.gif)
Adeladius Makwega
Dodoma
Kwa wale wasomaji wa matini zangu watakumbuka kuwa niliandika matini iliyopewa jina Maamuzi ya Hakimu Mrisho Kikwete.
Katika shauri hilo, Hakimu Mrisho Kikwete, ambaye alikuwa akihudumu katika Mahakama ya Mwanzo ya Msoga mwaka 1944, alipokea shauri mezani kwake la kosa la jinai kati ya Mbone Lunema dhidi ya Makinamsisi.
Shauri hilo lilihusu ndugu hawa waliokuwa katika ngoma, ambapo Makinamsisi alimsukuma Mbone Lunema na kumsababisha kuanguka, kupoteza meno yake mawili, na baadaye kuwa kibogoyo. Ndugu Mbone Lunema akaenda mahakamani kushitaki. Ndugu hawa wote walikuwa Wakwere wa koo zenye utani.
Mbele ya mahakama iliyo chini ya Hakimu Mrisho Kikwete, shauri hilo lilitupiliwa mbali kwa kuwa lilikuwa la kimila—utani. Tatizo lilikuwa kwa Mbone Lunema mwenyewe, ambaye aling’oka meno yake mawili kwa kutokuwa makini na utani huo uliofanywa na Makinamsisi.
Katika matini yangu, nilieleza kuwa maelezo haya yalinukuliwa na Profesa Tigiti Sengo, ambaye mwaka 1972 alikuwa mwanafunzi wa chuo kikuu aliyekwenda kijijini Msoga kufanya utafiti juu ya utani baina ya kabila la Wakwere na namna mashauri hayo yalivyoamuliwa mahakamani.
Profesa Sengo alielezwa kuhusu shauri hilo na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Msoga, Bagamoyo (sasa Chalinze), mwezi Juni 1972, Mheshimiwa Bakari Mgweno, ambaye alishuhudia kwa macho yake shauri hilo lilipoamuliwa mwaka 1944.
Kwa mujibu wa maandishi ya Profesa Sengo, mwaka huo wa 1972 alipatiwa pia nakala ya mwenendo wa shauri hilo hadi lilipotupiliwa mbali.
Katika matini yangu niliuliza swali: Je, Hakimu Mrisho Kikwete ni baba wa Mheshimiwa Jakaya Kikwete?
Swali hili lilikuwa sentensi yangu ya mwisho katika matini hiyo.
Binafsi, niliwatafuta rafiki na ndugu zangu Wakwere wanaoishi Msoga na Lugoba ili kupata jibu la swali hilo. Nilipowasiliana nao kwa njia ya simu, waliniunganisha na Mwalimu Michael Mbena Kigunia, mwalimu mstaafu mwenye umri wa miaka 82 mwaka 2022 na ambaye mwaka 2026 ana miaka 86.
Mwalimu huyu alieleza kuwa anaifahamu vizuri familia ya Kikwete tangu zamani—kuanzia babu, baba, na ndugu wengine—waliokuwa wakiishi pamoja katika mazingira ya nyumbani na hata shuleni.
“Familia ya Kikwete walikuwa na maisha mazuri; walizalisha chakula cha kutosha, hawakuangaika na njaa, na hata shuleni wengi wao walisoma tangu wakati huo.”
Mwalimu Mbena alienda mbali zaidi kwa kulijibu swali langu, akisema kuwa Hakimu Mrisho Kikwete alikuwa babu wa Jakaya Kikwete.
Alisema pia anamfahamu vizuri Hakimu Kikwete kwani wakati huo Mahakama ya Msoga ilikuwa kubwa na maarufu, ikihudumia Wakwere wengi.
Kwa bahati nzuri, Februari 1, 2022 saa 8:41 mchana, nilipata jibu la swali hilo kutoka kwa Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete mwenyewe, aliyekuwa Rais wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kabla sijanukuu jibu lake, nilikumbuka mafunzo ya walimu wangu wa Shahada ya Sanaa ya Habari kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa—akiwemo Dkt. Irene Mkini, Dkt. Gasper Mpehongwa, na Profesa Esau Ntabindi—walionifundisha kuwa maneno ya kiongozi yanaponukuliwa yanapaswa kuwekwa ndani ya alama za kunukuu.
“Mrisho Kikwete alikuwa babu yangu aliyemzaa baba yangu Kikwete Mrisho Kikwete, kwa jina lingine Halfani Mrisho Kikwete. Yeye alikuwa mtawala, na moja ya majukumu yake yalikuwa kusikiliza na kuamua mashauri ya kimila ya kabila la Wakwere.”
Haya ni majibu yake kama alivyonijibu swali langu.
Binafsi, namshukuru sana Mheshimiwa Jakaya Kikwete—kwanza kwa kuisoma matini yangu, na pili kwa kutoa jibu la swali hilo kwa heshima na taadhima.
Kitendo cha Mheshimiwa Jakaya Kikwete kujibu swali hili ni cha kiungwana na kinapaswa kuigwa na viongozi wengine. Kiongozi ni mtu wa watu, na hivyo hauna budi kutoa ufafanuzi, ni vyema kufanya hivyo.
“Nakutakia kazi njema, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, na Mwenyezi Mungu akujalie afya njema wewe na familia yako. Ahlan wa sahlan.”
Hii ni makala ya Mwanakwetu ya mwaka 2022, ambayo Mheshimiwa Jakaya Kikwete aliisoma na kuijibu hoja iliyoulizwa.
Kwako ndugu yangu Jakaya Kikwete, leo hii mwaka wa 2026 ninakuomba kwa hisani yako: ukiziona makala za Mwanakwetu, tafadhali nisaidie ziwafikie watu wengi zaidi wasome maana kuna mengi tunayoyafahamu sisi, lakini wengine hawayajui, wengi ni wadogo na hata wengine wakubwa lakini kuyajua mambo ni majaliwa ya Mungu.
Kama ilivyokuwa kwa matini ya Profesa Tigiti Sengo iliyohifadhiwa kwa maandishi ya mashine (typewriter), kuhusu kisa cha babu yako Mrisho Kikwete cha mwaka 1944, hadi kusomwa tena mwaka 2022—miaka 78 baadaye—na Mwanakwetu, makala hii imeipa uhai mpya taarifa hii, na itaendelea kusomeka hata katika karne zijazo.
Kwa msomaji wa matini zangu, nakutakia siku njema. Matini ijayo itahusu kabila la Wakerewe.
Nakutakia siku njema.
0717 649 257





.gif)
Post a Comment