.gif)
Adeladius Makwega – Rorya, Mara, Tanzania
Ni majira ya asubuhi ya Juni 23, 2026. Hali ya hewa ya Wilaya ya Rorya, mkoani Mara, ikiwa na nyuzi joto 27, unyevunyevu wa asilimia 5, uwezekano wa mvua kunyesha ni wa asilimia 54, na upepo ukivuma kwa kilomita 54 kwa saa.
Katika hali hiyo, msafara wa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara ulikuwa ukikatiza kuelekea kukagua miradi ya maendeleo katika wilaya hii inayopakana na taifa la Kenya.
Hii ni siku ya pili ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Mara, ambapo Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo, Dkt. Zabroni Masatu, aliwakilisha viongozi wakuu wa mkoa.
“Gari alilopanda mtayarishaji wa makala haya limesoma kilomita 200 zilizotembelewa kwa siku moja tu ndani ya Wilaya ya Rorya, likikagua miradi mitatu: vituo viwili vya afya na daraja la mawe la Mto Nyathorogo. Daraja hilo linaunganisha barabara ya Kumbini–Ahero. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imelijenga kwa gharama ya shilingi milioni 729, likiwaunganisha Wajaluo na Wakurya, yaani Wilaya za Tarime na Rorya, na kurahisisha mawasiliano kati ya maeneo hayo mawili.”
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, ndugu Patrick Chandi, alipongeza ujenzi wa daraja hilo kwa kusema:
“Daraja ni zuri, limejengwa kwa ubora mkubwa. Kabla ya kusikia maelezo ya risala yenu, nilidhani limegharimu mabilioni kadhaa, kumbe ni shilingi milioni 729. Hizi ni gharama sahihi na za haki. Hongereni sana viongozi wa Mkoa wa Mara kwa matumizi mazuri ya fedha za umma. Mimi mwenyewe ni mkandarasi, hivyo nazifahamu gharama hizi vizuri. Mmefanya kazi nzuri. Hata hivyo, naagiza muweke taa nne pande zote ili ndugu zangu watakapokuwa wanatoka kufunga ndoa waweze kuja hapa kupiga picha.”
Miradi miwili ya kwanza ilikuwa ni vituo vya afya vya Kuruya (milioni 250) na Kyang’ombe (milioni 643), vilivyolenga kuboresha huduma za afya kwa jamii.
Hata hivyo, alisema:
“Katika kituo cha afya Kyang’ombe kumetokea wizi wa vifaa vya ujenzi. Natambua kuwa shauri lipo mahakamani na linachukua muda mrefu. Lakini hali kama hii ikijitokeza tena, haipaswi kupoteza muda. Kaeni na viongozi wenu wa kimila, muangalie namna ya kukabiliana na waharifu hao kwa kutumia kanuni na sheria za kimila, hata kuwatoza gharama za hasara iliyotokea.”
Alisema Komredi Chandi.
Katika eneo la Kyang’ombe, kando ya kituo cha afya, kulikuwa na mti mkubwa wa mkuyu uliokuwa ukitoa matunda madogo. Kwa kawaida, miti ya mikuyu ipo ya aina mbili: yenye matunda makubwa na yenye matunda madogo. Matunda haya yanaliwa na binadamu na hata hutumika kutengeneza vilevi na jamu. Huku binadamu akipata vitamin A, C , K na pia humpatia binadamu madini ya Kalsiam, Fosforasi na Magnesiam.
Chini ya kivuli cha mti huu ndipo ulipofanyika mkutano mkubwa wa CCM Mkoa wa Mara, ambapo viongozi walizungumza na wananchi chini ya kivuli cha mkuyu huo.
Wananchi walipata fursa ya kutoa kero zao, wakigusia masuala mbalimbali ikiwamo miradi ya maendeleo, changamoto za watumishi, utendaji kazi wa watumishi wa umma, uhaba wa ajira kwa vijana, na suala la usalama wa raia.
Hoja za ajira kwa vijana na usalama zilijadiliwa kwa msisitizo mkubwa na wananchi walio na umri mkubwa walisema bila woga.
Kuhusu hoja hii, wananchi walieleza hatari wanazokumbana nazo wavuvi, ikiwamo kuporwa samaki, kupigwa, na hata kuuawa na majangili ndani ya Ziwa Victoria.
“Kama hoja hii imeshindikana kushughulikiwa katika ngazi za kawaida, basi ifikishwe katika ngazi ya marais wa nchi tatu zinazotumia Ziwa Victoria: Tanzania, Kenya na Uganda.”
Hoja ya mwisho ilitolewa na mama mmoja mzee, aliyesema haya:
“Chama Cha Mapinduzi ni chama changu, nakipenda. Lakini kuna jambo limeniudhi sana. Ukiwatazama vijana wetu wa Jeshi la Polisi Tanzania kwa sasa, ni kana kwamba siyo raia wa taifa hili. Hili linaniumiza sana. Tumechoka kusikia watoto wetu wanauawa, vijana wetu wanakufa. Ninaomba watafutwe polisi ambao ni raia wa nchi hii watulinde. Maana vijana wanaouawa ni wale ambao wanasoma kwa tabu, hawana ajira, na mwisho wa siku wanapoteza maisha. Wazazi tunabaki na jukumu la kuzika. Wakienda kutafuta kazi, nafasi wanapewa wale wanaovaa vizuri. Hili jambo linaniumiza sana, Mheshimiwa Mwenyekiti.”
Baada ya hoja hizo, zilijibiwa na wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, kila idara kwa nafasi yake, pamoja na mwakilishi wa OCD Rorya.
Mwisho, Komredi Chandi alisema:
“Nampongeza Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Khalifani Haule, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Abdul Omari Mtaki, kwa kufanya kazi vizuri na kuwaletea maendeleo wananchi.
Nawapongeza sana. Hakuna kurudi nyuma—chapeni kazi bila kuchoka. Kuhusu changamoto zilizobaki, msiwe na wasiwasi. Nimeziagiza mamlaka husika kuzifanyia kazi mara moja. Mwezi Agosti 2026 nitarejea Rorya kufuatilia utekelezaji wake.”
Baada ya ukaguzi wa miradi hiyo mitatu na mkutano wa wananchi, ziara hiyo ilihitimishwa katika Wilaya ya Rorya, Mkoa wa Mara.
Mwanakwetu anasema nini leo?
Haya ni makala ya muhtasari wa ziara ya Juni 23, 2026 ya Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Mara katika Wilaya ya Rorya, ambapo miradi ilikaguliwa na wananchi kusikilizwa.
Mwanakwetu upo. Kumbuka:
“Tunahitaji Kulindwa na Polisi ambao ni Sehemu Yetu.”
Nakutakia siku njema.
Mawasiliano:
Barua pepe: makwadeladius@gmail.com
Simu: 0717 649 257











.gif)
Post a Comment