Adeladius Makwega, Musoma - Mara
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Ndugu Eliakim Chacha Maswi, amesema kuwa watumishi wa umma wanapaswa kujiendeleza kitaaluma kwa wakati ili mabadiliko na maendeleo yanapotokea katika taasisi zao, wakute wakiwa na sifa stahiki za kupanda madaraja na kushika nafasi mbalimbali za uongozi.
Akizungumza Juni 5, 2026, katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare mkoani Mara, ndugu Maswi alisema:
“Nimedokezwa kuwa mnakaribia kupanda ngazi na kuungana na Tengeru pamoja na kuanzisha programu ya Shahada ya Maendeleo ya Jamii. Haya yote ni mambo mazuri. Nawaomba mjitahidi kujiendeleza ili muwe na sifa zinazohitajika. Isiishie kuwa tunaanzisha shahada halafu nafasi hizo zinajazwa na watumishi wapya pekee; na nyinyi pia jiendelezeni ili mnufaike na fursa hizo.”
Ndugu Maswi alisema kuwa ziara yake katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare, ambacho kina miaka 60 tangu kuanzishwa kwake, imelenga kutambua mchango wake mkubwa katika kuzalisha wataalamu wengi nchini Tanzania na kuimarisha ustawi wa wananchi katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Awali, katika kikao cha ndani na viongozi wa chuo hicho, ndugu Maswi alitoa shilingi milioni 10 kwa ajili ya ukarabati wa gari la kubebea wanafunzi wagonjwa kwenda hospitalini wakati wa dharura, baada ya kubainika kuwa lilikuwa na hitilafu.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Ndugu Humphrey Kong’oke, alimshukuru Katibu Mkuu Maswi kwa kutembelea mkoa huo. Alisema Mkoa wa Mara unanufaika kwa kiasi kikubwa na uwepo wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare, ambacho hupokea karibu wanafunzi 1,000 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania pamoja na nchi jirani kila mwaka.
Awali, akisoma risala ya chuo hicho, Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare, Ndugu Pascal Joseph Mahinyila, alisema:
“Chuo chetu kinakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwamo uhaba wa miundombinu. Idadi ya waombaji wa kujiunga na chuo ni kubwa kuliko uwezo wetu wa kuwapokea. Changamoto kubwa zaidi ni uhaba wa mabweni na vyumba vya madarasa.”
Katika ziara hiyo, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara aliambatana na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Stanley Kajuna; Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya Jamii na Afisa Vijana wa Mkoa wa Mara, Fidel Balaghaye; Afisa Maendeleo ya Jamii, Upendo Kiswaga; Afisa Ustawi wa Jamii, Elizabeth Mahinya; pamoja na Afisa Ustawi wa Jamii, Sofia Kiwanga.
Wakati shughuli hizo zikiendelea, hali ya hewa katika Mji wa Musoma ilikuwa nyuzi joto 28 , unyevunyevu wa hewa ukiwa asilimia 60, uwezekano wa mvua asilimia 55, huku upepo ukivuma kwa kasi ya kilomita 10 kwa saa.
makwadeladius@gmail.com
0717 649 257
Post a Comment