Maafisa Ustawi Mkoa wa wa Mara Wasukuma Ushirikiano wa Karibu na Wamiliki wa Makao ya Watoto

 

 





Adeladius Makwega, Mara

Katika juhudi za kuimarisha ustawi wa watoto wanaoishi katika makao mbalimbali, wito mzito umetolewa kwa wamiliki wa makao ya watoto mkoani Mara kushirikiana kwa karibu na maafisa ustawi wa jamii.

 

Wito huo umetolewa na Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mara, Bi. Elizabeth Mahinya, ambaye amesisitiza kuwa mafanikio ya huduma kwa watoto yanategemea mshikamano na mawasiliano ya wazi kati ya pande zote husika.

 

Akizungumza Juni 30, 2026, katika kikao kazi kilichowakutanisha maafisa ustawi wa jamii pamoja na wamiliki wa makao ya watoto, Bi. Mahinya alieleza kwa msisitizo kuwa hakuna changamoto isiyopatiwa ufumbuzi pale ushirikiano unapopewa kipaumbele.

 

“Ni wakati wa kujenga daraja la ushirikiano thabiti. Pale ambapo kulikuwa na mwanya, basi tuuzibe mara moja. Kila mmoja awe tayari kusikiliza na kushirikiana na mwenzake. Tukiweka wazi changamoto zetu, tutapata suluhisho la pamoja na kuimarisha huduma kwa jamii,” alisisitiza.

 

Kauli hiyo imepokelewa kwa mwitikio chanya kutoka kwa wadau. Bi. Rhobi Samwel, mmiliki wa makao ya Hope for Girls and Women Tanzania, alieleza kuwa wako tayari kugeuza maneno hayo kuwa vitendo kwa kuhakikisha ushirikiano unakuwa sehemu ya utendaji wao wa kila siku.

 

Naye Bi. Sofia Kiwanga, Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mara, alifafanua kuwa hatua kubwa tayari imepigwa, huku utekelezaji wa malengo ukifikia asilimia 76. Aliongeza kuwa kilichobaki ni kuongeza juhudi katika utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa ili kufikia matokeo yaliyokusudiwa.

 

Mbali na majadiliano hayo, kikao hicho pia kilishuhudia uchaguzi wa viongozi wa UMAWATA ngazi ya Mkoa wa Mara—Umoja wa Wamiliki wa Makao ya Watoto Tanzania. Viongozi waliochaguliwa wataongoza juhudi za kuimarisha sekta hiyo katika ngazi ya mkoa, wakiongozwa na Mwenyekiti Ibrahim Mussa, Katibu Chuni Manyama, Mweka Hazina Said Tinde pamoja na Makamu Mweka Hazina Godfrey Mchome.

Kikao hicho kilileta pamoja wadau mbalimbali kutoka taasisi za kidini na mashirika binafsi, kikidhihirisha dhamira ya pamoja ya kuhakikisha watoto wanapata malezi bora, salama na yenye matumaini ya kesho iliyo njema.

 

Kwa pamoja, wadau hao wameonesha kuwa pale panapokuwepo ushirikiano wa dhati, mustakabali wa watoto unakuwa na mwanga zaidi.

makwadeladius@gmail.com

0717649257











 

 

0/Post a Comment/Comments