Adeladius Makwega – Butiama
Shule ya Tambaza kwa miaka mingi ilikuwa na maabara bora za masomo ya sayansi. Hali hiyo ilifanya wanafunzi wengi kuchagua kusoma masomo hayo, huku wakijitahidi pia katika masomo mengine. Ndiyo maana nimeeleza kwa kina katika matini zilizotangulia kuhusu wasomi kadhaa wa masomo ya Biashara na Mahesabu, akiwamo CAG Dkt. Charles Kicheere na hata aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Katanga.
Unapotaja madaktari na mainjinia waliosoma shule hii, ni wengi mno, kutokana na mazingira bora ya maabara.
Ubora wa maabara hizo uliwashawishi hata walimu wageni kutoka shule nyingine kuwaleta wanafunzi wao wa masomo ya ziada Tambaza kwa ajili ya kufundishwa. Hivyo, ilikuwa jambo la kawaida kuona wanafunzi kutoka shule nyingine za Dar es Salaam wakija Tambaza kwa masomo ya ziada.
Miongoni mwa wanafunzi waliokuja kusoma masomo hayo alikuwa binti mmoja kutoka Shule ya Sekondari Zanaki, ambaye alikuwa dada wa mwanafunzi wa Tambaza aliyejulikana kama Muchunguzi Kamugisha (Mulokozi Kamugisha). Binti huyu hakupata tabu sana, kwa kuwa ndugu yake alikuwa shuleni hapo. Hata wanafunzi wa Tambaza waliojaribu kumsumbua, walikumbana na ulinzi mkali kutoka kwa Kamugisha.
“Kamugisha,
hebu tuache tuzungumze na dada yako!”
Naye akajibu: “MwachenI dada yangu; amekuja kusoma, na hapa hakuna atakayemuoa.
Sitaki usumbufu—mwacheni!”
Msomaji wangu, tambua kuwa binti huyu alipata marafiki wengi waliotaka kujenga naye udugu. Hata hivyo, kwa uchunguzi wa Mwanakwetu, hakuna aliyefanikiwa kuwa na ukaribu mkubwa naye. Kizuizi kikubwa kilikuwa ndugu yake, Muchunguzi Kamugisha, pamoja na mwalimu aliyekuwa akimfundisha masomo ya ziada.
Aidha, kitendo cha wanafunzi kumsumbua binti huyu kilimkera sana mwalimu huyo. Ilibainika pia kuwa mwalimu na binti huyu walikuwa wa kabila moja na familia zao zilikuwa na uhusiano wa karibu.
“Kamugisha, unataka kumuoa mwenyewe? Mwenye dada hakosi shemeji! Au mwalimu tayari kashalipa mahari?”
Maneno hayo yalikuwa yakirudiwa mara kwa mara na wanafunzi wa Tambaza, yakimfikia Kamugisha kama santuri iliyokwama.
Hali hiyo ilimkwaza sana mwalimu aliyekuwa akimfundisha binti huyu wa Zanaki. Kutokana na hilo, wanafunzi kadhaa waliokuwa wakijaribu kumsogelea walijikuta wakiandika maelezo na hata kupewa adhabu ya kufyeka katika viwanja vya shule, jirani na Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST).
Hatimaye, mwalimu huyo alishinda “vita” hii kwa kuhakikisha binti huyo anasoma kwa bidii. Alifanya mtihani wake wa kidato cha nne mwaka 1993 katika Shule ya Sekondari Zanaki na kufaulu vizuri. Mwanakwetu alichunguza zaidi na kubaini kuwa mwalimu huyo wakati huo alikuwa bado hajaoa—huenda naye alikuwa na nia ya kumposa binti huyo baada ya kumaliza shule.
“Ndoano” ya mwalimu ilikuwa na chambo cha aina mbili: kwanza, elimu aliyokuwa akimpatia binti huyo, na pili, kipato chake kama mwalimu.
Hivyo, ushindi wa mwalimu haukuwa na mjadala. Swali linalobaki ni moja: je, aliweza kumuoa binti huyo? Hilo linabaki kuwa kitendawili kwa sasa.
Ujio wa wanafunzi wa kike shuleni hapo haukupokelewa vizuri sana. Mara tu binti alipofika, kelele, vifijo, miluzi, makofi na mayowe vilitawala. Wakati mwingine, hata binti aliyekuwa akipita tu kutoka Shule ya Sekondari Jangwani jirani na Tambaza alipata msisimko huo.
Kulikuwa na kijana mmoja aliyesoma Tambaza mwaka 1993, kidato cha tatu, aliyejulikana kama Peter Sisya. Alikuwa na dada yake ambaye walifanana sana, kana kwamba ni mapacha. Dada huyu alikuwa akisoma Jangwani Sekondari. Kila siku alipita karibu na STAMICO, iliyo mkabala na Tambaza, akielekea shuleni au nyumbani Upanga.
Peter Sisya alikuwa na marafiki wengi, akiwamo Mwanakwetu, hasa kutokana na umaarufu wa dada yake, ambaye pia alikuwa mrembo.
Wasichana kutoka shule nyingine pia walifika Tambaza kuwasalimia ndugu zao au wazazi waliokuwa wakifanya kazi hapo. Hali ya kuwashangilia iliendelea kama kawaida, jambo lililosababisha hata dada wa Peter Sisya kubadilisha njia ili kuepuka vurugu hizo.
Nakumbuka siku moja tukiwa darasa la 3R1, alifika binti mmoja kutoka Jangwani Sekondari. Kama ilivyokuwa desturi, wanafunzi walimshangilia sana hadi shule nzima ilitoka madarasani kumtazama. Alifika karibu na darasa letu kumfuata kaka yake.
Binti huyu aliwahi kusoma shule ya msingi na kijana mmoja aliyejulikana kama Atanas Luis, ambaye alikuwa bingwa wa michezo ya ngumi, karate na mingineyo.
Kelele hizo zilisababisha taharuki kubwa shuleni. Atanas Luis alijitokeza na kumuita: “Fausta, njoo!” Kisha akamlinda na kumpeleka karibu na ofisi ya utawala.
Wakati huo, saa ya mkononi ya binti huyo ilipotea bila kufahamika ni nani aliyeichukua. Walimu walimchukua na kumtaka aandike maelezo ya tukio hilo mara moja.
Baada ya kuandika maelezo yake, Makamu Mkuu wa Shule, ndugu Wajimila, alimwambia: “Rudi shuleni kwako, lakini tutaendelea kukuhitaji kwa maelezo zaidi na ushahidi.”
Fausta aliondoka akiwa salama, akisindikizwa na kaka yake pamoja na Atanas Luis.
Kwa kuwa tukio hilo lilihusisha darasa la 3R1, kila mwanafunzi wa darasa hilo alitakiwa kuandika maelezo. Vinginevyo, darasa zima lingefukuzwa shule.
“Sisi tupo hapa kuhakikisha tunadumisha nidhamu. Hatuwezi kuvumilia wanaoiletea Tambaza sifa mbaya. Hatutasita kufukuza darasa zima ikiwa itabidi. Tunataka kuwajua walioanzisha vurugu hizi—ni kina nani?”
Alisema Mwalimu Wajimila, akiwa ameongozana na mwalimu wa nidhamu.
Je, nini kitaendelea? Subiri matini ijayo.
Kumbuka, haya ni makala ya “Mgogoro wa Azania na Tambaza XXV.”
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
.gif)










.gif)
Post a Comment