Adeladius Makwega – TANGA
Katika matini iliyotangulia, msomaji wangu utakumbuka tulikabidhiwa barua za kuwajulisha wazazi/walezi kushiriki kikao cha Jumatano, Aprili 27, 1994, katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, huku Afisa Elimu wa Jiji hilo, Mwalimu Abdul Mbegu, akitueleza masharti kadhaa wakati wa kushiriki kikao hicho.
Binafsi nilijiandaa na kuzisaka sare zangu za shule, ambazo zilikuwa kaptura ya polyester grey na shati jeupe la mikono mifupi. Nilipokuwa najaribu kuzivaa sare hizo, zilikuwa tayari zimenibana mno, maana zilikuwa zimekaa miezi saba bila kuvaliwa. Haikuwa na namna; nilizifua vizuri na kuzipiga pasi ili ziwe tayari kwa kikao.
Huku nikimjulisha mzazi wangu juu ya kushiriki kikao hicho, nilipomkabidhi mzee wangu, Francis Fidelis Makwega, wito huo, alinijibu “ndiyo.” Siku hiyo ilipofika, tulitoka zetu Mbagala hadi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, tukapokelewa na makarani wachangamfu wa ofisi hiyo na kuoneshwa benchi la kukaa sisi pamoja na wazazi wetu.
Tukiwa katika benchi hilo, nilikutana na wenzangu kadhaa, akiwamo Arone Sifuni, Rubua Mustafa, Lukas Mganga, na binti mmoja wa Kisutu, lakini sikuweza kumuona Mohammed Said (Mzukizi), ambaye tulikuwa naye katika shauri moja.
Tukiwa katika benchi hilo, alipita mama mmoja, mtu mzima sana, akiongozana na mzee mmoja wa kimo cha kawaida, aliyekuwa amevalia kanzu nyeupe na makubadhi, akitembea taratibu kana kwamba hataki. Mzee huyu alipokuwa akija upande wetu, alikutana na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, waliokuwa wakimtania na kucheka sana kutokana na ucheshi wake.
Mzee huyo alifika pale tulipokaa sisi na wazazi wetu, akatusalimia sote kwa kutupa mikono.
Akasema,
“Aha, hawa ni vijana wangu mmekuja, ehe! Poleni sana. Wazazi tambueni kuwa mtoto akiunyea mkono, haukatwi bali huoshwa tu. Sisi ni wazazi. Sasa ndiyo tunakwenda kwenye kikao.”
Katika lile benchi, mwenzetu Lukas Mganga alikuwa mkubwa kwetu na alitakiwa kumaliza kidato cha nne mwaka 1993, kama nilivyoeleza katika makala zilizotangulia, ndipo akapata matatizo.
Ndugu Mganga akatuuliza,
“Mnamfahamu huyu mzee?”
Tukajibu,
“Hapana.”
Akasema,
“Huyu ni Ibrahimu Raha (Mzee Jongo) wa Michezo Redio.”
Tukjajibu Kweli, tumeisikia sauti yake. Hata alipokuwa akipita, alikuwa akitaniwa na watumishi wa Ofisi ya Mkoa wa Dar es Salaam kwa sababu ya vichekesho vyake — hayo tuliyasema.
“Yeye ni miongoni mwa wajumbe wa Bodi ya Rufaa ya Elimu ya Mkoa wa Dar es Salaam. Pia ni Mwenyekiti wa Wazazi wa Mkoa wa Dar es Salaam (Jumuiya ya Wazazi ya CCM).”
Alisema Lukas Mganga.
Tukiwa katika benchi, jina lako linaitwa, kisha unaingia ukumbini wewe na mzazi wako.
Tukasikia,
“Lukas Mganga!”
Kesi ya Lukas ilikuwa kubwa. Ilidaiwa walikutwa na majani makavu mifukoni, yanayodaiwa kuwa ni madawa ya kulevya, wakiwa shuleni na wakiwa wamevaa sare za shule. Majani hayo makavu yalipelekwa kwa mkemia kwa uchunguzi.
Lukas alipoingia kwenye bodi, hakukaa muda mrefu. Alitoka huku machozi yakimtoka. Tulipomuuliza, alijibu kuwa maamuzi ya Bodi ya Shule yamebaki kama yalivyo, na kwamba amefukuzwa shule.
Rubua Mustafa akaitwa., Rubua Mustafa na mwenzake mwingine walikutwa na vitabua ambavyo viliibiwa baada ya stoo ya vitabua kuvunja siku Tambaza ilipofungwa miezi mitatu, siku ilipofunguliwa shule ambapo wanafunzi wote walijaza fomu ya kula kiapo cha kutofanya vurugu tena stoo ya vitabu vya kidato cha tano na sita ilivunjwa na wanafunzi wengi wakakimbilia stoo hiyo na kubeba vitabu na kutokomea navyo, mzigo huo alibebeshwa Rubua Mustafa na mwenzake.
Akaingia yeye na mwenzake; mara wakatoka. Tulipowauliza, walijibu kuwa wameshinda rufaa yao na wameambiwa baada ya juma moja waende kuchukua barua za kurudishwa shuleni huyu Rubua Mustafa alifukuzwa akiwa kidato cha pili.
Aliitwa binti wa Kisutu. Binti huyu, ambaye jina lake nimelisahau, alikuwa amevalia sketi ya rangi ya damu ya mzee, fulana nyeupe na kandambili. Akaingia ndani akiongozana na baba yake binti huyu alisema yeye anatokea Temeke Mikoroshini.
Baada ya muda, binti alitoka na hawakurudi tena pale tulipokuwa tumekaa. Walishuka ngazi jirani na ofisi hiyo na kuondoka zao.
Kisha wakaita, “Arone Sifuni, Adeladius Makwega na Mohamed Said!”
Tukaingia ukumbini mimi, Sifuni na wazazi wetu,Arone Sifuni alikuja baba yake ambaye alikuwa mtumishi wa Wizara ya Elimu lakini Mohammed Said yeye hakuwapo, wala mzazi wake.
Tulipoingia ukumbini, mbele kwenye meza walikaa Ditopile Ukiwaona Ramadhani wa Mzuzuri (Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wakati huo) na Abdul Mbegu (Afisa Elimu wa Jiji la Dar es Salaam wakati huo), pamoja na wajumbe wengine ambao sikuweza kuwafahamu, isipokuwa Mzee Jongo na mama aliyekuwa anaingia naye ukumbini wakati tulipokuwa tumekaa katika benchi.
Ditopile Mzuzuri alituomba tujitambulishe sote, na tulifanya hivyo. Nao walijitambulisha majina yao, huku Mkuu wa Mkoa akijitambulisha majina yake yote manne:
“Ditopile Ukiwaona Ramadhani wa Mzuzuri.”
Akasema
“Karibuni sana ofisini kwangu. Kama wajumbe, tulivyojadili rufaa hizi tatu ambazo wazazi mlizileta mbele ya bodi zikiwa na hoja nyingi, hususan rufaa ya Adeladius Makwega. Kwani Makwega ni yupi?”
Mwanakwetu akanyoosha mkono. Ditopile atakitisa kichwa kisha akaendelea kuongea:
“Maamuzi ni kwamba mwanafunzi Mohamed Said, mwanafunzi Arone Sifuni na mwanafunzi Adeladius Makwega, wote warudishwe shuleni mara moja, waendelee na masomo. Bodi ya Rufaa inaamini upande wa wazazi hauna hoja nyingine na haya maamuzi ndiyo maombo yenu labda upande wa Mkuu wa Shule — kama unapinga maamuzi yetu — unaweza kukata rufaa kwa Waziri wa Elimu ndani ya siku 45 kuanzia utakapoyapokea maamuzi haya kwa barua. Je, unazo hoja?”
Aliuliza Mkuu wa Mkoa, Ditopile Mzuzuri.
Macho yetu sote, sisi na wazazi wetu, yalimtazama Mwalimu Wajimila, aliyemwakilisha Mkuu wa Shule, Mwalimu Mtera huku mbele yake kulikuwa na mafaili kadhaa, ambayo yalikuwa yetu.
Juu ya faili moja kuliandikwa “amefukuzwa shule”
kwa wino wa bluu. Binafsi sikufahamu faili hilo lilikuwa la nani.
Mwalimu Wajimila akasema:
“Kwa niaba ya Mkuu wa Shule na kwa niaba ya Bodi ya Shule ya Sekondari Tambaza, maamuzi hayo tunayakubali dhidi ya wanafunzi hawa watatu: Arone Sifuni, Adeladius Makwega na Mohamed Said. Lakini wakirudi pale, itaonekana kuwa wanafunzi wanafanya fujo kisha wanakata rufaa, wanashinda, na wanarudishwa shuleni. Sasa Tunaomba wahamishiwe shule nyingine za umma.”
Mwenyekiti wa Bodi, mheshimiwa Ditopile Mzuzuri, akajibu:
“Sawa, tumesikia lakini nataka jambo hili lifanyiwe maamuzi na wajumbe wangu. Hayo ni maombi yako.Wazazi, nyie wanafunzi na mkuu wa shule tokeni nje tufanye maamuzi juu ya maombi haya mapya.”
Tukatoka nje ya ukumbi. Mwalimu Wajimila alikuwa amekumbatia mafaili yake kifuani, akiwa ameinama, amekaa pembeni peke yake. Sisi tulikuwa na wazazi wetu tukisubiri kitakachojiri baada ya mjadala wao, huku wazazi wetu wakiongea.
Baba yangu akaaulizwa na Mzazi wa Arone Sifuni kwani wewe unafanya kazi wapi? Baba yangu akajibu,
“Mimi ni mwalimu wa Shule ya msingi Bunge.”
Baada ya muda mfupi, karani wa Ditopile Mzuzuri, mama mchangamfu sana, akatuita tena ukumbini.
Tukaingia.
Mwenyekiti wa Bodi ya Rufaa ya Mkoa wa Dar es Salaam, Ndugu Mzuzuri, akasema:
“Mkuu wa Shule, tunafanya maamuzi haya kwa manufaa ya shule zetu na watoto wetu wa Dar es Salaam. Tulipompokonya Aga Khan shule ya H. H Agakhan Tambaza, shabaha ilikuwa watoto wetu wasome — siyo kufanya vurugu, wala siyo kuwafukuzwa hovyo hovyo bila sababu za msingi, mimi mwenyewe nimesoma Tambaza. Hata hivyo, maombi yako yamepokelewa, na Katibu wa kikao hiki, Mwalimu Mbegu, atayafanyia kazi.
Wazazi, poleni sana. Shauri hili limeisha. Baada ya juma moja, nendeni Ofisi ya Jiji la Dar es Salaam mkachukue barua za kurudishwa shuleni. Wanangu mkasome, mnanielewe? Nyie wanafunzi? Nendeni mkasome!”
Sisi tukajibu:
“Ndiyo.”
Tulijibu hivyo huku tumejikunyata mithili ya paka aliyeloweshwa maji.
Mzee Jongo alikuwa akicheka tu tangu hoja za Wajimila na jinsi Mkuu wa Mkoa, Ditopile Mzuzuri, alivyokuwa akiongoza kikao hicho.
Tukatoka katika kikao hicho Arone Sifuni akaagana na Baba yake na mimi kuagana na Baba yangu akanipa nauli na mimi kuambatana na Arone Sifuni tukapita Ilala Kota hadi Mtaa Pemba nyumba namba moja pale tukanywa chai na tukamsimulia kilichotokea mama wa Arone , huku mama huyu akawa anacheka.
Kisha Mwanakwetu kurdui zake Mbagala.
Kwa wale wanaokumbuka awali nakala ya rufaa ilipokuwa inakwenda bodi baada ya Peter Pinda na Phideli Mwidunda kuikamilisha baba yangu hakuisaini hadi niliporudi kwa Peter Pinda alipokwenda kuondoa zile nyaraka za mwisho zenye jina la mzazi na kuweka jina la mlezi kumbuka nyaraka tano kw ahiyo karatasi tano ziliondolewa na kuweka jina la mlezi ambapo alisaini wakili Phidelis Mwidunda kama mlezi.
Swali ambalo unaweza kujiuluza ilikuwaje Baba wa Mwanakwetu hakusaini nyaraka hizo kwa mara ya kwanza? Jibu lake ni moja tu ilikuwa ni hofu ya namna nyaraka zile ziliandikwa kisheria.Jmabo hili Mwidunda na Pinda walilibaini na kulitatua haraka ndani ya siku zile 45 za kupeleka rufaa kwa Afisa Elimu jiji. Ifahamike wazi Baba wa Mwanakwetu alikuwa tu mwalimu wa shule ya msingi , hawa akina Abdul Mbega, Ditopile Mzuzuri walikuwa ni watu wkaubwa kwake na ndiyo maana hata Ditopile Mzuzuri aliuliza Adeladius Makwega ni yupi?
Je, nini kitaendelea? Subiri matini ijayo.
Kumbuka, huu ni Mgogoro wa Azania na Tambaza XLI.
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
.gif)
%20Instagram.png)







.gif)
Post a Comment