Adeladius Makwega – Mbagala
“Mwanakwetu, mbona jana hukuja kazini? Nimekuangalia kwenye kiti chako siku nzima sikukuona, kaka. Je, ulikuwa na shida gani? Maana hata simu zako zilikuwa hazipatikani.”
Haya yalikuwa maneno ya Easter Musa Mwangaza akimuuliza ndugu yake Mwanakwetu.
Mwanakwetu alijibu kuwa siku iliyotangulia alikuwa na kazi za nje ya ofisi kwa siku nzima, ndiyo maana Easter hakumuona. Kuhusu simu zake kutopatikana, alisema ni tatizo la mtandao kwa sababu walizunguka maeneo mengi.
Kwa hakika, msomaji wangu, katika mazingira ya kazi watu wanaweza kuthamini uwepo wako ikiwa una nafasi au cheo kinachohitajika kwao, kama vile kusaini barua, vocha na nyaraka nyingine za kikazi. Lakini kama huna nafasi hiyo, unaweza kutokuwepo kazini na hakuna hata mtu mmoja akatambua kuwa haupo kwa sababu thamani yako kwao ni ndogo.
Hata hivyo, mtu anayekuthamini kwa dhati atatambua kutokuwepo kwako. Anaweza kukupigia simu, na akikukosa, siku utakapofika kazini atakuulizia. Kwa hakika usijipe matumaini makubwa kwa simu za kikazi pekee; mara nyingi jamii haikuhitaji wewe binafsi, bali huduma unayoitoa.
Msomaji wangu, hapo ulipo jipime na jiulize: uwepo wako hapo ulipo unaangukia wapi? Lazima kuwe na mtu ambaye atakutafuta na ambaye nawe utamtafuta kwa sababu ya mahusiano mema tu na siyo kazi wala chochote kile.
Kumbuka, Mwanakwetu alikuwa karibu na jamaa hawa na waliendelea na mazungumzo yao.
“Mwanamke mwenye utu na anayejitambua, hata akiona mtoto anafinywa au kupigwa, lazima tumbo lake la uzazi litashituka. Mwanamke timamu hawezi kuwa na roho mbaya. Hata wale wanaotupa watoto, mara nyingi uchungu huwatokea baadaye. Ndiyo maana wengi wao hufanya hivyo karibu na makazi ya watu ili mtoto aokotwe na kulelewa. Kinachowasukuma kufanya hivyo ni dhamiri na uchungu wa uzazi.”
Mazungumzo haya yaliendelea kati ya ndugu wawili: Gideon Chilongani, Afisa Usafirishaji, na Easter Musa Mwangaza, Mwandishi na Mwendesha Ofisi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
“Ni kweli zipo kesi za baadhi ya wanawake kutoa mimba au kuwaua watoto wao. Kwa wengi wao, huenda wakawa na changamoto za kiakili au wamefikia hatua ya kukosa kabisa namna ya kufanya. Ndiyo maana uamuzi wa kutoa mimba hufanyika bila kujali utu, sheria wala imani. Mathalani, huenda familia zao zimewatelekeza au hata aliyewapa ujauzito amekataa kabisa kuuhusishwa na ujauzito huo naye. Katika hali kama hiyo, mwanamke anaweza kukata tamaa na kuona hana njia nyingine.”
Mjadala uliendelea huku Mwanakwetu akisikiliza kwa umakini mkubwa.
Kwa upande mwingine, wanaume wanapaswa kuwa makini wanapoambiwa kuhusu ujauzito wanaohusika nao. Si vyema kuukataa bila ushahidi. Japokuwa yapo matukio ya udanganyifu, mengi yanahitaji busara na uwajibikaji.
Mwanakwetu alivutiwa sana na mjadala wa vijana hawa, ambao ni watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Wanaume wajitahidi kuwatia moyo wenza wao wakati wa ujauzito. Maisha yanaweza kuwa magumu, lakini kile kidogo unachopata mshirikishe mwenza wako ili aweze kutunza ujauzito na afya yake.
Mjadala huu ulimvutia sana Mwanakwetu, kiasi kwamba baadaye aliamua kuuweka katika makala haya.
Akiwa katika tafakari zake, Mwanakwetu alikumbuka simulizi ya mmoja wa watu maarufu duniani aliyepitia changamoto kabla ya kuzaliwa kwake. Huyo ni marehemu Steve Jobs, mfanyabiashara na mwanzilishi mwenza wa kampuni ya Apple. Alileta mapinduzi makubwa katika sekta mbalimbali, zikiwemo kompyuta binafsi, filamu za uhuishaji, muziki wa kidijitali, simu za mkononi, kompyuta za kibao na uchapishaji wa kidijitali.
Steve Jobs, kwa kushirikiana na Steve Wozniak, alisaidia kueneza matumizi ya kompyuta binafsi kupitia Apple II.
Katika simulizi yake, Steve Jobs aliwahi kusema:
“Nilizaliwa San Francisco tarehe 24 Februari 1955. Nilipelekwa kuasiliwa na wazazi wangu wa kunizaa ambao hawakuwa wamefunga ndoa. Nililelewa na Paul Jobs na Clara Jobs. Walinijengea hamu ya kujifunza na kuchunguza mambo ambayo ilidumu maisha yangu yote. Malezi niliyopata kutoka kwa wazazi wangu wa kuasili yalichangia kukuza uhuru wangu wa kufikiri na mtazamo mpana kuhusu dunia.”
Aliendelea kueleza kuwa mama yake wa kumzaa alikuwa Joanne Schieble, huku baba yake akiwa Abdulfattah John Jandali, mhamiaji kutoka Syria na Profesa wa Sayansi ya Siasa.
Mama yake alisisitiza kwamba mtoto wake aasilishwe na familia yenye elimu ya juu. Familia ya kwanza iliyopanga kumlea ilijiondoa baada ya kutaka mtoto wa kike badala ya wa kiume. Baadaye Paul na Clara Jobs walimlea baada ya kusaini hati ya kisheria wakiahidi kumpeleka shule hadi chuo kikuu.
Steve Jobs alisema:
“Ingawa niliasiliwa, sikuwahi kujihisi nimetupwa wala kutelekezwa. Daima niliwaita Paul na Clara Jobs wazazi wangu wa kweli.”
Maneno haya aliyatoa katika hotuba yake maarufu ya mahafali katika Chuo Kikuu cha Stanford.
Maelezo ya maisha yake yanaonesha kuwa akiwa mtu mzima aliwatafuta mama yake wa kumzaa na dada yake, Mona Simpson, ambaye ni mwandishi wa riwaya. Waliweza kujenga uhusiano wa karibu sana.
Hata hivyo, Jobs hakuwahi kukutana na baba yake wa kumzaa, John Jandali. Inasemekana baadaye aligundua kuwa mmiliki wa mkahawa aliokuwa akipenda kula mara kwa mara alikuwa baba yake mzazi. Licha ya kugundua ukweli huo, hakuwahi kwenda tena katika mkahawa huo.
Mwanakwetu anasema nini leo?
Kwa hakika, maelewano ya pande zote ni jambo la msingi. Kila upande unapaswa kuwa na uelewa na kutambua kwamba tunaishi leo kwa sababu waliotutangulia walitoa nafasi ya sisi kuishi. Vivyo hivyo, nasi tunapaswa kutoa nafasi kwa wengine kuishi.
Ndiyo maana aliyewahi kuwa Rais wa 40 wa Marekani, Ronald Reagan, aliwahi kusema:
“Nimegundua kwamba kila mtu anayeunga mkono utoaji mimba tayari ameshazaliwa.”
Kauli hii ililenga kuhimiza watu kutafakari thamani ya uhai wa binadamu na haki ya kuishi ambayo kila mmoja amepewa.
Mwanakwetu upo?
Kumbuka:
“Nafasi Uliyopewa Kuishi Wape na Wengine.”
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
Simu: 0717 649257
.gif)









Post a Comment