MGOGORO WA AZANIA NA TAMBAZA XXXVII

 





Adeladius Makwega - DODOMA

Katika matini zilizotangulia, nilielezea namna nilivyokuwa nipo katika daladala, naelekea Mtoto Aziz Ali, nyumbani kwa Wakili wa Serikali, Phidelis Mwidunda, na namna nilivyoifungua bahasha yenye nyaraka ya utetezi iliyowasilishwa kwa Bodi ya Rufaa ya Jiji la Dar es Salaam.

Nakala hii ilikuwa na karatasi nyingi, ikiwa na maelezo ya kina na vielelezo kadhaa, huku ikieleza namna mwanafunzi Adeladius Makwega alivyoanza kidato cha kwanza akitokea Mtoni Kijichi Primary School, akiwa ni mwanafunzi pekee aliyefaulu darasa la saba mwaka 1990.

Wanasheria hawa wawili waliongezea herufi “F,” ambayo ni jina la baba la mwanafunzi, na kumtambulisha kama Adeladius Francis Makwega badala ya jina la awali lililokuwa na majina mawili, kama alivyojiunga na Tambaza Sekondari mwaka 1991, yaani Adeladius Makwega.

Sababu hiyo nadhani wao, kama wanasheria, walikuwa na sababu zao za msingi, huku ikiwa ndiyo usahihi, kwani jina Makwega si jina la baba, bali ni jina la ukoo, na majina ya Mwanakwetu sasa yalikuwa matatu kukidhi hoja za kisheria.

Jambo la pili, nilibaini kuwa waliambatanisha vielelezo kadhaa ambavyo vilianza kielelezo A mpaka F. Mojawapo ya vielelezo hivyo ilikuwa ni ripoti za maendeleo ya taaluma za kila muhula, tangu kidato cha kwanza muhula wa kwanza hadi kidato cha tatu muhula wa kwanza.

Walipokuwa wakijenga hoja, walikuwa wakimrejesha katika vielelezo hivyo Mwenyekiti wa Bodi ya Rufaa, ambaye alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Kwa mfano, walijenga hoja ya tabia ya mwanafunzi wakirejea maelezo ya walimu wote wa darasa tangu kidato cha kwanza. Walimjulisha mzazi kuwa mwanafunzi husika alikuwa na tabia nzuri, huku akiwa na daraja A la tabia njema.

 

Walihoji: iweje walimu wote wa darasa, miaka mitatu mfululizo, waendelee kumtaja mwanafunzi Makwega kama mwanafunzi mwenye tabia nzuri; wanafunzi wote wa darasa la 3R1 wamkitaja Makwega kama mwanafunzi mwenye tabia njema; iweje, ghafla bin vuu, bodi ya shule iseme Makwega alikuwa na tabia mbaya? Ati ndiye aliyeiletea Tambaza sifa mbaya? Hapa maana yake bodi ya shule inapoka mamlaka ya mwalimu wa darasa?

Mawakili hawa walienda mbali zaidi na kusema kuwa ripoti ya taaluma ya mwanafunzi ni mojawapo ya mawasiliano ya shule na mzazi kila baada ya miezi sita, na kama kuna hoja ya mwanafunzi kubadilika tabia, shule husika itamjulisha mzazi ili kusaidia kumrekebisha mwanafunzi tabia yake kwa pamoja, siyo kumfukuza shule (walimu na mzazi).

Hoja nyingine iliyojengwa na mawakili hawa ilikuwa: wanafunzi wa darasa la 3R1 wote walicharazwa bakora sita kila mmoja kutokana na fujo alizofanyiwa mwanafunzi wa kidato cha tatu wa Jangwani, Fausta Nguzo; iweje tena itolewe adhabu nyingine?

 

Kwa hiyo, kitendo cha kumfukuza shule mwanafunzi Makwega kilikuwa ni kumpa adhabu nyingine, jambo ambalo si la haki na ni kitendo cha uonevu kwa mwanafunzi huyo.

Pia, kitendo cha mwanafunzi huyu kukaa nyumbani tangu Oktoba 20, 1993 hadi Bodi ya Rufaa ya Mkoa itakapofanya maamuzi kitakuwa pia ni adhabu nyingine kubwa ya tatu dhidi ya mwanafunzi huyo.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba mbele ya bodi yako tukufu mwanafunzi huyo arudishwe shuleni ili aweze kumaliza elimu yake ya kidato cha tatu na cha nne mara moja, ili apate fursa ya kuitumikia nchi yake ya Tanzania katika taaluma atakayojaliwa.

Kwa kifupi sana, huo ndiyo ulikuwa utetezi mbele ya Bodi ya Rufaa ya Mkoa, ambapo sasa ilikuwa ni kila wiki kwenda kwa Afisa Elimu wa Jiji kuulizia tarehe ya kikao, ambapo safari zilikuwa za nenda rudi, nenda rudi.

Je, kipi kitaendelea?

Subiri matini ijayo.

Kumbuka, haya ni makala ya mgogoro wa Azania na Tambaza XXXVII.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 



 

0/Post a Comment/Comments