
Adeladius Makwega – Makundusi, Serengeti
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, Juni 2, 2026, amefanya kikao na wananchi wa kata kadhaa za Wilaya ya Serengeti zilizo jirani na Mbuga ya Serengeti. Amesema kuwa mamlaka zinazosimamia wanyama zitumie mbinu zote stahiki kuhakikisha wanyama waharibifu hawaleti madhara kwa mazao na jamii zinazoishi kandokando ya mbuga hiyo, huku wananchi wakitakiwa kutoa ushirikiano kwa taasisi zote zinazofanya kazi nao.
“Changamoto ya wanyama lazima itatuliwe kwa wakati. Ndiyo maana nimekuja hapa na wataalamu wangu. Suala la kutenganisha eneo la malisho na mbuga lazima likamilike ili kila mmoja aheshimu mipaka ya mwenzake,” alisema Kanali Mtambi.
Kanali Mtambi aliyasema hayo alipokuwa akijibu swali la Bi. Sofia Prosper kutoka Kijiji cha Makundusi, ambaye alitaka kujua ni lini tatizo la wanyama kuharibu mazao yao litapatiwa ufumbuzi. Alieleza kuwa amekuwa mkazi wa kijiji hicho tangu mwaka 1984 na changamoto hiyo imeendelea kwa muda mrefu.
Katika hali ya pekee, wananchi wa Kijiji cha Makundusi kwa kauli moja waliuliza maswali mbalimbali na kutoa ushauri. Miongoni mwao alikuwa Sabato Sabato, ambaye alipendekeza kuwekwa kwa uzio maalumu ili kuzuia wanyama kubaki katika maeneo yao na wananchi kubaki katika maeneo yao.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Angelina Marko Lubela, alisema anamkaribisha mkuu huyo wa mkoa katika wilaya hiyo na kueleza kuwa kikao hicho ni fursa kwa wananchi kuzungumza naye moja kwa moja.
Bi. Angelina Lubela aliongeza:
“Wilaya ya Serengeti ni salama, huku wananchi wakiendelea na majukumu yao ya kila siku. Changamoto mbalimbali zinaendelea kupatiwa ufumbuzi.”
Awali, akifungua kikao hicho cha Mkuu wa Mkoa na wananchi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Makundusi, Mseti Joseph, alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Mara kwa kufika kijijini hapo na kubainisha kuwa hiyo ni ziara yake ya pili katika kijiji hicho.
Katika kikao hicho, kata zilizoshiriki ni Natta, Kyaimbai na Ikoma. Kijiji cha Makundusi pekee kina wakazi 8,000 na kipo katika Kata ya Natta.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Serengeti pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mara. Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gerald Musabila Kusaya, alikuwa sehemu ya ziara hiyo iliyoanza mapema siku hiyo.
Wakati hayo yakiendelea katika Kijiji cha Makundusi, hali ya hewa ya Wilaya ya Serengeti kwa Juni 2, 2026, ilikuwa nyuzi joto 28 , unyevunyevu wa asilimia 40, uwezekano wa mvua asilimia 37, na upepo ukivuma kwa kasi ya kilomita 13 kwa saa.
makwadeladius@gmail.com
0717 649 257











Post a Comment