Adeladius Makwega – Mbagala
Leo ni Sikukuu ya Mwili na Damu Takatifu Sana ya Kristo. Katika Injili kulingana na Mtakatifu Yohane, Bwana mwenyewe anatufundisha yale ambayo Mwili na Damu yake hutupatia.
Anasema: “Yeyote aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele, nami nitamfufua siku ya mwisho.”Hii ina maana kwamba tunapoula Mwili wake na kuinywa Damu yake, tunashiriki uzima wake wa milele.
Tena asema: “Yeyote aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake.” njia ya Mwili na Damu yake, tumepewa fursa ya kipekee ya kuwa katika ushirika wa karibu na Yesu pamoja na Baba.
Ndugu zangu wapendwa, tunaukaribiaje Mwili na Damu ya Bwana katika Komunyo Takatifu? Je, tunautazamia uzima wa milele pamoja na Mungu? Je, tunafurahia kuunganishwa naye?
Hizi ndizo zawadi kuu za Mwili na Damu ya Yesu. Basi na tugundue upya uzuri na kina cha fumbo hili, ili tuweze kuishi milele katika ushirika na Mungu.
Katika tafakari ya siku hii, Kardinali Luis Antonio Tagle wa Vatican alisisitiza umuhimu wa fumbo hili la Ekaristi Takatifu kama chanzo cha uzima wa milele na umoja wa waamini ulimwenguni.
Hapa nyumbani Tanzania, katika Parokia ya Mtakatifu Augustine – Mwisenge, Jimbo Katoliki la Musoma, Padri Julius Ogolla alikumbusha waamini umuhimu wa kujiandaa kiroho kabla ya kumpokea Yesu katika Ekaristi Takatifu. Alisisitiza usafi wa roho na moyo safi, akisema:
“Mwili na Damu ya Yesu ni chakula cha uzima. Ni ishara ya upendo wake mkuu—upendo aliouonesha kwa kujitoa sadaka kwa ajili yetu ili tufike mbinguni.”
Kutokana na Sikukuu hii, Mwanakwetu ameandaa utenzi mfupi wa tafakari:
Leo ni siku tukufu, ya neema isiyopimwa, Mwili na Damu yake, zawadi tuliyopewa, Kristo atufundisha, kwa sauti yenye huruma, Uzima wa milele, ndani yake twaupata.
Asema kwa upole, yeyote atakayekula, Mwili wangu na damu, kwa imani akinywa, Atapata uzima, usio na kikomo, Nitamfufua tena, siku ile ya mwisho.
Tena anatufunza, siri kuu ya upendo,Tukila na kunywa, tunaingia ushirika, Yeye hukaa ndani, nasi ndani yake pia, Pamoja na Baba, twafanywa familia.
Basi ndugu wapendwa, tuyatafakari haya,Komunyo Takatifu, tuikaribie kwa moyo,
Uzuri wa fumbo hili, tuujue pasipo shaka,Ili tuishi milele, na Mungu wetu daima.
Aidha, katika safari yangu ya kwenda kusali Dominika hii (Juni 7, 2026), nilikutana na tafakari nyingine ya maisha ya kawaida. Niliona waamini wengi wakielekea kanisani, ingawa baadhi walikuwa wamechelewa kama mimi.
Njiani, nilisikia mazungumzo ya mama na binti yake kuhusu changamoto za usalama wakati wa ibada za alfajiri. Tukio la Mama Sangula lililotajwa—aliyekumbana na hatari lakini akaokolewa karibu na geti la parokia—linatukumbusha umuhimu wa kuwa na umoja na ulinzi katika jamii.
Mazungumzo hayo pia yaligusia hali ya makaburi—mahali pa kupumzika wapendwa wetu. Ni wito wa kuyatunza na kuyaheshimu, kwani hata katika imani yetu, tunatarajia ufufuo wa wafu.
Nakumbuka enzi za zamani Mbagala, waamini walikuwa wakikusanyika kusafisha makaburi kwa pamoja, hasa wakati wa Ijumaa Kuu. Ilikuwa ni ishara ya imani, mshikamano na matumaini ya uzima wa milele.
Je, leo bado tunadumisha roho hiyo?
Mwanakwetu upo? Tafakari:
Zawadi ya Uzima wa Milele.
Nakutakia siku njema.
Email: makwadeladius@gmail.com
Simu: 0717 649 257
.gif)
.gif)








Post a Comment