WANYABASI – WANYAMONGO WAUNGANISHWA NA DARAJA

 




Adeladius Makwega – Tarime, Mara, Tanzania

 

Ni majira ya asubuhi ya Juni 22, 2026. Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Mara, ikiongozwa na Komredi Patrick Chandi ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, ilifika Wilayani Tarime na kukagua miradi kadhaa ya maendeleo. Wilaya hii ina utajiri mkubwa wa madini ya dhahabu.

 

Katika ziara hiyo, walipokelewa na msururu wa maduka 35 yaliyojengwa kwa thamani ya shilingi milioni 395 chini ya usimamizi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime.

 

“Hii ni kazi nzuri. Ninawapongeza sana kwa kazi kubwa mliyofanya, kuanzia kubuni hadi kukamilisha mradi huu. CCM imeupenda mradi huu—hongereni sana,” alisema Ndugu Chandi.

 

Kauli hiyo ilitolewa mbele ya Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Dkt. Zabroni Masatu, pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele.

 

Baada ya hapo, ziara iliendelea kwa kukagua miradi mingine mitatu ndani ya wilaya hiyo.

Miradi miwili ilikuwa na ufanano, ambayo ni majengo ya utawala ya shule mbili za sekondari, ikiwemo Shule ya Sekondari Mjini Kati. Jengo hilo lilijengwa kupitia fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kutoka Mgodi wa North Mara kwa gharama ya shilingi milioni 172.

 

Baada ya kusomewa taarifa ya mradi huo, Ndugu Chandi alikagua na kusema:

 

“Huu mradi ni mzuri na unaendana na hadhi ya CCM na nafasi yangu kama Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara. Hongereni sana wenyeviti wa vijiji, madiwani, viongozi, na wananchi wote wa wilaya hii.”

 

Wakati wa ziara hiyo, ilibainika kuwa Shule ya Sekondari Mjini Kati haina umeme. Hapo hapo, CCM Mkoa wa Mara ilitoa agizo:

 

“Natoa siku thelathini kuanzia leo, umeme uwe umefika katika shule hii.”

 

Mradi mwingine unaofanana na huo ni jengo la utawala la Shule ya Sekondari Matongo, ambalo pia linajengwa kwa fedha za CSR kutoka Mgodi wa North Mara kwa gharama ya shilingi milioni 172. CCM ilivutiwa na mradi huo na kutoa pongezi nyingi.

 

Sehemu ya kuvutia zaidi katika ziara hiyo ilikuwa ni ukaguzi wa daraja lenye urefu wa mita 41.5, linalowaunganisha makabila mawili yaliyokuwa maadui kwa muda mrefu—Wanyabasi na Wanyamongo.

Historia inaeleza kuwa makabila haya yalitenganishwa na Mto Tigite, na hakukuwa na mahusiano ya kijamii kama kuoana wala kuvukana kutoka upande mmoja kwenda mwingine.

 

Sasa, daraja la Mto Tigite limejengwa na TARURA, na kuleta umoja na udugu. Hapo awali, waliovuka kwa siri walitumia kamba, jambo lililochochea uadui na kuzuia mshikamano.

 

“Daraja hili limejengwa na kusimamiwa na TARURA kwa gharama ya shilingi milioni 400. Nina imani Wanyamongo na Wanyabasi sasa mtaoana, mtalima pamoja, mtachunga pamoja na kuishi kwa amani,” alisema Ndugu Chandi huku akishangiliwa na wananchi waliokusanyika katika gulio jirani na daraja hilo.

 

Mwanakwetu anasema nini leo?

Huu ni muhtasari wa makala ya ziara ya Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Mara katika Wilaya ya Tarime, Juni 22, 2026.

 

Wakati huo, hali ya hewa katika Mji wa Tarime ilikuwa nyuzi joto 27, unyevunyevu asilimia 10, uwezekano wa mvua asilimia 46, na upepo ukivuma kwa kasi ya kilomita 5 kwa saa.

Mwanakwetu upo? Kumbuka:

 “Wanyabasi – Wanyamongo Waunganishwa na Daraja.”

Nakutakia siku njema.

 

Barua pepe: makwadeladius@gmail.com

Simu: 0717 649257








 

 

 

0/Post a Comment/Comments