HADITHI MBILI, UJUMBE MMOJA

 




 

Adeladius Makwega – Mbagala

 

Jioni ya Julai 14, 2026, Mwanakwetu alikutana na simulizi hii:

 

“Tumefanya maandalizi ya kikao cha Bodi yetu vizuri sana. Majira ya jioni akapiga simu mwenyekiti wa Bodi akasema,

 

‘Jamani ehee, nimeona hapa mna maandalizi ya kikao, yamekamilika. Hongereni sana kwa kazi. Naona ratiba ya kikao inaonesha kitaanza saa mbili kamili na kumalizika saa 10 ya jioni. Sasa jamani, huo mji wenu una mabaridi makali sana (yaani una baridi kali sana), kwa hiyo naagiza kikao kianze saa 5 na kimalizike saa 7 mchana. Mimi nitasafiri kesho hiyo hiyo mapema; nitafika kabla ya saa tano kasoro na kurudi saa saba mchana baada ya kikao kumalizika.

 

Hiyo baridi ya mji wenu siipenda kabisa. Siwezi kusafiri, ati nilale na baridi hiyo kisha niamkie hapo! Nitasafiri ndani ya gari, ninashuka, naingia kikaoni; kutoka zangu narudi huku.’

 

Tukayapokea maagizo haya kama yalivyo, na kweli siku ya kikao cha Bodi hii kilianza saa tano na kumalizika saa saba. Mwenyekiti alishuka katika gari, akaingia kikaoni, na kutoka kikaoni akaingia ndani ya gari na kurudi zake huko alikotoka.”

Mwanakwetu akamwambia huyu jamaa maneno haya:

 

“Kuna wakati mimi nilikuwa mjumbe wa Bodi ya Chuo cha Maendeleo ya Jamii Mabughai, na mwenyekiti wa Bodi hii alikuwa Balozi Injinia Zena Said, ambaye sasa nadhani ni Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia.

 

Mimi nilikuwa naishi Lushoto, na Injinia Zena, ambaye alikuwa Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, yeye alikuwa anatokea Tanga Mjini.

 

Kikao cha Bodi hii mara nyingi kilikuwa kinaanza saa 3 kamili ya asubuhi, lakini saa mbili na nusu wajumbe na mwenyekiti wetu tulikuwa ukumbini; na saa tatu kamili, mshale juu ya alama, tunaanza kikao hicho hadi saa 11 jioni tunamaliza.

 

Ndani ya kikao kulikuwa na ratiba ya siku nzima, saa karibu 9 ndani ya mkutano; kisha kulikuwa na ratiba ya nje, hasa kukagua majengo, mali za taasisi na kuangalia mipaka ya chuo, maana chuo hiki kilikuwa na changamoto ya eneo lao kuvamiwa.

 

Ndani ya kikao tulijadili mambo mengi, moja baada ya lingine, huku jambo mnalolitilia shaka mnalifuatilia kwa kina ili mfanye maamuzi sahihi.

 

Tukiwa kikaoni, mwenyekiti wetu, Balozi Injinia Zena Said, anasema,


‘Kazimbaya Makwega, kaka yangu, toweni na mawazo yenu kwa uhuru kikaoni, maana hawa watumishi wa taasisi wao wanaleta mapendekezo na sisi Bodi ndiyo tunaamua. Naombeni tusikae kimya; kila mmoja nitamuuliza katika hili anashauri nini?’

 

Maamuzi yalifanyika kwa kina kabisa na wajumbe wakiwa wamewahi kikaoni.”

 

Haya, Mwanakwetu anamwambia huyu ndugu aliyemsimulia kisa cha kwanza.

 

Ndugu yule mwenye kisa cha kwanza akasema,

 

“Nyie hongereni. Kumbe hata Tanga, Tanzania, kuna baridi kama huku kwetu?”

 

Mwanakwetu akajibu,


“Lushoto, Tanga, kuna baridi kali sana hasa mwezi Mei, Juni na Julai.”

 

Ndugu mwenye kisa cha kwanza akasema:

 

“Hata hicho kikao chenyewe mwenyekiti alikuwa anaingia na kutoka, anaingia na kutoka. Kwa hakika, hata kama kikao kilifanyika kwa saa mbili badala ya saa zile nane, huyu mwenyekiti hakukitendea haki kikao husika.

Mara achukue maji anywe, mara achukue dawa atoke anywe, mara hiki na kile.

 

Jamani, hizi teuzi zenu angalieni mchague watu wenye afya ya mwili na akili ili waifanyie kazi jamii vizuri; vinginevyo wanakwenda kuwaongezea mizigo badala ya kuishushia jamii mzigo. Mchague mtu kwa kuangalia: je, anaweza kufikiri vizuri? Je, ataweza kupanda ngazi za taasisi na kushuka, siyo anahemahema hovyo?”

 

Mwanakwetu akawa anamsikiliza ndugu huyu, akamalizia kusema haya maneno:

 

“Hawa vijana wanaomaliza shule na vyuo kwa sasa wana akili sana, wamekula mafuta ya samaki vizuri. Tuwe makini tunapochagua watu wa kuwasimamia; vinginevyo hawawezi kukubali kuiacha jamii yao ibaki kama ilivyo.”

 

Jamaa huyu akamalizia kwa haya,

 

“Ngoja nimpokee mgeni, nasikia hodi, maana kuna mwalimu wa tuition wa mwanangu kafika. Kwa heri.”

 

Mwanakwetu alipoagana na ndugu huyu, ndipo akaamua kuyatayarisha makala haya kama yalivyo.

 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

 

Makala haya yanatoa mafunzo muhimu kuhusu uongozi, uwajibikaji, nidhamu ya kazi, na umuhimu wa kufanya maamuzi kwa umakini katika taasisi au jamii.

 

Kwanza, tunajifunza kwamba kiongozi anatakiwa kuwa na dhamira ya kweli ya kusimamia majukumu yake ipasavyo.

 

Cha kusikitisha katika kisa cha kwanza, mwenyekiti wa Bodi alibadili ratiba ya kikao kwa sababu binafsi (baridi), na hata hakushiriki kikamilifu kikaoni. Hii inaonesha ukosefu wa kujitoa na kutoipa kazi uzito unaostahili.

 

Pili, makala haya yanasisitiza umuhimu wa nidhamu na ushiriki kamili katika vikao au kazi yoyote ya umma. Kisa cha pili kinaonyesha mfano mzuri wa uongozi ambapo mwenyekiti na wajumbe walikuwa wanawahi, wanajadili kwa kina, na kila mtu anahusishwa kutoa mawazo. Hii hupelekea maamuzi bora na maendeleo ya taasisi.

 

Tatu, kuna funzo kuhusu uchaguzi wa viongozi wenye uwezo wa kimwili na kiakili. Haifai kuchagua watu kwa vyeo bila kuzingatia afya zao, uwezo wa kufikiri, na utayari wa kufanya kazi. Viongozi dhaifu huongeza matatizo badala ya kuyatatua.

 

Nne, makala haya yanaonyesha kuwa vijana wa sasa wana uwezo mkubwa wa kufikiri na wanatarajia uongozi bora. Hivyo jamii inapaswa kuwa makini kuchagua viongozi watakaoweza kuendana na kasi ya maendeleo na matarajio ya kizazi kipya.

 

Makala haya si ubaguzi wa afya ya mtu wala umri wa mtu, hapana. Watu wenye umri mkubwa tujitathmini wenyewe na afya zetu; lazima tukubali kurudi nyuma kufanya baadhi ya mambo ya umma. Hili litasaidia jamii kupata viongozi sahihi.

 

Kwa ujumla, funzo kuu ni kwamba:


Uongozi bora unahitaji uwajibikaji, nidhamu, ushirikishwaji, na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kwa manufaa ya jamii, si kwa maslahi binafsi.

Makala haya ni maalumu kwa heshima ya Balozi Mhandisi Zena Said, Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia. Pia, kwa hisani yenu naomba Ubalozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia muhitasiri kwa Kiarabu na kisha nakala tatu—Kiswahili, Kiingereza na Kiarabu—zihifadhiwe katika maktaba ya Ubalozi wa Tanzania nchini Saudi.

 

Mwanakwetu upo? Kumbuka:

 

“Hadithi mbili, ujumbe mmoja.”

Ahlaan wa Sahlaan

makwadeladius@gmail.com
0717649257














 

 

0/Post a Comment/Comments