Adeladius Makwega-DODOMA.
Hali ya Shule ya Sekondari Tambaza iliendelea kuwa ya mivutano mikubwa baina ya walimu wapya shuleni hapo akiwamo mwalimu Mkuu Ndugu Mtera, Wajimila Mkuu Msaidizi na walimu wengine kama mwalimu Songo maarufu kama mwalimu Nyau.
Kanuni iliyokuwapo ilikuwa kila linapotokea tukio basi kufukuzana shule ilikuwa kawaida mno. Hapo sasa wazazi wengi waliokuwa na nafasi waliwahamisha watoto wao na waliobaki walisoma kwa kupitia changamoto nyingi.
Kumbuka shule hii ilifungwa kwa muda mrefu, huku wanafunzi kadhaa wakibaki majumbani bila ya kusoma lakini sasa shule imefunguliwa na hali hii ilikuwa ya mapambano mwanzo mwisho, huku kukiwa na taswira kuwa sasa serikali ilikuwa imeagiza kuwa wanafunzi wa Tambaza lazima wadhibitiwe kwa gharama zozote zile. kwani wao ni kina nani?
Navyo vyombo vya habari vikijaribu kuandika habari kadhaa juu ya hali ya shule hii.
Labda msomaji wangu nikurudishe nyuma kidogo, muda mfupi kabla ya walimu wa zamani hawajahamishwa, wanahabari kadhaa wa magazeti waliwahi kufika shuleni hapo ili kuandika na kupiga picha ya hali ya shule hiyo ilivyo. Magazeti yalichapisha picha za wanafunzi wa Tambaza wakiwa katika magenge yao.
Shuleni hapo kulikuwa na magenge maeneo mbalimbali likiwamo genge jirani na bwalo la chakula. Pahala hapo palikuwa na vyuma vya kunyanyua vya kilo kadhaa na bingwa wa kubeba vyuma vyenye kilo zaidi ya vyote alikuwa ni Wiliam Damson (Puzza). Vyuma hivyo vilitengenezwa wakati DANIDA wanafanya ukarabati wa majengo ya shule hii kwani wanafunzi wa Tambaza waliwaomba mafundi wakawatengezea bila hiana.
Waandishi wa habari hao ambao walifika shuleni hapo walijitambulisha kwa uongozi wa shuleni siku kadhaa wakikusanya taarifa za matukio mabaya ya wanafunzi na huku habari hizo zikitoka katika magazeti mbalimbali kama vile Uhuru, Mfanyakazi, Mzalendo Daily News na Sunday News. Wakiwa katika kazi hiyo wanafunzi wa Tambaza walibaini hilo huku nao kuwafuatilia wanahabari hao.
Siku ya pili walipofika wanahabari hao waliingia na pikipiki aina ya XL ambayo ilipaki katika upande wa mbele wa Tambaza na kuingia kwa Mkuu wa Shule Julius Mushi na kuzungumza naye na wao kuendelea na kazi yao hiyo.
Wanafunzi wa Tambaza walijulishana kuwa jamaa hawa wameingia. Wakalifanyia kazi hilo huku wanahabari hao wakipiga picha kadhaa. Walipomaliza kazi walirudi kwa Mkuu wa Shule ya Tambaza na kumuaga kuwa kazi imekamilika.
Wakaenda kwenye pikipiki yao na pale walipofika walipotaka kupanda pikipiki hiyo walibaini kuwa mikoba yao iliyokuwa na vifaa vya kazi waliyoiacha pale haipo. Walirudi hadi kwa Mkuu wa Shule hii nakumueleza tukio hilo.
Mwalimu Julius Mushi anafanyaje katika hilo?
Alichanganyikiwa kabisa na akitambua kuwa wanahabari hao wataenda kuindika vibaya shule hii zaidi baada ya tukio hilo.
Jambo hilo lilijadiliwa kwa nusu saa na ikapigwa kengele ya dharura ambapo wanafunzi wote wa Tambaza kundi la walioingia asubuhi waliokuwa wakitoka na wale waliokuwa wakiingia mchana walikusanyika.
Walimu, watumishi wote wa Tambaza na mwalimu Mkuu Msaidizi walifika mstarini wakawa wakimsubiri Mkuu wa Shule hii ili asema kuna nini?
Julius Mushi, mwalimu mmoja mrefu, mweupe sana, mwembamba, nadhifu sana ambaye alikuwa amevalia miwani mieupe aliongozana na jamaa wawili mwingine akiwa na kamera shingoni.
“Hamjambo Wanangu? Mnatambua kuwa nyinyi hapa mnasoma, mkimaliza shule mtaingia katika taaluma mbalimbali, wengine walimu kama mimi, wengine madaktari, wengine wahasibu, wengine mainjinia na wengine mtakuwa wanahabari. Hawa hapa pembezoni kwangu ni wanahabari walikuja hapa kufanya kazi zao za kihabari na walipita ofisini kwangu, wamefanya kazi zao, walipomaliza tu wamefika kuniaga, walipokuwa wakiondoka katika pikipiki yao wamebaini kuwa mkoba wao haupo, basi ninawaombeni yule aliyeuona na kusogeza kando naomba aurejeshe.”
Ndani ya mkoba huo kulikuwa na nini? Julius Mushi aliwauliza jamaa hawa, mpiga picha ambaye aliongea kwa lafudhi ya Kiswahili cha Kijaluo (Tukidhani ni Mkenya) alijibu kuwa kulikuwa na kibali cha kusafiria, Kamera moja ya ziada na frash mbili za kamera hizo.
Alipomaliza kutaja vifaa hivyo mwanahabari huyu,J ulius Mushi(Mkuu wa Shule) aliwaomba wanahabari hao wajitambulishe mbele ya wanafunzi wa Tambaza na walifanya hivyo huku wanafunzi wa Tambaza wakicheka kwa tukio hilo.
Kweli baada ya ya siku mbili Mkuu wa Shule ya Tambaza Julius Mushi aliandika katika ubao wa matangazo shukrani kwa kupatikana kibali cha kusafiria cha wanahabari hao.
Baada ya muda mchache ndipo walimu wote wa zamani kuhamishiwa shule zingine naye Julius Mushi kuhamishiwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dar es Salaam.
Hao ndiyo wanafunzi wa Tambaza.
Kwa kuwa Mwanakwetu ni mwanahabari nimekuwa nikijiuliza sana juu ya jina la yule mpiga picha aliyefikwa na kadhia hii, hisia zangu hasa kwa kukumbuka wajihi wa huyu mwanahabari na kama zinarudi kwa mpiga picha mmoja wa Daily News siku nyingi siku nikikutana naye nitamuuliza maana kiwa pia mwenyeji wa Mkoa wa Mara.
Kwa kuwa Waisilamu wapo katika mfungo, naomba msomaji wangu na nikuzawadie ubeti huu.
Mola ondoa Magonjwa, Hasa ule wa Ukimwi, Watoto Kuambukizwa, Kosa lao Hawajuwi, Mayatima Wamekuwa, Na tena Hawaulizwi, Ramadhani Imefika, Mola Tusamehe Dhambi.
Kumbuka hii ni sehemu ya XXII ya Mgogoro wa Azania na Tambaza
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
.gif)


.gif)








Post a Comment