Adeladius Makwega-DODOMA
Katika matini iliyotangulia niliendelea kubainisha maswali na maoni kadhaa ya wadau mbalimbali juu ya mgogoro huo, huku nikipata maoni na maswali mengi ambayo najitahidi kuyajibu kama ninakavyojaliwa kufanya hivyo.
Kwa kuwa bado naendelea kuyapokea pale ninapojaliwa najitahidi kuyaweka wazi nawe msomaji wangu unufaike.
Hadi leo hii natambua kuwa ndugu zangu Waisilamu bado wapo katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa heshima ya hilo leo hii naweka ubeti wa tatu juu ya mfungo huo.
Hili ni kumi la Kwanza, Litapita Kwa Upesi, Sote tunabebembeleza, Rehema zake Mkwasi, Dua tumeziongeza, Tunamuomba Halisi, Ramadhani Imefika, Mola tusamehe Dhambi.
Msomaji wa matini hii ukiweka kando ubeti huo tambua kuwa Tanzania yetu imekuwa nafasi chache ambazo zinatambuliwa na katiba hata kuweka vizingiti kadhaa kumlinda mhusika huyo kama yule aliyemteua anataka kumuondoa katika mamlaka hayo.
Mara nyingi nafsi nyingi huwa zinatajwa na katiba tu lakini kumuondoa mhusika huyo huwa katika majaliwa ya mteuzi. Miongoni mwa nafasi chache zinazowekewa vizingiti ni ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Nafasi hiyo inatajwa kupitia Ibara ya 143 na 144 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama inavyofanyiwa marekebisho yake ya mara kwa mara.
Mathalani ibara nambari 143.-(1) inasema, Kutakuwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Jamhuri ya Muungano. (2) Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu atakuwa na majukumu matatu.
Mosi kuhakikisha kwamba fedha zozote zinazokusudiwa kutolewa kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali matumizi yake yameidhinishwa na kwamba zitatolewa kwa mujibu wa masharti ya ibara ya 136 ya Katiba hii, na iwapo atatosheka kwamba masharti hayo yatatekelezwa ipasavyo, basi ataidhinisha fedha hizo zitolewe;
Pili, kuhakikisha kwamba fedha zote ambazo matumizi yake yameidhinishwa yatokane na fedha zilizomo katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali au fedha ambazo matumizi yake yameidhinishwa na sheria iliyotungwa na Bunge, na ambazo zimetumika, zimetumiwe kwa ajili ya shughuli zilizo husika na matumizi ya fedha hizo na kwamba matumizi hayo yamefanywa kwa kufuata idhini iliyotolewa kuhusu matumizi hayo.
Tatu, angalau mara moja kila mwaka kufanya ukaguzi na kutoa taarifa juu ya ukaguzi wa hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano, hesabu zinazosimamiwa na watumishi wote wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na hesabu za Mahakama zote za Jamhuri ya Muungano na hesabu zinazosimamiwa na Katibu wa Bunge.
Haya ni majukumu makubwa sana kwa taifa lolote lile ili yaweze kufanywa yanahitaji mtu mwenye uwezo, ujuzi na anayeweza kujitegemea kimaamuzi.
Natambua mwanakwetu unaweza kujiuliza leo nina nini?
Kumbukumbu za Tanzania yetu zinaonesha kuwa tangu uhuru wa Tanganyika 1961 hadi leo 2022 ndugu kadhaa wamewahi kushika nafasi hiyo ya CAG, nao ni RWA MC Coll 1961-1963, Gordon .A. Hutchison 1964-1969, Mohamed Aboud 1969-1996, Thomas Kiama 1996-2005, Ludovick Utouh 2006-2014, Profesa Musa Asaad 2014-2019 na Charles Kichere 2019 hadi sasa.
Wakati Marehemu Rais John Magufuli anamuapishe Charles Kichere Ikulu Dar es Salaam alisema maneno ambayo nadhani kwa wakati ule hayakutiliwa maanani sana kwani yalimezwa na namna alivyoondoka Profesa Musa Asaad.
“Ninajua una qualification nzuri tu, na huwa hatufanyi makosa tunapoteua, form 4 ulitoka na divisheni 1 na form 6 ulitoka na divisheni 1, ili kuonesha wewe ni kipanga na siyo kilaza (Kicheko Kinasikika Ukumbini) ukaenda ukachukua sheria, degree ya sheria unayo lakini pia ukachukua degree ya akaunti na ukatoka na Upper Second with honours na hukuwahi kupata suplimentary, ukachukua Masters na umefanya kazi pahala pengi kwa hiyo tuna kuamini.”
Haya yalikuwa maneno ya Rais Magufuli kwa CAG mpya Charles Kichere baada ya kula kiapo Ikulu mwaka 2019.
Huyu ndugu yetu alisoma Tambaza Sekondari darasa la K, darasa hilo lilikuwa na wanafunzi kadhaa akiwa Christopher Mwakyusa (Kito), Dkt Elizer Ndalama ambaye nimemtaja katika simulizi zilizotangulia kuwa ni bingwa wa mifupa pale MOI lakini hivi karibuni nimeambiwa kahamia Marekani na wengine wengi.
Charles Kichere alipofika kidato cha tatu akaingia mchepuo wa masomo biashara wakati Christopher Mwakyusa ambaye sasa ni mtaalamu wa masuala ya fedha na Dkt Ndalama wao wakaenda kusoma masomo ya sayansi.
Japokuwa Kichere alikuwa akisoma masomo ya biashara baadhi ya masomo alikuwa akisoma na wenzake hawa alioanza nao kidato cha kwanza. Kichere alifika kidato cha nne na kufanya mtihani huo huku akingoja matokeo yake yeye na wenzake wengine.
Matokeo ya kidato cha nne yalitangazwa.
Cha kusikitisha,mwaka huo waliohitimu kidato cha nne wanafunzi wa Tambaza japokuwa walifanya vizuri katika masomo mengi lakini somo la ENGLISH LANGUAGE hawakufanya vizuri kabisa. Kulikuwa na A moja tu ya somo hilo.
A hiyo haikutoka kwa wale mabingwa wa Lugha hiyo bali alipata ndugu Charles Kichere peke yake.
“Walimu wa Tambaza na wanafunzi wa shule hiyo huku wakisikitika kwa matokeo hayo ya lugha hiyo liyoingia Tanganyika kwa meli, walimsaka kutaka kumjua, je nani alipata A hiyo ya ENGLISH LANGUAGE?”
Wanasema baadaye walitambua kuwa aliyefanya vizuri kwa somo hilo alikuwa ni Charles Kichere. Huku yeye alipita majumbani kwa rafiki zake kuwatambishia kwa kufanya vizuri kwake katika somo la Kiingereza.
Charles Kichere kijana aliamua kupita kwa jamaa zake wote nyumba kwa nyumba huku wengine wao wakipata alama mbaya za somo hilo.
Wakati huo alikuwa akiishi Kinondoni Hananasif ukimaliza tu zile nyumba za serikali mashirika pale unapoanza nyumba binafsi.
Kwa ukiachana na ujuzi wake wa masomo ya biashara CAG Charles Kichere alikuwa bingwa wa somo la Kiingereza Tambaza Sekondari.
Je kipi kitaendelea?
Subiri matini ijayo.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
.gif)






.gif)
Post a Comment