MGOGORO WA AZANIA NA TAMBAZA XXXII

 

Adeladius Makwega-DODOMA

 

Katika matini iliyotangulia nilitoa ahadi ya kuyajibu maswali mawili juu yule mwanasheria wa wizara ya sheria ambaye nilipewa nyaraka za rufaa ili kumpelekea na kukujulisha kile kilichomo katika nyaraka hiyo.

Naomba hili kwa leo niliweke kiporo ili niweze kujibu maswali yako msomaji wangu.

 

Wa kwanza kabisa kulirusha jarife la maoni ni ndugu Philemon Felix yeye anasema kuwa mke wa Brigedia Kotta anaitwa Margaret Kotta alikuwa mwalimu wa Tambaza sekondari na anasema yeye alimfundisha somo la Historia hapo hapo Tambaza kati ya mwaka 1976-1979.

Ndugu Felix anaiweka kalamu yake chini kwa kusema kuwa mama huyu ndiye binti yake wa mwisho ni huyu mrembo Faraja Kotta.

 

 

Maoni ndugu Ferix yanaungana na ya ndugu Daniel Mbura yeye anaanza na salaam ya Habari ndugu Makwega! Nilimjibu kwema.

 

“Faraja Kotta ameolewa na Lazaro Nyarandu Waziri wa zamani wa Maliasili, lakini sijui wanaishi wapi?”

 

Kwa maoni hayo ya ndugu Mbura yanatoa nafasi tumtafute Faraja Kotta mwenyewe ajibu swali hilo lakini kama ameolewa na Lazaro Nyarandu naamini alikuwa mbunge huko Singida ndiyo kusema Faraja Kotta anakaa Singida, kwa hiyo binti huyu alivuka mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma hadi Singida.

 

Ndiyo kusema watu Wasingida waliwazidi kete wajanja wa Jiji la Dar es Salaam, hongereni sana Wanyiramba na Wanyaturu. Itabidi ndugu zangu Wanyiramba mtengeneze Bahari Koko hapo Singida ili Faraja Kotta aweze kuwa anakwenda kutembelea bahari hiyo.

 

Maana mrembo huyu amezaliwa na kukulia kando ya Bahari ya Hindi, akitaka kwenda kupunga upepo baharini anatembea kwa dakika moja tu.

 

Naye Anicetus Kalinjuna anajitwika jarife la maswali kwa kuuliza juu ya saa ya Fausta aliichukua nani? Kulijibu swali hilo sasa naikumaliza uhondo wa simulizi hii, kwa kifupi ndugu watatu yaani Arone, Mohammed na Adeladius(Mwanakwetu) hawakushiriki kabisa katika tukio hilo bali alishiriki mtu mwingine ambaye sasa ni kiongozi kiroho na miongoni mwa wanafunzi wa 3R1 wakati huo ndugu huyu anaitwa Ngitu Pereira, ndugu Ngitu alisoma salama na wala hakupata msukusuko wowote na kumaliza kidato cha nne salama mwaka 1994.

 

Jambo hilo lilikuwa fumbo kwangu kwa miaka mingi hadi mwaka mwaka 2010 nikiwa mtumishi wa TBC nilijulishwa na walinzi wa shirika hilo kuwa nina mgeni getini.

 

Niliitikia wito huo na kukutana na ndugu niliyesoma naye miaka 17 iliyopita wakati huo, alinisalimu vizuri, huku kando akiwa na gari aina ya Toyota Hilux. Aliniuliza unanikumbuka nikajibu ndiyo huku nikimtaja jina lake unaitwa Ng’itu Pereira.

Binafsi nilijua ngufu Ng’itu alikuwa pengina anatangazo hapa TBC

 

Akiniambia kaka mimi nimekuja kuna jambo nataka tulizungumze linanisumbua kwa hiyo nilipotambua kuwa upo hapa nikasema ngoja nikuone tuzungumze. Ndani ya gari alilokuwamo kulikuwa na watu wengine alivuta kando upenuni mwa ukuta wa TBC BH hapo kuna barabara inakwenda sokoni.

 

Akilini mwanagu nikajiuliza huyu jamaa ana jambo gani?

 

Aliniuliza unalikumbuka lile tukio la Arone Sifuni, Mohammed Said na wewe? Nikacheka alafu nikasema nakumbuka kaka.

 

“Mimi nilifanya fujo zile na saa yake ya yule dada niliichukua mimi, sasa nimekuja hapa kukuomba msamaha, mimi sasa ni mtu wa Imani, nisamehe.”

 

Iliningia simanzi kidogo, nikamuuliza umemtafuta Arone Sifuni na Mohammed Said?

 

Akauliza kwani wako wapi?

Nikamjibu kuwa Arone Sifuni amefariki mwaka 1994 nayeye Mohammed Said sifahamu alipo.

 

Nikamjibu ndugu huyu kuwa mimi nimekusamehe. Kweli ndugu huyu aliniaga nayeye kuingia katika gari ile kuondoka zake na mimi kurudi kazini.

 

Nilikuwa nawasiliana naye sana, japokuwa sasa sina mawasiliano yake tena.

 

Kumbe ndugu huyu alikuwa akinitafuta kwa miaka mingi hata baadhi ya tuliosoma nao aliwaleleza juu ya jambo hilo. Wengi walistaajabu kwani hakuwa mwanafunzi mtundu shuleni hata kidogo na wala hakuna aliyeihsi hili.

Unayemdhani ndiye kumbe siye.

 

Nina Imani hata Arone Sifuni na huko alipo atakuwa amemsamehe ndugu huyu.

 

“Leo hii naifunga hoja hii ya saa kwa kusema kuwa usimkarisikie Yuda kumsaliti Bwana Yesu kwa kuwa pia imeandikwa Yuda atamsaliti Bwana Yesu.”

 

Msomaji wangu wa mwisho ameomba jina nisilitaje, anasema kuwa ndugu Peter Pinda mlipokuwa mkienda kwake hamkuwahi kukatazwa kuingia? Kwa ushahidi wa Ibrahimu Liguo, Hamisi Ramadhani , Emmanuel Yesaya, Heriheri Haggai , Bernad Lema na Atanas Luis na mimi hatukuwahi kukatazwa hata mara moja japokuwa alikuwa na mbwa wakali mno.

 

Kama nilivyosema katika matini zilizotanguliwa nina hakika alikuwa na cheo serikalini ndugu huyu lakini cheo hicho sikukifahamu. Lakini kwa mazingira yale ya majirani zake huku Jaji Mkude, huku Nsa Kaisi (mkuu wa mkoa), huku Brigedia Kotta na hata huku Jaji Augustino Ramadhan, nina hakika alikuwa mtu mkubwa.Lakini wakati huo alikuwa ni mtu anayefikika kwa urahisi tilia maanani yule Dereva wa Treni .

 

 

Niende mbali zaidi hata kile kitendo cha kufuga ng’ombe na watu wanachukua maziwa kwa bili au kununua hiyo nayo inatoa ishara kuwa unafikika kwa urahisi na majirani zako wanakuamini.

Binadamu asiye kuamini hawezi kuja kununua maziwa nyumbani kwako.

 

Kwa kuhitimisha maswali na maoni haya kwa leo natoa ushauri kwa watu wenye nafasi za umma wajitahidi wawe wanafikika kwa urahisi. Kwanza hiyo nafasi si yako bali hawa miloni Watanzania ndiyo wenye hiyo nafasi. Pili hiyo nafasi ni ya muda tu ukienda sana miaka 10-15 inagota unarudi kuwa mtu wa kawaida.

 

Mwingine anachukua nafasi hiyo badala yako kutoka kwa ile jamii maana hiyo nafasi haiwezi kubaki tupu.

 

Tatu unapopewa nafasi ya umma wewe ni mwakilishi wa upande unaotoka iwe dini, iwe kabila iwe eneo ulipozaliwa, jitahidi hawa jamaa wakufikie kwa urahisi.

 

Naomba nitoe mfano wakati Mahakama Kuu ya Tanzania Jaji Salumu Masatti akifanya kazi,  inadaiwa alitokea Ulanga, Wapogoro, Wandamba na Wangindo wakiwa na kesi Mahakama Kuu walipita kwanza kwa ndugu yao Jaji Masatti nyumbani kuomba ushauri wa kisheria kwa ndugu yao. Kama alitoa ushauri yeye mwenyewe au kuwatuma kwa wanasheria wengine lakini ndugu huyu aliwasaidia.

 

Hata kama wakishindwa kesi kwa kuwa walipokelewa vizuri na Jaji Masatti nyumbani kwake  wakirudi kijijini wanakutaja vizuri.

 

Mwisho natambua kuna hoja za usalama kwa yule mwenye nafasi, sawa lakini weka mazingira mazuri wakaguliwe wa staha na heshima ili mwisho wa siku nduguzo wakufikie, maana hao ndiyo uliozaliwa nao, kukua nao, kusoma nao na pengine ndiyo watakaukuzika.

Naomba niishie hapo kwa leo.

 Kumbuka haya ni makala ya Mgogoro wa Azania na Tambaza XXXII.

 

Nakutakia siku njema.

 

makwadeladius@gmail.com

0717649257










0/Post a Comment/Comments