MGOGORO WA AZANIA NA TAMBAZA XXXV

 


 



Adeladius Makwega-DODOMA.

Mara baada ya kutoka ofisi za Jiji la Dar es Salaam nilipitia wizara ya sheria ya wakati huo na hapo nilielekezwa kumfuata mwanasheria mmoja wa serikali aliyefahamika kama Phidelis Mwidunda, mwanasheria huyo jina lake siyo Fidelis bali Phidelis msomaji wangu japokuwa matamshi ni yale yale.


Nilipokelewa katika geti la wizara hiyo ambalo lilikuwa jirani na jengo la Mahakama Kuu likitazamana na Bahari ya Hindi. Nina hakika wanasheria wa serikali waliokuwamo katika ofisi hiyo walikuwa wakiona mandhari hiyo wa Bahari Hindi sawasawa na mtu aliyekuwa amelala katika Hotel ya New African Hotel.



Mwanakwetu sidhani kama wanasheria na mawakili wa sasa wa serikali wanaipata mandhari hiyo tamu, maridadi na murua ya upepo mwanana wa Bahari ya Hindi huko Mtumba jijini Dodoma baada ya kuhamishiwa Wizara zote huko.

 

Ngoja warudi katika hiyo filamu yao ughaibuni tutajenga hoja ya kuwa na bwawa kubwa jirani na Wizara ya Katiba na Sheria na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Mji wa Serikali-Dodoma angalau wanasheria hawa wakishatoka kupambana na kesi waipate ile mandhari murua ya Bahari ya Hindi.

Nilipofika hapo nilikutana baadhi ya wanasheria wa serikali ambao walinipokea vizuri sana, wanasheria hao niliwauliza jamani nimekuta ndugu Phidelis Mwindunda? Walinijibu kuwa hapa hatuna ndugu Phidelis Mwidunda. Hapo yupo wakili wa serikali Phidelis Mwidunda, niliwajibu naam kuwa ndiyo huyu huyu.

 

Mawakili hawa waliniuliza, yaani wewe unakuja hapa ofisini kwetu unamuuliza mtu mkubwa kama Advocate Mwidunda alafu sisi hatukufamu? Nikawajibu samahanini ngoja na mimi nijitambushe.

“Mimi naitwa Adeladius Francis Fidelis Makwega, natokea Mbagala!”

Wakaniambia kaa katika kiti na meza cha mawakili serikali ili ukirudi kwenu Mbagala ukawasimulie. Kimoyo moyo nikasema hawa mawakili wahuni sana , ngoja na mimi nienda nao kihuni kihuni , niwaonesha kuwa mimi ni mwanafunzi wa Tambaza

 

Sasa wewe ni (M) mwanamume alafu jina lako unaitwa Adela, sasa wewe ni (M) mwanamume au mwanamke (F)?

Kumbuka nipo Wizra ya Sheria ya Jmahuri ya Muungano wa Tanzania katika chumba anachofanyia kazi wakili  Phidelis Mwidunda na mawakili wenzake wa serikalia wananichokoza, na kunidhalilisha.

 

Hekima ya mtu akikudhalilisha mbele za watu usimuoneshe kuwa lile jambo limekukela lakini ukipata faragha unaweza kumfundisha adabu bila ushahidi wa mtu mwingine na hili ndiyo ilikuwa inafanyika sana na wanafunzi wa Tambaza.Unagombana na mtu siku ambayo umesahau yeye anakuja kulipiza kisasi ambapo hili jambo baya sana , hekima nzuri ni kumdhalaua mtu anayekudhalilisha mbele ya watu.

Jamaa mmoja wakili aliongea jamaa mwingine huku akibana na stepla makaratasi yake. Nikamjibu mimi ni M na jina langu siyo Adela bali Adeladius, wakawa wanacheka tu.

 

Ndugu itabidi tukupe hati affidavite (hati ya kiapo)nyingine? Mimi wakati huo nilikuwa sifahamu maana ya affidavite, lakini niliwajibu sawa.

Jamaa huyu akajinu kuwa wakili Mwidunda yupo mahakamani, njoo Jumatatu atakuwepo na uje mapema, nikajibu sawa. Nikasema kumbe wahuni hawapo Tambaza tu, kumbe hadi makazini kuna wahuni?

 

 

Nilipotoka hapo nikapita Stesheni, nikawa na hoja mbili niende Mbagala? Nilijiuliza, nikaamua ngoja niende Kariakoo kwa shangazi yangu wa Sokoni kariakoo (Mwanakwetu tambua kuwa shangazi ni baba) nikafika nikaingia ofisini kwake, yeye alikuwa karani wa mkubwa soko hilo wakati huo.

Nikamuelezea shangazi yangu huyu anayeitwa Salome Fidelis Makwega (sasa ni marehemu). Nipomueleza juu hii nakala naifanya nini? Salome Makwega akaniambia huyu wakili kwake ni jirani na viwanja vya maonesho ya Sabasaba-Mtoni Azizi Ali, mkono wakulia, jirani kabisa na mwanzo ya Kambi ya Jeshi la Wananchi ya Twalipo, ukitoka hapa nenda kaiache hapo, mimi nitazungumza na ndugu Peter Pinda.


Shangazi yangu huyu alinichukua akanipeleka hotelini nikala vizuri pilau na soda, nikajiuliza, niende sasa hivi Mtoni Azizi Ali? Nilipomaliza kula niliamua kupita nyumbani kwa Arone Sifuni Mtaa Pemba nyumba namba moja yule kijana tuliyefukuzwa wote pamoja na Mohammed Said.


Nikatoka zangu nikapita njia jirani na Msikiti wa Shekhe Idrisa nikakuta Waislamu wengi wakisali na njia hiyo imezibwa kabisa. Kwa desturi ya misikiti ya katikati ya Jiji la Dar es Salaam siku ya Salat Ijumaa njia huwa zinafungwa kutokana wingi wa waamini na makubadhi mengi yapo nje, kwa hiyo nilipenyapenya katika milango ya maduka ya pembeni na kupita na kufika kwa akina Arone Sifuni.

 

Nilipofika hapo nilimkuta mama wa Arone, nikamsalimia akanipokea sebuleni kwake, mama huyu ambaye sasa ni marehemu aliniuliza mambo mengi juu ya rufaa, nikamueleza vizuri kuwa sasa mimi nimeshawasilisha rufaa yangu kwa Afisa Elimu wa Jiji la Dar es Salaam.

Nikamuuliza vipi ya Arone? Akasema pia na wao walishawasilisha, hapa hapa nikamuulizia Arone yu wapi?

Kumbuka tu msomaji wangu kuwa jina lake la nyumbani ni Katisi, hapa mama huyu aliwatuma mabinti zake wa kazi za nyumbani kumtafuta Katisi.

Mama wa Arone alikuwa mama mmoja mrefu sana, mweupe aliyekuwa anajipenda mno, huku akiwa na maisha mazuri, kwa hakika kila mara nilipomkuta vidole vyake vilipambwa na pete na shingo cheni za dhahabu. Mama huyu siku hii alinisimulia namna alivyokuwa akisoma Jangwani sekondari miaka ya 1970 na hadi alipokutana na baba wa Arone na kumzaa Arone.


Huyu alikuwa mama wa mjini, wa mama wa mjini mara nyingi huwa ni wakarimu mno na huwa na habari nyingi za mjini, kwani mama huyu aliniaambia kuwa alizaliwa hapo hapo mtaa Pemba mwaka 1956.


Mazungumzo haya yalifanyika sebuleni kwake huku feni ikizunguka kwa kasi mno maana mwezi wa Novemba huwa ni mwezi wa joto kali Jijini Dar es Salaam. Nikiwa sebuleni hapo usingizi ulinishika kutokana na kuchoka na niliamka alfajiri kwenda kwa ndugu Peter, kwa hiyo sofa la mama wa Arone liligeuka kuwa kitanda cha muda.

Nakumbuka neno la mwisho la mama huyu lilikuwa hivi Arone hamjampata? Mara nilisikia azana ya msikiti wa Idrisa ikinadi na hapo ndipo nilishituka kutoka usingizini nikabaini kuwa nimelaza kichwa changu katika kochi la nyumbani hii ya Mtaa wa Pemba nyumba namba moja.



Hadi usingizi unaishi Arone hakupatikana, wale mabinti wa kazi wa mama huyu sasa walishanizoea, wakiniita ah rafiki yake Arone!, Ah rafiki yake Arone!, huku na mimi nikiwapa tabasamu kali la Kimbagala Mbagala nikiwajibu Ah dada zake Arone!, Ah dada zake Arone!


Nadhani mama huyu aliwaambia wale mabinti wa kazi wasiniamshe, kama mzazi alitambua kuwa kijana wake nilikuwa nimechoka mno.

Niliomba maji ya kunywa na mabinti wa kazi wa mama huyu waliokuwa wakitokea Kigoma (Wamanyema) walinipa maji nikapoza koo langu, nami kuondoka zangu. Hadi ninaondoka hapo sikuweza kumuona Arone Sifuni.

Nikiwa kwenye basi niliifungua nyaraka ile na kuisoma tangu mwanzo hadi mwisho kukiwa na maelezo ya matukio kadhaa na hali ya Tambaza tangu mwaka 1991 hadi mwaka 1993 hadi wakati wa tukio la kufanyiwa fujo Fausta Nguzo.

Nilishuka jirani na Viwanja vya Sabasaba na kwenda nyumbani kwa wakili Mwidunda, nilipotea potea lakini baadaye niliambiwa kuwa alikuwa amepanga katika nyumba moja ya mchezaji wa zamani wa Yanga ambaye sasa jina lake nimelisahau.


Nikafika na kumkuta mkewe ambaye wakati huo alikuwa nadhani mjamzito na kumkabidhi Nyaraka hiyo na mimi kurudi zangu Mbagala.

 

Je kipi kitaendelea?

Subiri matini ijayo.

Kumbuka haya ni makala ya Mgogoro wa Azania na Tambaza XXXV.

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com
0717649257

NB kwa msomaji wangu ambaye hakujaliwa kuzisoma matini hizi wakati zinaanza anaweza kutembelea ukurasa wangu wa facebook unaotambulika kama adeladius makwega au instragram kama adeladius,pia unaweza, kuzisoma kupitia Blog hii https://www.mwanakwetu.co.tz/

 , kuzisikiliza kupitia https://link.radioking.com/mwanakwetu-radio, kuzitazama kupitia MwAnAkWeTu TV https://www.youtube.com/@MwAnAkWeTutv. 

 

 

 

 

0/Post a Comment/Comments