USALAMA WA KILA MMOJA WETU UKO HATARINI

 



Adeladius Makwega – MBAGALA

 

Juni 27, 2026, Mwanakwetu alikutana na taswira ya vijana wakishiriki michezo. Katika taswira hii, kijana mmoja ambaye nadhani alikuwa mgambo alikuwa amevalia sare za michezo na yeye anashiriki michezo kwa pembeni. Katika kushiriki michezo huko, akawa anaipandisha suruali ya tracksuit yake kwa kuwa ilikuwa imeshika kidogo. Wakati anafanya hivyo, ikaonekana kuwa kiunoni mwake ameweka pingu.

 

Mwanakwetu akasema kimoyomoyo:


“Huyu ni auxiliary polisi. Huyu anaamini hata hapa kunaweza kutokea vurugu, na kwa haraka anaweza kumdhibiti yeyote atakayefanya vurugu.”

 

Michezo ikaendelea kufanyika.

 

Baadaye, pembeni ya eneo hili, wakapita vijana wa polisi. Mara yanapita magari ya polisi wenye silaha; wanaenda, wanarudi, tofauti tofauti.

 

Baadaye, Mwanakwetu alibaini kuwa eneo hili lilikuwa na taasisi zote za vyombo vya ulinzi isipokuwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) peke yao.

 

Kimoyomoyo, Mwanakwetu akasema:


“Katika kundi la watu 500 wakikusanyika, lazima askari wa JWTZ atakuwepo, pengine amevaa kiraia tu.”

 

Hawa askari polisi walikuwa wakipita sana—wengine na virungu, wengine na bunduki. Muda mwingine magari yao yanapita kwa kasi. Akilini, Mwanakwetu anawawaza ndugu zake polisi, akisema:

 

“Wanawahi pahala kulinda au kuna pahala hapako salama?”

 

Mwanakwetu akiwa hapo, alitafakari kazi ya vifaa vifuatavyo kwa polisi: pingu, kirungu na bunduki ni nini?

 

Aliyatafuta majibu kwa kina, na haya yalikuwa baadhi ya hayo:

 

“Pingu za polisi ni kifaa maalum kinachotumika kuwafunga mikono watu (hasa watuhumiwa au wahalifu) ili kuwazuia kufanya harakati hatarishi. Kazi kuu ya pingu za polisi ni kuzuia mtuhumiwa kutoroka. Hufunga mikono ili mtu asiweze kukimbia au kujinasua kirahisi. Husaidia polisi kumdhibiti mtu anayehatarisha usalama wa wengine au wa polisi wenyewe. Mtuhumiwa anapopelekwa kituo cha polisi au mahakamani, pingu husaidia kuhakikisha anasafirishwa bila matatizo. Pia kifaa hiki kinaaminika kupunguza uwezekano wa mtuhumiwa kujiumiza au kuumiza watu wengine. Kwa ujumla, pingu ni zana ya usalama na udhibiti. Wanaoamini hilo wanasema pingu si adhabu, bali hutumika wakati wa kukamata au kushikilia mtu kwa mujibu wa sheria.”

 

Kumbuka, Mwanakwetu anatazama michezo huku akitafakari kifaa kingine cha polisi nacho ni kirungu:

 

“Kirungu cha polisi ni fimbo maalum (kifaa) ambacho askari polisi hubeba na kutumia katika kazi zao za ulinzi na usalama. Kirungu ni fimbo fupi na ngumu. Polisi hutumia kirungu kama chombo cha kudhibiti watu, kujilinda au kusimamia utulivu wakati wa kazi. Kwa lugha rahisi: kirungu cha polisi ni fimbo ya kujilinda na kudhibiti hali hatarishi. Hiki ni moja ya vifaa vya kawaida vinavyotumiwa na polisi pamoja na vifaa vingine vya kazi zao.”

 

Mwanakwetu anaendelea kuangalia michezo hiyo huku mtoano ukiendelea, magari ya polisi yanaenda na kurudi, vijana wa polisi wapo juu ya mabomba na magari ya wazi.

Mwanakwetu akisema hawa vijana wa polisi wanaweza kuanguka katika mabomba ya magari yao maana magari ya polisi yanakimbizwa sana maana hata polisi nao ni binadamu.

Polisi wengine wanapita kwa bodaboda na wengine kwa miguu nayo tafakari ya Mwanakwetu inaendelea kusonga.

 

Kifaa kingine kilichokumbukwa ni bunduki:

 

“Kazi ya bunduki kwa polisi ni kusaidia katika ulinzi na usalama wa raia, lakini hutumika kwa uangalifu mkubwa na si kwa matumizi holela. Bunduki hutumika kujilinda askari au wananchi pale kunapokuwa na hatari kubwa. Hutumika kudhibiti wahalifu hatari (mfano majambazi wenye silaha). Husaidia kukamata wahalifu kwa kupunguza nguvu zao, si lazima kuwaua.

Muhimu kuelewa: kazi ya bunduki si kuua moja kwa moja, bali kusaidia polisi kufanikisha usalama na ukamataji wa wahalifu. Matumizi yake yanafuata sheria na taratibu maalum ili kuepuka madhara kwa watu wasiokuwa na hatia. Bunduki ya polisi ni chombo cha mwisho kinachotumika wakati wa hali ya hatari sana ili kulinda maisha na kudhibiti uhalifu.”

 

Vifaa vingine vya polisi ni gesi ya machozi, ambayo hutumika kuwatawanya umati au vurugu.

 

Pia ipo redio ya mawasiliano; kazi yake kubwa ni kuwasiliana na askari wengine. Kifaa kingine ni kinga, ambacho hutumika kujilinda dhidi ya mawe au mashambulizi.

Lengo la kinga ni kusaidia udhibiti, lengo la redio ni mawasiliano, na usalama. Kirungu kinatumika kama nguvu ndogo (kudhibiti), na bunduki hutumika kama nguvu kubwa (hali hatari sana).

 

Msomaji wangu, kumbuka Mwanakwetu anayatafakari haya huku akitazama michezo hiyo.

 

Harakati za magari ya polisi zinaendelea.

 

Mwanakwetu akiwa hapo akatafakari kuwa jukumu la vifaa hivyo vyote ni kumlinda raia—yaani mimi, wewe na yule—ili asionewe na mhalifu yeyote yule. Ndiyo maana Jeshi la Polisi hulinda usalama wa raia na mali zao, Jeshi la Wananchi Tanzania hulinda mipaka, na hata ndugu zetu wa Usalama wa Taifa hulinda usalama wa nchi, si usalama wa mtu mmoja mmoja.

 

Mwanakwetu akajisemea mwenyewe:


“Hapa katika michezo panaweza pakatokea vurugu ambayo inaweza kusababisha madhara kwa mtu yeyote bila kujali wadhifa wake. Silaha husika—iwe kirungu, bomu la machozi au bunduki—ina wajibu wa kumdhibiti mhusika ili kurejesha amani.”

 

Mwanakwetu aliwaza kuwa kama hakuna umakini wa watumiaji wa vifaa hivi, mwisho wa siku silaha hizi zinaweza kuwarudia wao wenyewe. Ili kulinda heshima ya jukumu lao kwa taifa, lazima vifaa hivyo vitumike vizuri.

 

Mwanakwetu alitazama michezo hiyo hadi mwisho, kisha akarudi zake. Akiwa nyumbani ndipo akaamua kuyaandaa makala haya.

 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

 

Askari wetu wanaofanya kazi na vyombo vya ulinzi na usalama lazima watambue kuwa kama kuna matumizi mabaya ya vifaa hivyo, wasidhani wao wako salama. Wanaishi katika dunia hii hii yenye matumizi mazuri au mabaya ya vifaa hivyo. Kama kuna matumizi sahihi, watakuwa salama; lakini kama kuna matumizi mabaya dhidi ya yeyote yule, hata kama ni mdogo kiasi gani, silaha hiyo hiyo inaweza kutumika vibaya hata dhidi yao wenyewe—iwe bado wanahudumu au wamestaafu.

 

Hili ni jambo la msingi sana ndugu zetu wanaofanya kazi katika vyombo hivi wanapaswa kulifahamu na Mwanakwetu anaomba Mungu makala haya kila mmoja wetu aisome kwa umakini mkubwa.

 

Watanzania, tusisahau katika hili kisa cha mfano ni mauaji ya Brigedia Jenerali Imran Kombe, Juni 30, 1996, miezi michache baada ya kustaafu.

 

“Imran Hussein Kombe alikuwa afisa wa jeshi na ujasusi wa Tanzania. Wakati wa Vita vya Uganda na Tanzania vya mwaka 1979, aliongoza Brigedi ya 201 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (TPDF) katika uvamizi wa Uganda. Kuanzia mwaka 1980 hadi 1983, alihudumu kama Mkuu wa Wafanyakazi Jeshini (Chief of Staff) wa TPDF, kabla ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Usalama na Ujasusi ya Tanzania. Alishikilia wadhifa huo hadi mwaka 1995. Alipigwa risasi na kuuawa na polisi mwaka uliofuata, baada ya kudhaniwa kuwa alikuwa mwizi wa gari.”

 

Imran Kombe alikuwa Brigedia Jenerali wa JWTZ. Isitoshe, alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa—vyeo vya juu kabisa nchini Tanzania.

 

Kiroja ni kwamba askari waliomfyatulia risasi walitoka Kituo cha Polisi Oyster Bay na siyo kituo cha polisi Marangu ambapo kilikuwa kituo jirani na makao makuu ya idara hiyo.

 

Msomaji wangu, fahamu kuwa cheo cha Brigedia Jenerali ni cha juu jeshini. Kipo juu ya Kanali (Colonel) na chini ya Meja Jenerali (Major General). Mara nyingi hupewa maafisa wenye uzoefu mkubwa.

 

Kwa kifupi: Imran Kombe alikuwa kiongozi wa juu wa kijeshi nchini Tanzania, lakini aliuawa na askari polisi kwa kumfananisha na jambazi.

 

Ndugu zangu Watanzania ndugu yenu Mwanakwetu wa Mbagala naongea nanyi,

 

“Matumizi sahihi ya silaha ni jambo muhimu sana, maana uwezo wa silaha unatofautiana: huyu ana kirungu, huyu ana bomu la machozi, huyu ana bunduki ya kawaida, mwingine ana submachine gun, na mwingine ana nyuklia.Mwenye mali ya hiyo (silaha) ni Watanzania lazima walindwe.

Hata, ukiwa na nguvu za kupigana kwa mwili, atakuja mwenye kirungu. Ukiwa na kirungu, atakuja mwenye bomu la machozi. Ukiwa na bomu la machozi, atakuja mwenye bunduki ya kawaida. Ukiwa na bunduki ya kawaida, atakuja mwenye submachine gun. Ukiwa na submachine gun, atakuja mwenye mabomu mazito. Ukiwa na mabomu mazito, atakuja mwenye nyuklia. Ukiwa na nyuklia moja, atakuja mwenye nyuklia nyingi. Maana yake, ukiwa na silaha yoyote ile na usitumie kwa haki, mwisho wa siku utateketea, maana yupo aliyekuzidi.”

 

Mwanakwetu anashauri viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama wawashauri viongozi wetu kwa haki, wasiwaogope, wasiangalie fedha, wasiangalie vyeo vyao haya ya kupitia tu. Na mkiwaogopa, usalama wa kila Mtanzania unakuwa mdogo. Narudia: usalama wa kila Mtanzania uko hatarini.

 

Mwanakwetu upo? Kumbuka:

Nani Kama Imrani Kombe?

“Mkiwaogopa, usalama wa kila Mtanzania uko hatarini.”

 

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com
0717649257

 

 

0/Post a Comment/Comments