BAISKELI YA BABA NA NDOTO YA MWANA

 


Adeladius Makwega – Musoma, MARA, TANZANIA.

Ilikuwa ni Julai 16, 2026, ambapo siku iliyotangulia kulikuwa na mechi ya kukata na shoka ya Kombe la Dunia la Mpira wa Miguu baina ya Argentina na Uingereza. Uingereza iliongoza kwa bao moja hadi dakika ya 84. Baadaye, Argentina walitoa usingizini na kuzinduka kama mgonjwa aliyepigwa nusu kaputi. Dakika ya 85, Enzo Fernandez alilisalimu lango la Uingereza, na dakika tano baadaye, likafungwa bao la pili dakika ya 90+2 na Lauretazo Martezeee. Kwa ushindi huo, Argentina waliingia fainali.

 

Mjadala ofisini ulikuwa ni kuhusu mechi hii. Wapo waliosema kuwa Uingereza ilifanya makosa makubwa; wengine wakisema Uingereza inaweza mpira wa TV na propaganda tu.

Mdau mmoja akaingia huku akisema kuwa,

 

“Jamani, kuna mtoto wa jirani amechaguliwa kidato cha tano, Shule ya Sekondari Tosamaganga (tupamawe). Ni mbali sana, na nauli za kwenda na kurudi ni kubwa.”

 

 

Mdau mwingine akasema, “Tosamaganga ni shule nzuri. Acha tu na kusoma; bali mtoto anapokwenda kujifunza mbali na nyumbani, kuna mambo mapya lazima atajifunza, ambalo nalo ni elimu tosha.”

Ndugu Leonard Lameck Mkaruka akasema:

“Jamani, nakubaliana na nyinyi juu ya kutembea ni muhimu sana ili tuweze kujifunza. Mimi, marehemu baba yangu akiwa kijana, alitembelea ofisi ya NPF mwaka 1977, ambayo baadaye ikaja kuwa NSSF, mfuko wa jamii. Baba akiwa katika ofisi ya taasisi hii alihudumiwa na afisa mkubwa mlemavu. Hapo hapo mzee alibaini kuwa kumbe hata walemavu wanaweza kusoma na kushika nafasi yoyote katika jamii; kikubwa ni kuwawekea mazingira mazuri ya kusoma tu.”

Mjadala hapa ofisini ukapamba moto. Ndugu Mkaruka akasema:

 

“Unajua, sasa hivi baiskeli za walemavu zinapatikana, lakini zamani ilikuwa ngumu hata kupata. Mathalani, mimi nakumbuka baba aliagiza baiskeli yangu mwaka wa 1978, nikiwa darasa la kwanza, pale siku alipotoka ofisi za NPF. Kweli nilianza masomo Shule ya Msingi Kotwo, ambayo ilikuwa Wilaya ya Tarime, sasa ni Wilaya ya Rorya mkoani Mara, na baiskeli ilinifikia mwaka 1982 nikiwa darasa la tano, shuleni hapo hapo.”

Wadau wakauliza, “Sasa Leonard Lameck Mkaruka, ulikuwa unaendaje shuleni ukiwa na ulemavu wakati baiskeli awali ulikuwa hauna?”

 

“Tangu mwaka 1978 hadi mwaka 1982, marehemu baba yangu Lameck Mkaruka, ambaye alikuwa Bwana Shamba, alikodisha baiskeli ya miguu miwili kwa mwanakijiji mmoja ambaye alikuwa na jukumu la kunibeba kila siku kwenda na kurudi nyumbani kutoka Kijiji cha Kiterere, umbali wa KM 10.”

 

Wadau katika ofisi hii wakasema, “Kweli, ukitembea unajifunza mengi.”

“Unajua, baiskeli ile baba alinunua kwa shilingi 1600 za Kitanzania, ambayo ilikuwa pesa nyingi sana, na baiskeli hii nimeitumia tangu mwaka 1982 hadi nafika chuo, na nimeiacha kuitumia baada ya kununua bajaji yangu mwenyewe.”

Wadau walimuuliza ndugu Leonard Lameck Mkaruka, “Naona baba yako atakuwa anapata raha sana.”

Majibu yalikuwa haya:

 

“Cha kusikitisha, baba yangu alifariki nikiwa kidato cha nne mwaka 1988, nikiwa Musoma Sekondari, na hata mshahara wangu baba hakuweza kuula kabisa. Lakini kama angekuwa hai, kwa hakika hili lisingalikuwa jambo la mjadala wowote ule.”

 

Baadaye, katika ofisi hii aliingia kiongozi mmoja, na mjadala ukafa muda huo huo.

Mwanakwetu anasema nini?

Simulizi hii ina mafunzo mazito sana—hasa kwa ulimwengu wa walemavu (watu wenye ulemavu), lakini pia kwa jamii kwa ujumla.

Mosi, ulemavu si mwisho wa mafanikio.
Hadithi ya baba wa ndugu Leonard kuonana na afisa mkubwa mlemavu kazini ilibadilisha kabisa mtazamo wake.
Funzo: Watu wenye ulemavu wana uwezo wa kusoma, kufanya kazi, na kushika nafasi kubwa. Kizuizi kikubwa si ulemavu—bali ni mitazamo ya jamii.

 

Pili, mazingira bora huwezesha mafanikio.
Baba alihakikisha mtoto wake anafika shule kila siku hata kwa kumkodishia mtu wa kumbeba umbali wa KM 10.
Funzo: Watu wenye ulemavu wakipewa msaada sahihi (miundombinu, vifaa, usafiri) wanaweza kufikia ndoto zao. Elimu jumuishi (inclusive education) ni muhimu sana.

Tatu, jitihada na uvumilivu huzaa matunda.
Kutoka kubebwa na baiskeli ya kukodi hadi kununua bajaji yake mwenyewe—hii ni safari ya mafanikio.
Funzo: Mafanikio hayaji kwa urahisi, bali kwa subira, juhudi, na msaada wa jamii/familia. Ulemavu hauzuii mtu kujitegemea baadaye.

Nne, nafasi ya familia ni kubwa sana.
Baba alijitoa kwa hali na mali kuhakikisha mtoto wake anasoma.
Funzo: Familia inaweza kuwa nguzo kuu ya mafanikio kwa mtu mwenye ulemavu. Upendo na uwekezaji wa wazazi hubadilisha maisha.

Tano, mitazamo ya jamii inahitaji kubadilika.
Mjadala ofisini unaonyesha jinsi watu wanavyojifunza kupitia hadithi halisi.
Funzo: Jamii inapaswa kuacha kudharau uwezo wa walemavu. Badala yake, iwape nafasi sawa na kuwaunga mkono.

 

Sita, “Kutembea ni Kujifunza” – maana pana.
Kauli hii ina maana zaidi ya kusafiri kimwili.
Funzo: Kujifunza kunatokana na uzoefu wa maisha. Kukutana na watu tofauti (kama yule afisa mlemavu) kunaweza kubadilisha kabisa fikra na mwelekeo wa maisha.

Mwanakwetu upo? Kumbuka:

“Baiskeli ya Baba na Ndoto ya Mwana”

Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649357













 

 

0/Post a Comment/Comments