MGOGORO WA AZANIA NA TAMBAZA XXXIX

 



Adeladius Makwega – DODOMA

Msomaji wangu, kumbuka tu hadi wakati huu ilikuwa ni mapema mwaka 1994. Nilikuwa bado nikiendelea kufuatilia kikao cha Bodi ya Rufaa kinafanyika lini. Utaratibu ulikuwa wa nenda rudi, nenda rudi; bado tarehe haijapangwa. Ufuatiliaji huo ulifanyika katika ofisi ya Jiji la Dar es Salaam, iliyopo kando ya Sokoine Drive.

 

Maisha ya Tambaza kwa hakika yalikuwa ya pekee sana, kwa kuwa shule hii iliwakusanya wanafunzi kutoka wilaya zote za Dar es Salaam, wanaotoka vijijini na mijini. Ndiyo maana ilikuwa shule ya vituko vingi sana vya kuchekesha na kusikitisha.

 

Katika darasa letu la R1 kulikuwa na wanafunzi karibu 45. Binafsi, kulikuwa na wanafunzi wanne ambao niliweza kujaliwa kufahamu kwao na wao kunifahamu kwetu. Wa kwanza ni Kahenya Katalama. Huyu alisoma shule ya msingi Muhimbili na aliishi katika Dar es Salaam School of Accountancy (DSA), Kurasini. Mama yake alikuwa mtumishi wa taasisi hiyo.

 

Ndugu huyu aliongea na mama yake na kumpa ruhusa tuwe tunajisomea katika vyumba vya madarasa ya chuo hicho. Kweli tuliruhusiwa kujisomea humo.

Mwanafunzi mwingine wa Tambaza niliyekufahamu vizuri ni Hamisi Ramadhani (Rashid Kazyoba). Huyu nimemtaja sana. Nilimfahamu kabla ya kwenda Tambaza kwa kuwa tulikuwa tunafanya naye mitihani ya kujipima katika shule ya msingi Mtoni (Mtoni kwa Mama Mere), pamoja na akina Seleiman Dewji, Hamisi Jangwa na wengine wengi.

 

Wa tatu ambaye nilikuwa nikimfahamu kwao ni Christian Maembe. Huyu alikuwa anakaa Mtoni Relini. Alikuwa kijana mpole sana, huku akiwa mpenzi wa nyimbo za reggae za Lucky Dube kama Baby Don’t Cry, Remember Me na I Got You Baby, huku akituimbia nyimbo hizo kila mara. Huyu ni ndugu wa msanii Vitalis Maembe, kama nilivyokueleza katika matini zilizotangulia.

 

Ndugu huyu nilimfahamu pia mapema kabla ya kwenda Tambaza kwa kuwa tulikuwa tunasali parokia moja (Parokia ya Mbagala), na mdogo wake, Vitalis Maembe, nilipokea naye Komunyo ya Kwanza mwaka 1988. Wao walitokea Mtoni Mtongani na mimi nilitokea Mbagala Sabasaba.

Mwanafunzi mwingine wa R1 niliyekuwa namfahamu hadi kwao ni Ibrahimu Liguo. Huyu jamaa aliishi Manzese, kwa ndani kidogo upande wa makabwela. Inakuwaje mwanafunzi wa Mbagala unamfahamu mwanafunzi wa Tambaza anayeishi mbali hivyo?

 

Kujibu swali hilo, tambua kuwa siku ya kwanza tu kuingia Tambaza Sekondari tuliingia darasani, kila mmoja akakaa anapopataka. Wanafunzi wakaanza kugombea pa kukaa katika baadhi ya maeneo ya darasa hilo. Wapo ambao hawakutaka kukaa mbele, na wengi walitaka kukaa madawati ya nyuma kwa dhana ya shule za msingi kwamba wasichana wanaketi mbele.

 

Nakumbuka siku hiyo tu ngumi zilipigana; kwa leo siwataji waliorushiana makonde, lakini madawati yalikuwa yanatosha kabisa.

 

Tukajulishwa kuwa kabla ya kuanza kwa masomo, walimu wa darasa watakuja, watajitambulisha, watatuita majina, halafu watatupanga namna ya kukaa darasani kwa mpango bora.

 

Kwa ukweli, hali ya shule za msingi zilikuwa mbaya sana, lakini si sekondari. Mathalani, katika shule ya msingi Mnazi Mmoja, kukaa chini kwa wanafunzi lilikuwa jambo la kawaida kabisa. Wasichana walikuwa wakija na vikapeti vidogo, wengine khanga, wakikaa chini, na mkondo mmoja ukiwa na wanafunzi hadi 100. Kwenye madawati walikaa wenye nguvu tu.

 

Nakumbuka kuna wakati Serikali ya Ali Hassan Mwinyi ilifanya oparesheni ya kuhakikisha mali zote za shule zilizoibwa zinarudishwa mashuleni na kwenye taasisi za umma. Hapa walilenga madawati na viti vya shule.

 

Mimi wakati huo nilikuwa nasoma shule ya msingi Mnazi Mmoja. Mara baada ya tangazo hilo, asubuhi yake nilifika pale jirani na Msikiti wa Manyema na Ofisi za Uhuru, nikakutana na mandhari ya viti na meza vilivyotapakaa baada ya kurudishwa usiku wa manane. Nina hakika sijawahi kuona oparesheni kama hiyo tena—oparesheni ya kurejesha samani za shule ambazo zilikuwa zinatumika katika mahoteli, mikahawa na majumbani mwa watu, hasa viti na meza za chuma baada ya kuibwa mashuleni Jijini Dar es Salaam.

 

Tukiwa darasani Tambaza, mwalimu wa darasa—mama mmoja mrefu, mweupe—alitupanga upya, na mimi nikakaa dawati moja na Ibrahimu Liguo. Hapo ndipo nilimfahamu huyu jamaa.

Kweli, serikali wakati huo walikuwa makini mno, tena mno. Je, leo hii wanafunzi wa shule za umma wanapoanza kidato cha kwanza wanapangwa darasani au wanaingia tu holela holela? Je, hayo madarasa yenyewe yana samani za kutosha, au wanakaa chini kama wakati ule wa miaka ya 1980 katika shule ya msingi Mnazi Mmoja?

Binafsi sina majibu, bali natambua msomaji wangu jibu unalo.

 

Sasa ngoja nirudi kwa Ibrahimu Liguo. Binafsi, nilikuwa sifahamu Manzese vizuri, lakini nilifika kwa akina Liguo, na yeye hakuwahi kufika Mbagala, lakini alifika kwa akina Makwega.

Kuna siku ndugu Liguo alikuja nyumbani kwetu, ambapo kulikuwa na binti mmoja wa Makwega anaolewa; tukasherekea. Wakati wa harusi, ndugu Liguo aliwaambia baadhi ya wadogo zangu kuwa yeye hajui Kiswahili na kwamba shuleni Tambaza tunazungumza Kiingereza tu.

 

Baadhi ya wadogo zangu waliokuwa shule ya msingi waliamini hilo. Hata walipomaliza shule ya msingi waliomba kujiunga na Tambaza, na kweli walifaulu na kujiunga na Tambaza mwaka 1994, akiwamo Mkomangi Mkundi (Gerald Stephen).

 

Kwa kuwa mimi na Ibrahimu Liguo tulikuwa marafiki sana, nayakumbuka matukio mengi juu yake. Kubwa kuliko yote ni siku ile nilipotoka kwa Mheshimiwa Peter Pinda aliponiambia niwafuate rafiki zangu watatu, akiwamo Ibrahimu Liguo, kama unavyokumbuka nilipita Tambaza Sekondari.

 

Hapo nilikutana na wanafunzi wengi. Nilipomaliza kuongea nao na kuwapa ujumbe wa ndugu Pinda, nilitaka kuondoka. Ibrahimu Liguo alinifuata akiniambia, “Makwega, usiondoke; kuna jambo nataka tuongee.” Nikamwambia sawa.

Akaniuliza, “Ulipokea zile shilingi 5,900/- kutoka mchango wa darasa kupitia Dunkani?” Nikamjibu ndiyo na kusema asanteni sana.

 

Akasema, “Mimi sikuchangia katika ule mchango kwa sababu nilikuwa na fedha yangu, lakini ilikuwa haijachenjiwa. Tangu siku ile nimekuwa nikiibeba kila siku shuleni ili nikupatie. Ngoja nikaichukue darasani nikupe.”

Akaenda darasani, akarudi na daftari lake lililokuwa limejaradiwa vizuri kwa gazeti. Akaifungua sehemu iliyojaradiwa, akatoa noti ya rangi ya kijani na akanipa.

“Pia nilikuwa naogopa ingeweza kupotea kama ningempa mtu, na ndiyo maana nimechelewa kukupa mchango huo. Nilikuwa najipanga nije Mbagala nikuletee; kwa kuwa umekuja, nenda kaichenji—itakusaidia sana.”

Mwanakwetu, nikiwa pale sikuitilia maanani, kwani mawazo yangu mengi yalikuwa kwenye masomo, na tayari shule ilikuwa imenipotea. Nilikaa nayo kwa siku mbili katika suruali ya jeans. Nilipoitazama vizuri ile pesa, nikaona picha ya Benjamin Franklin

, Rais wa zamani wa Marekani (nilivyodhani wakati huo). Nikatazama vizuri, kumbe ni noti ya dola 100 za Kimarekani.

 

Nikaiweka katika jinzi yangu nikaondoka. Sikuichenji mara moja; kwanza sikuamini kama ni pesa halisi. Niliikaa nayo muda mrefu. Baadaye nikamuonesha shangazi yangu wa NBC.

 

Akasema, “We mtoto, pesa hii umeitoa wapi?”

Nikamweleza namna wanafunzi wenzangu wa Tambaza walivyonichangia shilingi 5,900/- na pia namna Ibrahimu Liguo alivyonipa dola 100.

Kwa hiyo shangazi yangu alihitaji maelezo ya kina; akabaki na dola 100. Wakati huo Liguo, Atanas na Hamis walikuwa wanakwenda kwa mheshimiwa kutoa ushahidi.

Nilipomuuliza Liguo kuhusu dola 100, alinijibu kuwa tangu kidato cha kwanza alikuwa anakusanya pesa anazopewa na wazazi kwa matumizi ya shule na kuzibadilisha kuwa dola; zile zinazobaki. Hadi kidato cha tatu alikuwa na dola 100.

Akaniambia kuwa yeye alikuwa anafanya hivyo, na kwamba hata watu wengine wanahifadhi fedha zao katika vitu vya thamani kama almasi na dhahabu.

 

Nikarudi kwa shangazi yangu wa NBC kujieleza kwa kina, nikitamani Liguo afike naye amweleze shangazi yangu huyu anayefahamika kama Bernadeth Makwega.

Kwa bahati nzuri, shangazi huyu alinielewa vizuri, akaichenji na mimi nikapata shilingi 28,000/-. Pesa hiyo ilinisaidia mno, kwani ilikuwa fedha nyingi sana kwa kijana mdogo.

Mwanakwetu huyu, mfadhili wangu Ibrahimu Liguo, sasa ni Mkurugenzi wa Mipango katika Ofisi ya Msajili wa Hazina, ambayo awali ilikuwa chini ya Wizara ya Fedha na Mipango nchini Tanzania.

 

Sina hakika kama ndugu Liguo analikumbuka tukio hilo; leo nimkumbushe—sasa ni miaka 30 iliyopita—na dola yake 100 ya Kimarekani, ambayo sasa ni takribani shilingi 230,000 za Kitanzania kwa mwaka 2022.

makwadeladius@gmail.com
0717649257

MAELEZO YA PICHA

Picha ya kwanza ni 1R mwaka 1991, wakipiga picha darasani kwao. Tazama mstari wa mwisho jirani na ukuta: kuna mwanafunzi ameinama, anayefuata ni Adeladius Makwega, na anayefuata tena ni Ibrahimu Liguo.

Picha ya pili ni 1R1; ilikuwa ni siku hiyo hiyo. Aliyeshika skafu ya Robert Nesta Marley ni Adeladius Makwega, na aliyekaa mbele ya wanafunzi wote ni Ibrahimu Liguo.

Picha ya tatu na ya nne zote ni za Ibrahimu Liguo kama anavyoonekana sasa.

 

 

0/Post a Comment/Comments