CRDB: Ukiwekeza Lindi, ukakopa Mara... hakuna tatizo!

 



Adeladius Makwega –Musoma MARA TANZANIA.

 

"Ulipo, Tupo."

Huo si msemo wa matangazo tu; kwa Benki ya CRDB unaonekana kutafsiriwa kwa vitendo.

 

"Kwa sasa benki yetu inatoa huduma mbalimbali za mikopo kwa wananchi wanaojihusisha na shughuli tofauti, ikiwamo kilimo na ufugaji. Inawezekana mteja akapatikana CRDB Mara, au tawi lolote nchini, lakini akataka kuwekeza Mkoa wa Lindi.

 

Kwa utaratibu wetu, tawi alipo mteja linaweza kwenda hadi Lindi au eneo lolote nchini kukagua eneo la uwekezaji. Eneo hilo litafanyiwa tathmini ya kina, na baada ya hapo mteja atapatiwa huduma ya mkopo.

 

 Mteja hana ulazima wa kuwasiliana na tawi lililo karibu na eneo la uwekezaji wake; mawasiliano yote yanafanyika kupitia tawi analohudumiwa."

 

Hayo ni maelezo ya Faraja Binti Kaziulaya, Meneja Mwandamizi wa Biashara za Serikali za Mitaa wa Benki ya CRDB Makao Makuu, wakati wa ziara ya viongozi wa benki hiyo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Kanali Evans Alfred Mtambi, Julai 22, 2026.

 

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, aliipongeza Benki ya CRDB kwa namna inavyoendelea kutoa huduma bora kwa wananchi wa Mkoa wa Mara na maeneo mengine nchini kupitia ushirikiano mzuri na viongozi wa serikali pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.

 

"Fursa mnazozitoa zinawanufaisha wananchi wa Mkoa wa Mara. Nawaomba muendelee na kazi hiyo bila kuchoka, hasa hapa Mara ambako tuna fursa nyingi katika kilimo, mifugo, uvuvi, utalii na madini."

CRDB inaendelea kujitambulisha kupitia kaulimbiu zake  kadhaa zinazofahamika kama "Benki Inayomsikiliza Mteja", "Ulipo, Tupo", na "Fueling Prosperity Together."

 

Ujumbe huo unaonekana kuwapa matumaini wengi wanaotamani kuwekeza mbali na walipo. Kwa lugha nyepesi: unaweza kukaa Mara, ukawekeza Lindi, huku mkopo ukikufuata bila kukulazimisha kuhamisha makazi.

 

Ni kama kusema, "ng'ombe wako wako Lindi, lakini mkopo wako unaanzia Mara!"

 

Ugeni wa CRDB katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ulihusisha watumishi wanne; wanawake wawili na wanaume wawili.

Naye mwandishi wa makala haya hawakuondoka mikono mitupu. Mwanakwetu aliyefuatilia tukio hilo alipata nafasi ya kubadilishana mawasiliano na Binti Kaziulaya, jambo lililompa hamasa ya kuchunguza kwa karibu fursa mbalimbali za uwekezaji zilizojadiliwa katika kikao hicho.

 

Sasa anajiandaa kuwasiliana naye kwa lengo la kuanza safari yake ya uwekezaji.

Hapo mwandishi wa makala haya akimaliza kuwasiliana na Faraja Kaziulaya akipata jibu ataeleza uwekezaji wake ni katika nini na mkoa gani ili jamii ya Watanzania ijifunze kutoka CRDB na ndipo atakapopata jibu la swali ambalo wengi hujiuliza:

Je, kweli CRDB ni Benki Inayomsikiliza Mteja?

 

Kwa kuwa Bi. Faraja Kaziulaya ndiye anayesimamia biashara za Serikali za Mitaa, huenda ndiye mwenye majibu ya swali hilo.

Mwanakwetu upo?Kumbuka,

“Ukiwekeza Lindi, ukakopa Mara... hakuna tatizo!-CRDB.”

 

Nakutakia Siku Njema

makwadeladius@gmail.com
Simu: 0717 649 257









 

 

 

0/Post a Comment/Comments