Muuza Magurudumu Kavuka Miaka 18

Adeladius Makwega – Kichanga Chui


MSASANI, DAR ES SALAAM

“Nimeshuhudia vita viwili vya Ghuba: vile vya George Bush (Baba) kati ya mwaka 1990–1991, ambapo mataifa 35 ya Magharibi yalimuunga mkono Marekani dhidi ya Iraq chini ya Rais Saddam Hussein katika eneo la Ghuba ya Uajemi. Vilevile, vita vya George Bush (mtoto) vya mwaka 2003 ndivyo vilivyosababisha Saddam Hussein kuondolewa madarakani, kukamatwa na baadaye kunyongwa tarehe 30 Desemba 2006.

Katika mazingira niliyokulia ya Mbagala, wakazi wa asili ya eneo hili waliamua kulibatiza eneo la Mbagala Kizinga, Mbagala kwa Selenge, Mbagala Misheni na Mbagala kwa Diria—eneo lililo katikati na jirani na Mto Kizinga—kuwa Mbagala Baghdadi, likitokana na jina la Baghdad, mji mkuu wa Iraq.”

Haya yalimjia Mwanakwetu akilini baada ya kuona maneno ya malalamiko na shutuma dhidi ya familia moja mitandaoni, kuhusu kijana wa kiongozi mkubwa wa Tanzania kuonekana katika ziara pamoja na viongozi wa kitaifa na kimataifa, huku maneno ya matusi na kejeli yakiporomoshwa dhidi yake.

“Huyu muuza magurudumu anafanya nini katika ziara hiyo? Kama muuza magurudumu amepewa barua ya kazi yenye nembo ya Bibi na Bwana, tuambiwe…”

Mwanakwetu alijiuliza: je, haya malalamiko yana msingi au ni hisia za kijamii zisizo na ukweli? Je, Watanzania wanamuonea gere muuza magurudumu kuambatana na Bi Mkubwa? Au kusafiri kwa ndege kutoka Dar es Salaam hadi Moscow? Au kukaa katika hoteli za kifahari? Au kusalimiana na mtoto wa Maria Ivanovna Putina? Au hata kupeana mkono na mtoto wa Vladimir Spiridonovich Putin?

Kwa hakika, muuza magurudumu anapaswa kuelewa kuwa jamii ina maswali mengi kuhusu uwepo wake katika msafara huo.

“Katika utumishi wa umma, mtoto aliye chini ya miaka 18 ana haki na stahiki za mzazi wake. Lakini muuza magurudumu ameshavuka umri huo. Je, kwa nini bado awe katika msafara huu bila ufafanuzi? Kama kuna barua maalum, basi iwekwe wazi.”

 

Mwanakwetu anakumbuka pia vita vya Ghuba vilivyoleta madhara makubwa kwa Iraq, hadi wakazi wa Mbagala wakabatiza eneo lao jina la Mbagala Baghdadi, wakati huo kiongozi wa Iraq akiwa Saddam Hussein.

Historia ya familia ya Saddam Hussein inadokeza:

Uday Hussein (1964–2003) alikuwa mtoto wa kwanza wa Saddam Hussein. Alijulikana kwa ushawishi mkubwa katika michezo, vyombo vya habari na vikosi vya kijeshi. Aliongoza Shirika la Vijana la Iraq na kikosi cha Fedayeen Saddam. Alihusishwa na matukio mengi ya ukatili na alijeruhiwa vibaya katika jaribio la mauaji mwaka 1996.

Qusay Hussein (1966–2003) alikuwa mtoto wa pili na alichukuliwa kama mrithi wa utawala wa baba yake. Alisimamia vikosi vya usalama na ujasusi vya Iraq na aliuawa tarehe 22 Julai 2003 mjini Mosul wakati wa operesheni ya majeshi ya Marekani.

Saddam Hussein pia alibarikiwa na mabinti watatu: Raghad Hussein, Rana Hussein na Hala Hussein, ambao maisha yao yalibadilika baada ya kuanguka kwa utawala wa baba yao.Inasemekana pia alikuwa na wake wawili waliotambulika zaidi:Sajida Talfah, mke wa kwanza na binamu yake, waliozaa watoto watano: Uday, Qusay, Raghad, Rana na Hala. Samira Shahbandar, mke wa pili, ambaye aliolewa na Saddam mwaka 1986 na walipata mtoto mmoja anayeitwa Ali Saddam Hussein

 

Pia kuna madai ya wake wengine waliotajwa kama Nidal al-Hamdani na Wafa Mullah Huwaysh, ingawa taarifa zao hazikuthibitishwa kikamilifu. Kwa ujumla, wake wanaokubalika zaidi kihistoria ni Sajida Talfah na Samira Shahbandar.

Inasemekana Sajida Talfah anaishi kwa faragha nje ya Iraq, akiwa na matatizo ya kiafya na akipatiwa matibabu, huku watoto wa Saddam waliobaki wakiishi kwa kujificha nje ya Iraq, hasa Jordan.Raghad Hussein — anaishi Jordan tangu 2003 chini ya ulinzi. Rana Hussein — naye anaishi Jordan tangu 2003. Hala Hussein — taarifa zake ni chache na maisha yake ya sasa hayajulikani wazi.

Kwa upande wa watoto wa kiume, Uday Hussein na Qusay Hussein waliuawa mwaka 2003 huko Mosul, Iraq.

Inasemekana pia kwamba mtoto wa kiume anayeitwa Ali Saddam Hussein, aliyezaliwa na Samira Shahbandar, huenda anaishi maisha ya faragha nje ya Iraq, ingawa taarifa zake hazijathibitishwa wazi.

 

Msomaji wangu, haya yote yalimjia akilini Mwanakwetu alipokuwa akisoma maoni ya Watanzania kuhusu mtu aliyepachikwa jina muuza magurudumu, kisha akaamua kuyaweka katika makala haya.

Mwanakwetu anasema nini?

Kwa hakika, unapofanya siasa kama mzazi, kumbuka kuwa unafanya siasa wewe mwenyewe, si watoto wako wala familia yako. Tenganisha siasa na maisha ya nyumbani. Ukifanya hivyo, unalinda amani ya familia yako na vizazi vijavyo.

Kwa wale wanaokumbuka enzi za Charles Makongoro Nyerere alipokuwa NCCR Mageuzi ya Augustine Mrema, alikuwa akichanganyika na wananchi kwa urahisi bila hofu. Lakini leo watoto wa viongozi wenye hadhi kama ya Makongoro Nyerere hali inaweza kuwa tofauti kulingana na mazingira ya kisiasa na kijamii.

Mwanakwetu anaamini kuwa:familia zinazogusa siasa lazima ziwe makini, na jamii lazima ipewe ukweli bila maficho.

“Muuza magurudumu kavuka miaka 18.”

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257













 



0/Post a Comment/Comments