MGOGORO WA AZANIA NA TAMBAZA XXIII

 



Adeladius Makwega – Dodoma

Katika matini ya XXI, bila shaka msomaji wangu unakumbuka namna nilivyogusia nafasi ya CAG tangu mwaka 1961 hadi mwaka 2022, ambapo hadi mwaka 2026 ilikuwa inaongozwa na Ndugu Charles Kicheere, ambaye ni miongoni mwa wanafunzi waliosoma Tambaza.

 

Katika matini hiyo, unakumbuka nilieleza umahiri wa ndugu yetu huyu katika somo la Kiingereza, ambapo alipata alama ya A akiwa mwanafunzi pekee. A hiyo ya Charles Kicheere ilileta gumzo kubwa shuleni Tambaza kuanzia kwa walimu hadi wanafunzi.

Gumzo la alama hiyo ya A katika somo la English Language lilikuwa mjadala mkubwa ulioibuka shuleni Tambaza wakati huo, lakini pia lilichagizwa na utani wa wanafunzi miongoni mwao:

 

“Mimi nimepata A, nyie wote mmenifuata, kwa hiyo mimi ni bingwa wa Kiingereza Tambaza nzima.Mimi ni bingwa wa Kiingereza  Dar es Salaam nzima , mimi ni bingwa wa Kiingereza  Tanzania nzima.”

 

Japokuwa Charles Kicheere mwenyewe sasa ana msimamo tofauti na hoja hii ya kuwalinganisha wenzake kwa alama hiyo ya Kiingereza na kupita majumbani kujisifia.

 

Jambo jingine la ziada kuhusu ndugu huyu ni kwamba aliishi pia Kariakoo, mtaa wa Sikukuu, nyumba namba 10.

 


Kukuongezea, msomaji wangu, tambua kuwa Charles Kicheere alipomaliza kidato cha nne alipata Divisheni I ya pointi 9, akipata alama A sita katika masomo ya History, Geography, Book Keeping, Commerce, English Language na Siasa.

 

Kwa hiyo, Mwanakwetu, tambua kuwa ndugu huyu pia alikuwa bingwa wa somo la Siasa, ambalo baadaye baada ya kuingia mfumo wa vyama vingi, lilibadilika na kuwa Uraia (Civics/General Studies).

 

Mwaka huo, Tambaza hawakuwa na Divisheni I ya pointi 7 wala 8; hivyo Divisheni I ilianza na pointi 9, ambayo ilipatikana kwa wanafunzi wawili tu: Charles Kicheere na mwenzake aliyeitwa Thomas Marwa (nitamtafuta nijue alipo ndugu huyu).

 

“Charles Kicheere alifika kwangu akijinasibu sana baada ya matokeo kutoka, na kweli wenzangu wengine waliniambia kuwa alipita kwao. Mimi nilimpa pongezi, japokuwa mimi nilipata alama C ya English Language.”

 

Anasema mdau mmoja aliyekuwa darasa moja na ndugu yetu huyu.

 

Mwanakwetu, hebu tumuache CAG wetu tangu mwaka 2019, Dkt. Charles Kicheere, aendelee na majukumu yake matatu kama ibara ya 143(ii)(a), (b) na (c) inavyotajwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na marekebisho yake ya mara kwa mara.

 

Kwa heshima zote, nafungua ukurasa wa maoni kuhusu Dkt. Charles Kicheere kwa leo. Kwa heshima zote nakushukuru sana kwako CAG hasa kwa kunitafuta na kunieleza upende wako juu ya ukweli wa mambo ulivyokuwa juu ya A yako ya English Language ila nakuomba Dkt. Charles Kicheere usiwatume vijana wako wakaja kunipiga hoja huku nilipo.

 


Hata hivyo, msomaji usiwe na shaka haya ni mambo ya Tambaza Mwanakwetu anaongea na kaka zake lakini kumbuka kuwa Dkt. Charles Kicheere mwenyewe, alipowasiliana na Mwanakwetu, alikana kupita majumbani kujisifia alama yake ya Kiingereza. Lakini hakukanusha kupata Divisheni I ya pointi 9 pamoja na A zake sita, ikiwamo ya Siasa.

Msomaji wangu, natambua kuwa mfungo wa Ramadhani unaendelea. Naomba niendelee kukuzawadia ubeti mwingine wa Ramadhani:

Mola ondoa ukame, waokoe wakulima,
Mvua usiwanyime, mazao yatasimama,
Dua zote tuzisome leo, kesho na daima,
Ramadhani imefika, Mola tusamehe dhambi.

Kumbuka, haya ni makala ya XXIII ya Mgogoro wa Azania na Tambaza.

Nakutakia siku njema.

Mawasiliano:
makwadeladius@gmail.com
0717 649 257

 

 

 

 

0/Post a Comment/Comments