Adeladius Makwega, MARA.
Jua la asubuhi lilikuwa linawaka kwa upole juu ya Mlima Mukendo, wilayani Musoma, wakati Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anyaeshugulikia Kazi , Ajira na Mahusiano, Mheshimiwa Rahma Riyadh Kisuo, akiwasili katika ofisi ya umma kuanza ziara yake mkoani Mara.
Hapa hali ya hewa ilikuwa tulivu—nyuzi joto 24°C, upepo mwanana ukivuma kwa kasi ya kilomita 6 kwa saa—ikiwa kana kwamba inaunga mkono mazungumzo muhimu yaliyokuwa yakielekea kufanyika.
Ndani ya ofisi hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Kanali Evans Alfred Mtambi, alikuwa tayari kumpokea. Mara mazungumzo yao hayakuchukua muda mrefu kabla ya kuingia kwenye hoja nzito: mustakabali wa vijana wa Mara.
Kwa sauti yenye msisitizo, Kanali Mtambi alieleza mabadiliko makubwa yanayoonekana kwa vijana wa mkoa huo. Alibainisha kuwa sasa vijana wengi wamejikita katika shughuli halali za uzalishaji mali, hasa uchimbaji wa madini.
“Tunawaongoza kwa kuwapa mbinu sahihi, bora na zenye tija,”
alisema kwa kujiamini.
“Hatutaki tena kuona vijana wakipoteza muda na rasilimali kwa imani potofu.”
Alisimama kidogo, kisha akaendelea kwa mfano ulioibua tafakuri: zamani, wachimbaji walitegemea ramli na waganga wa jadi—wakipeleka kuku weupe au mbuzi weusi wakiamini watapata madini. Lakini mara nyingi, aliyenufaika alikuwa mganga, huku mchimbaji akibaki maskini.
“Ukikosa madini, unaambiwa umekosea masharti ya mganga. Hayo mambo hatutaki kabisa kuyaona kwa vijana wetu,” alisisitiza.
Mheshimiwa Kisuo, akiwa makini kusikiliza, alionekana kuguswa na juhudi hizo. Kwa tabasamu la kuridhika, aliwapongeza viongozi wa Mkoa wa Mara kwa kutekeleza kwa ufanisi Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hasa katika kuwawezesha vijana kujitegemea.
“Nimekuja Mara kuhakikisha juhudi hizi zinaendelea, na pia kutembelea taasisi zilizo chini ya wizara yetu,” alisema kwa utulivu.
Mazungumzo hayo mafupi lakini yenye uzito yalihudhuriwa pia na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, ndugu yetu, kaka yetu na kiongozi anyesimamia watumishi wa umma katika utendaji kazi ndugu Gerald Musabila Kusaya, pamoja na wataalamu wachache wa wizara.
Kadiri jua lilivyoendelea kupanda angani, ilidhihirika wazi kuwa kile kilichoanza kama mazungumzo ya kawaida, kilikuwa ni ishara ya mwelekeo mpya—Mara inayojenga vijana wake kwa maarifa, si imani potofu; kwa vitendo, si ramli.
0717649257
.gif)

.gif)
Post a Comment