biashara hiyo ingebadilishwa na kuelekezwa katika shughuli nyingine zenye manufaa makubwa kwa binadamu, huenda dunia ikapata faida zaidi kuliko kuendelea kulithamini jiwe ambalo binadamu hawezi kulila wala kumwongezea uhai.
Kwa upande wa misimamo ya kidini, Mwanakwetu anasema:
"Kuna wakati nilikuwa kanisani nikisali. Wakati wa matangazo, Katibu wa Parokia alitangaza mafanikio mbalimbali ya parokia. Mojawapo ilikuwa kununua Tabelenakulo ya dhahabu yenye thamani ya takribanikati ya shilingi milioni 11-17.
Kwa wale ambao si Wakatoliki, Tabelenakulo ni sehemu maalumu iliyopo madhabahuni ambapo Ekaristi Takatifu huhifadhiwa baada ya waamini kupokea Komunyo."
Walipotoka kanisani siku hiyo, Mwanakwetu alikuwa na kundi la watu kadhaa. Mjadala ukaibuka kuhusu gharama ya Tabelenakulo hiyo.
Muumini mmoja wao akasema:
"Mimi ningekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Walei, nisingeshauri kununua Tabelenakulo ya dhahabu. Katika dhahabu kuna maswali mengi. Hatujui ilichimbwa kwa mazingira gani, wala ni mateso gani yalihusika kuipata. Kwa hiyo, ningeshauri itumike metali nyingine. Mimi nina mashaka makubwa na dhahabu."
Siku hiyo Mwanakwetu hakuyapa uzito maneno hayo, lakini baada ya tafakari yake ya sasa ameona kuwa ni wazo linalostahili kutafakariwa na Kanisa Katoliki Ulimwenguni.
Kwa hakika, Kanisa hutumia dhahabu katika baadhi ya vyombo vitakatifu vya ibada, kama kalisi, fimbo za maaskofu na mapambo ya baadhi ya mavazi ya viongozi wa Kanisa.
Mwanakwetu anaamini kwamba kama dunia ingeafikiana kwa pamoja kupiga marufuku biashara ya madini ya vito, sehemu kubwa ya dunia ingeweza kuwa salama zaidi.
Kwa mtazamo wake, analifikisha wazo hili kwa viongozi wa dunia, hususan Umoja wa Mataifa, ili walitafakari kwa kina kama walivyofanya wakati wa kupiga marufuku biashara ya utumwa.
Anasema:
"Haya ya sasa ni utumwa wa madini."
Baada ya tafakari hiyo, ndipo Mwanakwetu akaamua kuyaandika makala haya kama yalivyo.
Mwanakwetu upo?
Je makala haya yaitwaje?
“Biashara ya Madini ya Vito ni Utumwa wa Kisasa? Dhahabu: Baraka au Laana kwa Binadamu? Dhahabu: Embe Dodo Upande, Nusu Tamu Nusu Chungu , Madini ya Vito: Utajiri Unaogharimu Amani? Kati ya Dhahabu na Damu: Tafakari ya Mwanakwetu , Je, Dunia Iko Tayari Kupiga Marufuku Biashara ya Madini ya Vito? Madini ya Vito: Wakati wa Kuhoji Manufaa Yake kwa Binadamu , Kutoka Utumwa wa Binadamu Hadi Utumwa wa Madini , Dhahabu na Almasi: Je, Bei Yake ni Maisha ya Binadamu? Madini ya Vito na Hatima ya Ubinadamu.”
Mwanakwetu anachagua Je Dunia Ipo Tayari Kupiga Marufuku Biashara ya Madini ya vito? Wewe msomaji wa Mwanakwetu unachagua kichwa kipi?
Nakutakia siku njema.
Adeladius Makwega
Barua pepe:
Simu: 0717659257
.gif)










.gif)
Post a Comment