MISEMO ITAKAYOPATA UMAARUFU

 



Adeladius Makwega – MBAGALA

 

Kwa muda wa juma zima, Mwanakwetu hakuandika makala yoyote mpya; badala yake, alijikita kikamilifu katika mfululizo wake wa makala kuhusu Mgogoro wa Azania na Tambaza.

 

Katika kipindi hiki, ndugu Mwanakwetu alipokea simu nyingi pamoja na ujumbe mfupi kadhaa, wengi wakimchokoza kwa kusema:

 “Kaka, mbona husemi chochote kuhusu maamuzi haya ya Bunge la Ulaya?”

Mwanakwetu akawajibu kwa kebehi:


“Sasa ni zamu ya Mgogoro wa Azania na Tambaza. Kuhusu utekaji, tulisema sana tangu Balozi Humphrey Polepole alipokuwa mbunge, baadaye balozi—akitoka Malawi hadi Cuba—na hata alipoacha ubalozi na kuwa mtu wa kawaida, tuliendelea kumuuliza maswali kama wanahabari. Kisha, kwa ubaya zaidi, hawa washenzi wakamteka ndugu yetu. Ndugu zangu, sasa ni zamu ya Mgogoro wa Azania na Tambaza.”

 

Baadaye, Bunge la Ulaya likafanya maamuzi dhidi ya Tanzania, na Euro 156,000,000—sawa na takribani shilingi za Kitanzania bilioni 470.34—ziko hatarini kutoingia katika taifa hili la Afrika Mashariki.

 

Lakini Mwanakwetu bado yuko bize, akiendelea na makala zake za Mgogoro wa Azania na Tambaza.

Jamaa wanamuuliza: “Umesafiri?”
Anajibu: “Nipo katika safari ya Mgogoro wa Azania na Tambaza.”

 

Ndugu, jamaa na marafiki wanaendelea kumchokoza. Wao wanataka kumuingiza kwenye mjadala wa Euro milioni 156 za Umoja wa Ulaya.


“Hali itakuwa mbaya, tutakimbiana hapa!”
Mwanakwetu anasema kimoyomoyo: Najua kinachoendelea.

Ghafla, Mwanakwetu anaelekea mkahawani kunywa chai. Njiani, anakutana na madereva kadhaa wakiwa pembeni ya magari yao, wakijadiliana:

 

“Tulipita kule… ehee! Barabara zimejaa mashimo. Mvua ikinyesha, vyura watazaliana humo—hata samaki tutavua! Nilitarajia kufika mapema, lakini nusura nichelewe. Badala ya saa moja na robo, nimetumia saa mbili na robo. Nimepata pancha tatu! Mwishowe nikawaacha wenzangu waendelee na safari kwa kupanda gari la wenzetu, nikakodi bodaboda kubeba matairi mawili hadi mjini kuyaziba. Gharama? Shilingi 35,000! Na safari yenyewe—malipo hakuna!

Sasa hata kama safari haina malipo, si tatizo—ni sehemu ya kazi. Lakini vipi gharama zangu? Hivi hawa maafidhina watalipa kweli?”

 

Dereva mmoja akacheka, mwingine akaongeza haya:


“Hapo kaka, fina li lai! Ni sawa na kuchangia timu icheze mechi halafu ifungwe—hakuna furaha, na pesa yako imepotea. Kuwa mpole tu. Unasukuma gurudumu la maendeleo!”

Dereva mwingine akasema:


“Siku hizi uwe makini. Ukienda vijijini bila hata senti mfukoni, unaweza kulala msituni. Bahati mbaya ukiwa na abiria walioko kama wewe—mmekwisha! Unakuwa chakula cha simba. Na hawa simba, nasikia wanapenda sana nyama ya binadamu—inasemekana ina chumvi nyingi. Baba, unaliwa tu!”

 

Mwanakwetu akapita zake kimya kimya, kana kwamba hasikii, na kuendelea na safari yake.

 

Baada ya kunywa chai, kupiga simu kadhaa, anarudi. Madereva wametawanyika. Lakini anakutana na mabawabu wakizungumza:

“Jana kulikuwa na ugeni mkubwa—watu kama 300 hadi 400 walikuwa kwenye kikao. Tulikuwa tunalinda, tukisikia makofi, vicheko na nyimbo. Mchana nikaenda chooni—lo! Bahari ya mkojo mweusi! Nikashindwa hata kujisaidia. Nikalazimika kwenda choo cha shimo jirani. Hapo ndipo nikatambua umuhimu wa choo cha shimo—jenga nyumba, lakini usisahau choo cha shimo!

 

Kumbe maji yalikuwa yamekatika. Wale wageni wakaenda kula, nasi tukapata chakula. Ndani ya foleni, nikasikia: ‘Vyoo vimeziba, maji hakuna!’ Nikakumbuka ile bahari ya mkojo. Wengine walikimbilia vyoo vya jirani, lakini mwenye vyoo akafunga milango na kuondoka na funguo. Watu wanabisha—wanaambiwa mwenye funguo hayupo!

 

Na sisi tupo karibu na chanzo kikubwa cha maji—kuna pampu tatu, lakini inafanya kazi moja tu. Nyingine zimeharibika. Sasa maji ni mgao. Je, tutakuwa salama? Huu si mwanzo wa kichocho na kipindupindu?”

Mwanakwetu akapita tena kimya kimya, akienda kukamilisha makala yake.

Jumamosi, Juni 20, 2026, ndipo Mwanakwetu alitafakari vijembe hivi na kuamua kuviweka katika makala haya.

 

Leo anasema nini?

Hakika, Euro milioni 156 zinahitajika kwa miradi mbalimbali ya maendeleo. Ingawa hakuna mgawanyo rasmi wa moja kwa moja kwa kila sekta, inajulikana kuwa fedha za Umoja wa Ulaya huwekwa katika mifuko ya miradi ya sekta nyingi (multi-sector programmes). Makadirio ya kawaida yanaweza kuwa hivi:

  • Nishati na umeme: 30–35% (Euro milioni 46–55)
  • Maji: 15–20% (Euro milioni 23–31)
  • Barabara na miundombinu: 20–25% (Euro milioni 31–39)
  • Afya na elimu: 10–15% (Euro milioni 15–23)
  • Utawala na programu za jamii: 10–15% (Euro milioni 15–23)

Umeme unachukua sehemu kubwa—takribani theluthi ya fedha zote—hasa kwa miradi ya kusambaza umeme vijijini. Barabara zinachukua karibu robo ya fedha, zikisaidia wakulima na wafanyabiashara. Sekta ya maji ni muhimu kwa uhai wa binadamu. Afya na elimu hupata sehemu ndogo lakini muhimu—kliniki, shule, vifaa, na mafunzo. Mwisho, utawala na jamii huboresha mifumo ya taasisi na programu za kijamii.

Lakini msomaji wangu, rejea yale visa viwili—madereva na barabara, pamoja na mabawabu na maji.

Hapo ndipo misemo inaweza kuzaliwa:
“Leo hakuna maji!”
“Umeme umekatika!”
“Mashimo barabarani yamezidi!”
“Barabara hazitengenezwi!”
“Nguzo zimetelekezwa vijijini!”
“Huduma ya dawa imesitishwa!”
“Dawa hazipatikani!”

 

Misemo hii itatawala midomo ya Watanzania iwapo suala la Euro milioni 156 halitapatiwa ufumbuzi.

Kwa hakika, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa inapaswa kuweka mkazo katika hali hii—ili Tanzania ibaki salama, na mimi na wewe tubaki salama.

Mwanakwetu upo? Makala haya yaitweje?
Niendelee na “Tambaza” au nichague “Misemo Itakayopata Umaarufu”?

Mwanakwetu anachagua: Misemo Itakayopata Umaarufu.

Nakutakia siku njema.


makwadeladius@gmail.com
0717649257

 

 

0/Post a Comment/Comments