MGOGORO WA AZANIA NA TAMBAZA XXXIV

 

Adeladius Makwega-DODOMA.

 

Msomaji wangu nakuomba kwa hisani yako nibaki katika kapu langu la maoni ambalo limesheheni maoni mengi, kwa hiyo naomba niendelee kuyapitia moja baada ya lingine.

Aliyevuja rekodi kutajwa katika maoni ni mribwende Faraja Kotta. Hoja ya kwanza ambayo imeibuka katika maoni haya ni urembo wa Faraja Kotta na Mama yake mzazi Bi Margareth Kotta, Je ni nani zaidi ?

 

Hoja hii imeibiliwa na wanafunzi wengi wa Tambaza walisoma shuleni hapo kwa kipindi tofauti, huku Mwalimu Kotta akifundisha masomo kadhaa ikiwamo Historia na hata Kifaransa.

 

“Kwa viwango vyetu sisi wahenga tunasema bila ya kupepesa macho kwamba Mwalimu wetu Mrs. Kotta was more beautiful (so many times) than the daughter- Mama Kotta alikuwa mrembo mara dufu ya binti yake.”

 

Alisema mwanafunzi mmoja wa Tambaza aliyehitimu miaka ya mwishoni mwaka 1970.

 

Ukiweka kando Mwalimu Kotta, mwalimu mwingine wa kike aliyefundisha Tambaza ambaye anatajwa kuwa mrembo mno ni Mwalimu Hirji huyu alikuwa chotara wa Kichaga.

 

Mwalimu Hirj anajaribu pia kushindanishwa na Mwalimu Margaret Kotta lakini bado Mwalimu Margareth Kotta aliibuka mshindi katika hilo.

 

Mwalimu mwingine aliyepata nafasi ya kufundisha Tambaza ambaye anatajwa kwa urembo ni Mwalimu Mdemu

 

Wanafunzi wa Tambaza tulitamani mno Mwalimu Mdemu kuja kutufundisha na bahati hiyo binafsi sikuipata kabisa lakini yale madarasa aliyofundisha kwanza wanafunzi wake walimpenda mno, wakivutiwa na mavazi yake na hata masomo yake alivyokuwa akifundisha na mwisho wa siku walifaulu mno. Huku Mwalimu Mdemu akiwa na desturi ya kubadilisha magari kila ajapo kazini.

Kwa bahati mbaya sekeseke la kuhamishwa walimu mwaka 1993 Mwalimu Mdemu alihamishiwa Forodhani ambapo nadhani huko ndipo alipostaafu utumishi wa umma. Nao wanafunzi wa Tambaza waliokuwa wakifundishwa na Mwalimu Mdemu wakibaki na kilio.

 

“Hata leo hii akifika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili lazima atakutana na kundi la wanafunzi wa Tambaza ambao ni madaktari aliowafundisha, nina imani akifika hapo anaweza kupona kabla hajapata matibabu.”

 

Aliniuma sikio mdau mmoja.

 

Msomaji wangu unaweza kujiuliza je Mwanakwetu yeye binafsi anasimama upande gani kati walimu hawa watatu Kotta, Hirj na Mdemu?

 

Kwa kusema Ukweli wa Mungu mimi niliwaona Kotta na Mdemu, Mwalimu Hirji sikujaliwa kumuona.

 

Binafsi nasema kuwa wote Mwalimu Mdemu na Mwalimu Kotta walikuwa warembo.

 

“Hakika hata tabasamu lake lilirandana na mwili wake, Margareth Kotta alikuwa mrembo sana, tumuombee pia Mungu ampunguzie adhabu ya kaburi yeye pamoja na mumewe maana sisi tulio hai leo hii, wajibu wetu kufanya na kutenda hayo na kila tunawapokumbuka kwa mema yao. Hiki Kiingereza chetu tunachotamba nacho kama si wao tulikuwa si lolote si chochote na wao kuna sehemu ya thawabu wanapata kutokana na sisi tunapoitumia elimu waliotupa kwa manufaa yetu ya jamii yetu ya Tanzania.”

 

Haya siyo yangu bali ni maoni ya Hussein Salehe.

 

makwadeladius @gmail.com

0717649257











0/Post a Comment/Comments