.gif)
Adeladius Makwega – Makundusi, Serengeti, Mara
Juni 2, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, pamoja na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, ndugu Gerald Musabila Kusaya, viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Serengeti na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mara, walifanya mkutano mkubwa katika Kijiji cha Makundusi. Wananchi kutoka vijiji saba vya kata za Natta, Kyambahi na Ikoma walishiriki katika mkutano huo.
Baada ya kikao kilichodumu kwa takribani saa sita, maamuzi ya Serikali kuhusu uwekaji wa fensi kando ya vijiji yalitangazwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi.
Akizungumza katika mkutano huo, Kanali Mtambi alisema:
“Serikali ya Mkoa wa Mara ilipokea hitaji la kuchukua hatua mahususi za kuhakikisha wananchi wanakuwa salama katika maeneo yanayopakana na hifadhi zenye wanyama wakali. Serikali Kuu na Serikali ya Mkoa kwa pamoja zimechukua hatua mbalimbali, na hatua zaidi zinaendelea kuchukuliwa ili kutatua changamoto hizi.”
Kanali Mtambi alieleza kuwa tatizo hilo limekuwa kubwa kutokana na sababu kuu mbili:
“Kimsingi, Mkoa wa Mara, kama ilivyo kwa mikoa mingine yenye wanyama wakali, unakabiliwa na changamoto inayosababishwa na ongezeko la wanyama pamoja na ongezeko la idadi ya watu. Kadiri idadi ya watu inavyoongezeka, ndivyo wanavyosogea karibu zaidi na hifadhi. Ili kukabiliana na hali hiyo, hatua mbalimbali zimechukuliwa za muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu.”
Akizitaja hatua hizo, alisema kuwa hatua za muda mfupi ni pamoja na kutumia maafisa wanyamapori kuwalinda wananchi katika maeneo yenye changamoto za wanyama hatarishi, kutoa elimu ya namna ya kukabiliana na wanyama wakali, na kushirikiana na wadau mbalimbali katika juhudi za kupunguza madhara hayo, ikiwemo matumizi ya ndege nyuki.
Aidha, alisema kuwa katika maeneo kadhaa, kwa kushirikiana na wawekezaji na wadau wengine, fensi zimewekwa, huku maeneo mengine yakiwa katika mpango wa kuwekewa uzio. Mpango huo unahusisha vijiji vilivyopo ndani ya kilomita 30 katika awamu ya kwanza na kilomita 35 katika awamu ya pili.
Kanali Mtambi alisema kuwa hapo awali kulikuwa na sintofahamu kuhusu vijiji sita vinavyopitiwa na mradi huo pamoja na kijiji kimoja kilichoomba kujumuishwa ili fensi ipite katika eneo lake kutokana na changamoto ya wanyama wakali.
Aliongeza kuwa:
“Fensi ni suluhisho muhimu la kupunguza madhara yanayosababishwa na wanyama hatarishi, lakini siyo suluhisho la asilimia mia moja. Baadhi ya wanyama, hasa wa jamii ya paka, wataendelea kusababisha madhara hata baada ya fensi kuwekwa.”
Alisema kuwa hatua nyingine zinazochukuliwa ni pamoja na kuendelea kutumia wataalamu, kuimarisha vituo vya wanyamapori, kuongeza magari ya doria, kusimika fensi na kutumia ndege nyuki. Lengo la hatua hizo zote ni kupunguza tatizo hilo kwa kiwango kikubwa.
Kanali Mtambi aliwaeleza wananchi kuwa katika vijiji hivyo kuna makundi mawili makuu ya shughuli za kiuchumi, ambayo ni wakulima na wafugaji. Alisema kuwa baadhi ya wafugaji hawataki maeneo yao ya malisho yaguswe na fensi, wakati wakulima wanapendelea fensi ipite katika maeneo hayo.
Kwa mujibu wa maelezo ya kitaalamu Kanali Mtambi alisema kuna sababu mbili zinazofanya fensi ipite katika baadhi ya maeneo. Sababu ya kwanza ni ya kiikolojia, kwani baadhi ya maeneo yakiachwa nje ya fensi yatazuia njia za asili zinazotumiwa na wanyamapori kuhama kutoka eneo moja kwenda jingine. Sababu ya pili ni kwamba fensi ikisimikwa tofauti na mpango wa wataalamu inaweza kuathiri upatikanaji wa vyanzo vya maji kwa wanyamapori.
Akiendelea kueleza maamuzi ya Serikali ya Mkoa wa Mara, Kanali Mtambi alisema kuwa hadi Juni 2, 2026, ni vijiji viwili pekee ambavyo havikutaka maeneo yao ya malisho yapitiwe na fensi.
Alisema kuwa hoja za wananchi hao ni pamoja na hofu ya kupokonywa maeneo yao ya malisho, hususani kwa wafugaji. Hoja nyingine ni kwamba endapo mifugo itaruhusiwa kupita katika mageti maalumu ya fensi, kuna uwezekano wa wanyama wakali kuwafukuza mifugo na wachungaji, huku fensi ikiwa kikwazo cha kuwakimbia wanyama hao. Hoja ya tatu ni ugumu wa kutafuta mifugo inayopotea, kwani shughuli hiyo mara nyingi hufanyika hadi usiku wa manane.
Akihitimisha maamuzi ya Serikali, Kanali Mtambi alisema:
“Kwa vijiji vya Motukeri, Bokole, Nyichoka, Natambiso na Nyanungu, usimikaji wa fensi ya kuzuia wanyama uanze mara moja. Kwa vijiji vya Makundusi na Pakinyigoti, mikutano ya wataalamu kutoka pande zote iharakishwe kuanza ili maamuzi sahihi yafanyike baada ya vikao hivyo kukamilika.”
makwadeladius@gmail.com
0717 649 257








.gif)
Post a Comment