MGOGORO WA AZANIA NA TAMBAZA XIX

 



Adeladius Makwega – Arusha

Msomaji wangu, naomba kwa leo nipitie kikapu changu cha maswali na maoni kwani kinakaribia kujaa, kikiwa na maswali na maoni lukuki.

Wa kwanza kulipiga kasia la maswali hayo ni ndugu Jumanne Mwasamba. Yeye ameniuma sikio kuwa anatokea huko Mpanda, mkoani Katavi.

Ndugu yangu Jumanne, kwanza alinitakia heri ya mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Namshukuru sana kwa kunitakia heri ya mwezi huo mtukufu wakati makala haya yanatayarishwa kwa mara ya kwanza.

 

Kwa kuwa natambua kuwa wasomaji wangu walikuwa katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani wakati makala haya yanatoka kwa mara ya kwanza, nilitoa zawadi ya mfungo huo kwa ubeti huu wa shairi:

Alhamdulillah nashukuru, namshukuru Qudusi,
Kutwa tunamdhukuru kwa wingi bila kiasi,
Apate kutunusuru na adui Ibilisi,
Ramadhani imefika, Mola tusamehe dhambi.

Ndugu Mwasamba anauliza: Je, Tambaza ilikuwa shule ya wavulana pekee?

Katika kujibu swali lake, napenda kusema kuwa ni kweli shule hii ilikuwa ya wavulana pekee. Hata wakati huo tuliposoma sisi, mazingira ya shule hii yalilenga kutoa elimu kwa wavulana tu.

Kuna mambo mawili yanayothibitisha hilo. Kwanza ni jina la awali la shule, H.H. Aga Khan Boys, ambalo linaonekana katika jiwe la msingi lililopo mbele ya shule, upande unaotazamana na Shule ya Kimataifa ya Tanganyika.

Pili ni muundo wa vyoo vya shule hii, vilivyopo mwisho wa korido ya kwanza na ya pili. Wakati huo vilihudumia wavulana pekee. Vyoo vya wasichana vilitengenezwa baadaye; hapo awali walikuwa wakitumia vyoo vya walimu na watumishi wanawake.

 

Hata hivyo, baadaye wasichana walianza kujiunga na shule hii katika ngazi ya A-Level. Dada zetu hawa tulikuwa tunawapenda sana, na walisoma kwa raha huku wakipendeza kwa sare zao za shati jeupe la mikono mifupi na sketi ya kijivu na kifuani nendo ya samawati..

Nakumbuka sikuwahi kushuhudia tukio lolote baya dhidi yao. Mwaka 1991 alikuwepo dada mmoja aliyependeza sana kwa sare yake. Wanafunzi wa Tambaza tulimpa jina la utani kutokana na mvuto wake, lakini kwa sasa nitalihifadhi jina hilo hadi nitakapopata ruhusa yake.

Kasia langu la pili la maswali na maoni linamuangukia ndugu Joshua Grei, aliyemaliza Azania Sekondari mwaka 1989. Kwanza, anatoa pongezi kwa matini hizi.

Anasema kuwa vurugu kubwa ya kwanza anayoikumbuka, kabla ya zile zilizosababisha Tambaza kufungwa na baadhi ya wanafunzi kuhamishwa, ilitokea mwaka 1989 alipokuwa kidato cha nne Azania.

Ugomvi huo ulizuka kati ya Azania na Tambaza baada ya mvutano wa takribani wiki mbili, uliosindikizwa na kaulimbiu ‘TUJE TUJE’ kila wanafunzi wa Tambaza walipopita karibu na Azania wakitokea upande wa Fire kuelekea kupanda magari ya kurudi nyumbani.

 

Kauli hiyo iliwachochea sana wanafunzi wa Azania, hasa wale wa kidato cha tano waliotoka Kanda ya Ziwa, wakihisi kuonewa na Tambaza. Hata mlezi wa wanafunzi wa Azania wakati huo, marehemu Mzee Major, aliwahi kusema:

“Nyie si wanaume kama wenzenu wa Tambaza; safari hii mkipigwa, nitawashonea sketi na kuwaita AZAJANGWA.”

Kauli hii iliongeza ujasiri kwa wanafunzi wa Azania.

Kulikuwa na mashindano ya shule za sekondari yaliyofanyika katika viwanja vya Don Bosco, vinavyomilikiwa na Kanisa Katoliki. Azania na Tambaza zilifika fainali.

Katika fainali hiyo, iliyofanyika katika uwanja wa Azania, kulikuwa na wachezaji maarufu kama Rodric John wa Tambaza na Robert Mwampebwa wa Azania, ambaye kwa sasa ni mwandishi wa habari nchini Kenya. Pia alikuwepo marehemu Hamisi Said, aliyewahi kuchezea timu ya taifa.

Chanzo cha vurugu kilianza Azania walipopata bao la kwanza kupitia Hamisi Said. Hali hiyo ilipandisha mori kwa wanafunzi wa Azania na kuwakasirisha wanafunzi wa Tambaza, ambao walikuwa wameapa kushinda na hata kuvamia jiko la Azania iwapo wangeshinda.

Hali ilizidi kuwa tete uwanjani, huku wanafunzi wa Tambaza wakitoa vitisho kwa refa. Wakati huo Azania ilikuwa inaongoza kwa bao moja.

Dakika zilipokuwa zinayoyoma, refa alitoa penalti tata kwa Tambaza, na Rodric John akasawazisha. Matokeo yakawa 1–1.

 

Baada ya hapo, vurugu zililipuka. Wanafunzi wa Tambaza walishangilia kwa fujo wakirusha mawe na vitu vingine, na Azania wakajibu mapigo kwa fimbo za mianzi.

Hatimaye, wanafunzi wa Tambaza walitawanyika katika makundi mawili—moja kuelekea fensi ya Muhimbili na lingine upande wa Jangwani. Vurugu ziliendelea hadi maeneo ya Fire, Kariakoo na Shule ya Uhuru.

Jeshi la Polisi lililazimika kuingilia kati; baadhi ya wanafunzi walikamatwa na kupelekwa kituo cha Msimbazi, huku wengine wakipatiwa matibabu katika Hospitali ya Muhimbili.

Kwa leo, msomaji wangu, naomba niishie hapa. Naiweka kalamu yangu chini na nakutakia siku njema.

Kumbuka, hii ni sehemu ya kumi na tisa ya Mgogoro wa Azania na Tambaza.

Nakutakia siku njema.
Barua pepe: makwadeladius@gmail.com
Simu: 0717 649 257

 

 

 

0/Post a Comment/Comments