Adeladius Makwega-DODOMA
Juma moja lilipita na sasa ilikuwa ni Novemba 12, 1993 nilimfuata shangazi yangu yule wa Sokoni Kariakoo kumuomba nauli ya kwenda Msasani ambapo wakati huo nilikuwa nalipa nauli ya mtu mzima kwenye basi na siyo shilingi 5/- ya mwanafunzi na nadhani nauli ya mtu mzima ilikuwa shilingi 15/-.
Nilipata nauli hiyo na kesho yake nilipita kwa Arone Sifuni ambaye alikuwa anaishi Mtaa Pemba nyumba nambari 1, nadhani watu wengi hata waliozaliwa na waliokulia Dar es Salaam huwa hawafahamu Mtaa wa Pemba unapoanzia bali wanauona tu pale jirani na Soko la Kariakoo.
Mtaa huu unaanzia jirani kabisa na kiwanda cha bia kwa hiyo ndiyo unashuka na kukatiza Msimbazi hadi kufika katika zile Bendera za Soko la Kariakoo jirani na lango kuu la kuingia Sokoni Kariakoo.
Arone Sifuni alikuwa ni Mpare kwa baba na Mmanyema kwa mama yake. Wazazi wake walikuwa hawakai pamoja na nilipofika kwao nilibaini kuwa alikuwa na jina lingine la nyumbani akiitwa Katisi, nadhani jina hilo alipewa kutokana na miaka ya 1960 1980 kulikuwa na mwanamuziki Mmarekani aliyekuwa anaitwa Katisi Brown.
Mimi na Arone Sifuni kabla ya kufukuzwa shule hatukuwa marafiki lakini baada ya kufukuzwa shule pamoja tulikuwa ni marafiki wa kujua cha kufanya baada ya shida, kumbuka kuwa hata shida zinaweza kuwafanya watu kuwa ndugu lakini Mohamed Said sikujaliwa kukufahamu kwake na sikumuona tena tangu Oktoba 1993.
Mama wa Arone alikuwa anamiliki nyumba hii ya Mtaa wa Pemba nambari moja na alikuwa na mtoto mmoja ambaye ni Arone, mama huyu alinipenda mno kwa hiyo nikifika kwake anasema ah Makwega kijana wa Mbagala hawajambo huko? Najibu hawajambo mama!
Na ndiye mama huyu aliniyenifundisha kulitaja mno jina la Mbagala
Arone leo hayupo ametoka yupo kwa rafiki zake vijiweni, najibu haya mama akirudi mwambie Makwega kapita ninaenda Msasani kufuatilia lile suala langu kwa yule ndugu anayenisaidia. Mama huyu alijibu sawa pia hata Baba yake Arone analifuatilia
.
Nilibaini kuwa Baba wa Arone aliyekuwa anakaa Chang’ombe alikuwa mtumishi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Siku hii nilitoka zangu Mtaa wa Pemba hadi Stesheni kwa mguu, nakupanda basi la Saa 9 mchana kwenda Msasani nakushuka Morogoro Stoo, niliuchapa mguu hadi kwa ndugu Peter.
Nikiwa pale nje ya makazi haya alikuja mzee mmoja mtu mzima sana ambaye kwa utafiti wangu aliniambia kuwa alikuwa Dereva wa Treni kwa hiyo alipata matatizo kazini, alifika hapo nayeye alikuwa akisaidiwa na ndugu Peter kwani wanazaliwa wilaya moja.
Ndugu huu aliniuia na wewe na mimi nilimjibu kuwa sisi ni wanafunzi wa Tambaza tunamgonja anatusaidia katika shauri letu, mzee huyu alisema hilo lenu dogo na litakwisha tu.
Ndugu huyu alisema kuwa yeye alielekezwa na Waziri Segera Nswima amuone ndugu Peter Pinda.
Ndugu Peter alirudi kazini akiwa anaendesha gari aina ya Land Cruez (Hard Top nyeupe) alishuka na mkoba mweusi na mara vijana wake wakaja kumpokea.
Walipokuwa wakimsalimia walikuwa wakipiga magoti, mimi nilishangaa, yule Dereva wa Treni aliniambia kuwa hiyo ndiyo heshima ya kwetu.
Alikaa ndani kwa dakika kama tano, mara alimuita yule ndugu Dereva wa Treni akazungumza naye kwa muda kidogo, dereva wa Treni mara akatoka na kuondoka zake. Ndugu Peter akamtuma kijana wake akasema ebu liite hilo dume la Tambaza liingie ndani, kweli huyu kijana akaja akaniita kwa utani kumbe wewe ndiyo dume la Tambaza? Unaitwa uingie sebuleni .
Kweli nilibaki hapo sebuleni hadi saa 11.30 jioni, alikuja dada mmoja mrefu, mweusi, weusi wake unag’hara vizuri sana, nywele zake alizichana akazifunga na kibanio, juu alivaa blauz nyeupe na sketi ya rangi kama udongo. Aliposhushwa na gari ambalo sikuliona kwa kuwa nilikuwa nimezibwa na mti wa mkrisimasi na gari hilo lilipomshusha tu likaondoka masikio yangu yalisikia tu miungurumo yake.
Sikumpa shikamoo dada huyu, nilimuona kama mzao wangu, aliingia sebuleni na baada ya dakika kama tano ndugu Peter akaja sebuleni akiwa ameshika karatasi nyingi kama kitabu, akivikagua vilikuwa kama vitano.
“Nyaraka hizi chukua peleka nyumbani, mpe baba yako asaini hapa na hapa na hapa katika vitabu vyote vitano alafu vipeleke jiji kwa afisa elimu sekondari kwa nakala tatu hizo mbili unirudishe hapa.”
Nikabeba vile vitabu vyangu akamwambia kijana mmoja mweupe mfupi dereva kutupeleka kwa gari yake pickup nyeupe, mimi pamoja na huyu dada mweusi, mimi nilikaa nyuma sehemu ya wazi, dada mweusi na dereva walikaa mbele. Pick up hii ilienda hadi Chang’ombe jirani na Kibasila Sekondari akashuka dada huyu.
Dereva akaniita njoo ukae mbele nikakushushe Polisi Chang’ombe, kweli alifanya hivyo. Tukiwa ndani ya gari lile tulikuwa tunamsifia yule dada mweusi namna alivyokuwa mrembo kwa uzuri wake wa asili.
Nikuume sikio msomaji wangu kuwa baada ya miaka 10 nilikuja kubaini kuwa yule dada mrembo, mweusi, aliyefunga nywele kwa nyuma Novemba mwaka 1993, niliyemnyima shikamoo yangu, ambaye tulimsifia mno na dereva kumbe alikuwa ndiye Mama Tunu Pinda.
Mimi nikashuka Polisi Chang’ombe nikatembea kwa mguu hadi Temeke mwisho nakupanda Chai Maharage hadi Mbagala.
Nilifika muda ule ule na nakumfuata mzee ili asaini nyaraka hizo ambazo moja ilikuwa na kurasa kama 70 saini ilitakiwa kuwekwa ukurasa wa mwisho. Nilipofika nyumbani nyaraka hizo mzee hakuzisaini, nilirudi kwa shangazi yangu wa Sokoni Kariakoo kumueleza, aliniambia nidamkie kwa ndugu Peter atalitatua tu hilo.
Asubuhi nikamdamkia kwa ndugu Peter ambapo aliniambia nisitoke, kwanza alikwenda kazini kwake na nyaraka zile, baadaye akanipitia akaniongoza hadi Jiji Dar es Salaam kwa afisa elimu wa mkoa na kuzikabidhi.
Pale Jiji Dar es Salaam wakaniambia kijana usiwe unamsumbua mzee uwe unakuja hapa kuulizia rufaa yako kila wiki.
Ndugu Peter nakala tatu alizibakiza jiji, nakala mbili alitoka nazo, moja aliiweka katika gari lake na moja alinipa nikampe jamaa mwingine wizara ya sheria.
Je jamaa huyo niliyekuwa natakiwa kumpa nakala moja alikuwa ni nani? Je nakala hiyo ilikuwa imeandikwa nini?
Subiri matini ijayo
Kumbuka haya ni makala ya Mgogoro wa Azania na tambaza XXXI.
Nakutakia siku Njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
.gif)





.gif)
Post a Comment