MGOGORO WA AZANIA NA TAMBAZA XXVI

 





Adeladius Makwega-DODOMA

 

Katika matini iliyotangulia nilieleza namna mwanafunzi wa Jangwani wa kidato cha tatu Fausta alivyoingia Tambaza na namna alivyookolewa na Atanas Luis (Mzee Ole) na kuchukuliwa na walimu kwenda katika ofisi ya makamu mkuu wa shule ya Tambaza na huko akiandika maelezo juu ya namna alivyofika Tambaza na kipi kilitokea.

Kwa hakika Fausta alipoteza saa yake ya mkononi. Kwa kuwa tukio hilo lilitokea jirani na kidato cha tatu mkondo wa 3RI wanafunzi wote wa mkondo huo walitakiwa kuandika maelezo huku maelezo hayo yakilinganishwa na maelezo ya Fausta ya awali.

Kumbuka tu Fausta aliokolewa na Atanas Luis kwa hiyo Atanas Luis ambaye naye alikuwa akitokea 3RI nayeye karatasi ya kuandika maelezo ilimuhusu japokuwa alifanya wokovu kwa Fausta ambaye walisoma wote shule msingi.

 

Kwa hiyo maelezo yaliandikwa na wanafunzi wote zaidi ya 40 wa 3R1 na maelezo hayo kusomwa na walimu huku ikiwa ngumu kutambua aliyehusika kumfanyia fujo dada yetu huyu.

 

Maamuzi ya kamati ya nidhamu ya walimu ya shule ya Tambaza yalikuwa darasa nzima ya 3R1 wachalazwe bakora sita sita kila mmoja na liwe onyo la mwisho

Kweli Kengele iligongwa na wanafunzi wote wakaitika mbele ya hadhara tangu kidato cha kwanza hadi cha sita na kosa hilo likasomwa na darasa zima la 3R1 wakachapwa fimbo sita kila mmoja.

Nakumbuka miongoni mwa walicharaza fimbo hizo sita alikuwapo injini Wille John, wakati huo alikuwa kijana mrefu sana mwenye mwili mkubwa na mweupe sana Injinia wa Sautiwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mohammed Khalifani maaru kama Jemapere. Injini Wille John wakati alipokuwa akichapwa fimbo hizo zilikuwa zikimuingia vilivyo kwa hiyo makamu mkuu wa shule Wajimila alitumia muda mwingi kumaliza kumchapa mheshimiwa huyu fimbo hizo sita.

 

Kitendo cha kuwachapa wanafunzi 40 fimbo sita nayo ni adhabu kubwa kwa mwalimu anayehusika na zoezi hilo, kwa hiyo makamu mkuu wa shule alipomaliza kumchapa injini Wille John aliomba msaada wa walimu wengine kuendelea na zoezi hilo.

Hapa Mwanakwetu nayeye alicharazwa bakora sita na mwalimu mmoja wa kike ambaye hakumtambua jina lake.


Suala hilo tukajua limekwisha huku wanafunzi wa 3R1 na wengine wakiendelea na masomo kama kawaida. Kwa desturi ya Tambaza vituko vingi vilikuwa vinafanywa na wanafunzi wa kidato cha pili, kidato cha tatu lilikuwa ni darasa tulivu mno, kama ilivyo kidato cha nne, tano na sita kwa kuwa sasa wanajiandaa kuingia kidato cha nne.

 












Kwa desturi ya shule ile wakati ule kidato cha tatu na cha nne waliweza kushiriki katika vituko kadhaa kwa nadra mno kama kimemkuta jirani na yeye tu lakini siyo kwa kukifungia safari kama walivyokuwa kidato cha kwanza na cha pili, ambapo wao vituko vyote waliviita pikiniki.

Baada ya miezi miwili, ilibainika kuwa suala hilo lilikuwa linaendelea chini kwa chini Mwalimu Mtera na Mwalimu Wajimila walipokuwa wanaingiza zile barua za maelezo ya wanafunzi wa 3R1 katika mafaili yao walibaini kitu, kwa hiyo waliamua kuyapitia mafaili yote ya kila mwanafunzi mwenye barua zaidi ya moja ya makosa ya nyuma katika faili lake aliorodheshwa.

Hilo lilibainika kupitia watumishi wa Tambaza ambao walibakizwa shuleni hapo baada ya walimu kuondoka na baadhi yao walikuwa na wanafunzi ndugu zao wakisoma shuleni hapo.

Kwa hiyo kati ya darasa la wanafunzi 40 yalipatikana majina 15 na wengine waliingizwa humo kutokana na kuwa viongozi wa darasa pia. Majina ninayoyakumbuka ni Edga Chibura, Atanas Luis, Said Masoud, Aron Sifuni, Mwanakwetu(Adeladius Makwega) na Mohammed Said Mzukizi (japokuwa hakusoma 3R1).

 

Katika simulizi hii awali nilikueleza juu ya bodi ya mpya ya Tambaza sekondari ambayo iliundwa baada ya shule kufungwa na kufunguliwa huku ikiwa na wajumbe wengi kutoka vyombo vya ulinzi na usalama.

Swali la kujiuliza wanafunzi wa Tambaza walilifahamu vipi hilo?

Jibu lake ni kuwa wajumbe wa bodi za shule inashauriwa kuwa miongoni mwa wazazi wenye watoto shule au wale wanaoishi jirani na eneo hilo, namkumbuka mjumbe mmoja wa bodi hii alikuwa Mzee Agrey Mwambene ambaye alikuwa na mwanawe Tambaza sekondari , huyu mzee alikuwa mtumishi wa Wizara ya Mambo ya Ndani pale Dar es Salaam jirani na Posta Mpya huku akiwa mkazi wa Mbagala.

 

Kwa hiyo kila mjumbe alipokuwa akifika katika vikao hivyo wanafunzi wa Tambaza waliwasonta vidole kwa kazi walizokuwa wakifanya, hilo lilileta mjumuisho wa wajumbe wengi kutoka katika vyombo. Hivyo

Kesi iliendelea kumbuka wale wanafunzi 15 walipekwa mbele ya Bodi ya Shule.

 

Msomaji wangu nikikurudisha nyuma zaidi kumbuka nilisema Fausta alisoma darasa moja na Atanas Luis kwa hiyo wakafaulu pamoja Atanas akaenda Tambaza, naye Fausta Binti Mrembo akaenda Jangwani. Fausta Binti Mrembo akiwa Jangwani, kwa sasa Fausta mtumishi wa umma kwa sasa na mama wa familia yake, mwenye watoto wawili wakubwa wa kiume.


Ifahamike wazi kuwa Fausta na Atanas pia walikuwa wakisali pamoja na hata komuniyo ya kwanza walipokea pamoja, kwa hiyo kwa habari za utoto walikuwa wakifahamiana mno walikuwa zaidi ya ndugu

 

Kumbuka wanafunzi 15 wa  3RI wapo matatani  na kwa baadhi ya wanafunzi waliokuwa wakubwa na wakilitazama shauri hilo kwa mbali na wakifahamu udugu huo wa Fausta na Atanas, walimuomba Atanas amfuate Fausta kumuomba akiitwa katika Bodi ya Shule ya Tambaza asifike.

 

Atanas Luis alifanya hivyo kuokoa jahazi la darasa lake, huku akiugulia fimbo sita mbele ya hadhara.

“Kule shuleni mambo yamekuwa mabaya na tutafukuzwa shule na majina 15 yamepelekwa katika bodi ya shule kuhojiwa na desturi ya bodi hiyo tutafukuzwa shule sasa tunakuomba ukiitwa usije.” Aliombwa Fausta.

Fausta alimsikiliza vizuri Atanas Luis. Nyuma ya pazia baadhi ya wanafunzi wakisema kuwa Fausta amemtaja kijana mmoja mweupe sana akimuita mzungu ndiye aliyemfanyia fujo, Fausta alisema akimuona anamkumbuka lakini mbona wanafunzi wengine weusi tii kama akina Mwanakwetu wameingizwa humo?

Sasa Atanas Luis ameshaongea na Fausta lakini naye Fausta alieleza kuwa mkuu wa shule ya Jangwani amemuita na kumueleza amepokea barua ya wito wa kumruhusu binti huyo kushiriki kikao cha Bodi ya Nidhamu ya Tambaza ili kutoa ushahidi. Maelezo haya ya Fausta yalimpa kitete zaidi Atanas Luis na sote tulikuwamo katika kadhia hiyo.

Nao watumishi wa Tambaza wakisema kuwa wajumbe wa Bodi ya shule hii wamedai kuwa itakuwa jambo jema kama mwanafunzi Fausta wamfuatwe Jangwani sekondari ili kuondoa mizengwe na vitisho vya wanafunzi wa Tambaza na Fausta atoe ushahidi kwa uhuru.

Hata Fausta mwenyewe akiwa na mashaka juu ya safari yake ya kwenda Tambaza ilikuwa na nia gani? Hapa kila mmoja alijawa na kitete

Je kipi kitaendelea ?

Subiri matini ijayo.

Kumbuka haya ni makala ya Mgogoro wa Azania na Tambaza XXVI.

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com
0717649257

 

 

 

 

0/Post a Comment/Comments