Maafisa TEHAMA Mkoa wa Mara Wateta

 


Adeladius Makwega–Mukendo, Musoma, Mara

Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, ndugu Ngobai Mwisarya, Juni 9, 2026, amewataka maafisa TEHAMA wa Mkoa wa Mara kufanya kazi kwa ushirikiano na kujituma ili kufanikisha shughuli zote za Serikali kwa ufanisi na weledi.

“Kwa sasa kila kitu kipo ndani ya TEHAMA. Wewe kama Afisa TEHAMA unawajibikaje? Lazima ujipime na kujitathmini vizuri katika utendaji wako wa kazi zote unazozifanya, iwe Jumatatu, Jumanne, Jumatano, Alhamisi au Ijumaa. Ukizembea, basi taasisi yetu ya umma itazembea. Nawaombeni tufanye kazi kwa bidii huku tukithamini muda.”

 

Haya yamesemwa na ndugu Mwisarya wakati akifungua kikao cha maafisa TEHAMA kutoka halmashauri zote za Mkoa wa Mara, ikiwamo Manispaa ya Musoma, Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Halmashauri ya Mji wa Tarime, Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Halmashauri ya Mji wa Bunda, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, na Halmashauri ya Wilaya ya Butiama.

Awali, akisoma ajenda za kikao hicho, Katibu wa kikao, Switbert Masumira, ambaye pia ni Afisa TEHAMA, alisema kuwa kikao hicho kilikuwa na ajenda nane. Mojawapo ya ajenda hizo ilikuwa ni kutoa maelekezo waliyoyapokea kutoka kikao cha Maafisa TEHAMA wa Mikoa yote nchini kilichofanyika jijini Dodoma kuanzia Mei 25 hadi 30, 2026.

Baada ya kikao hicho, maafisa TEHAMA walipata fursa ya kujionea namna mfumo wa TEHAMA unavyofanya kazi kwa kasi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, kufuatia maboresho makubwa yaliyofanyika.

Wakati hayo yakifanyika, hali ya hewa ya mji wa Musoma ilikuwa nyuzi joto 28, unyevunyevu wa asilimia 10, uwezekano wa mvua asilimia 53, na upepo ukivuma kwa kilomita 16 kwa saa.

Wasiliana na mwandishi:

Barua pepe: makwadeladius@gmail.com

Simu: 0717649257





 


 

 

0/Post a Comment/Comments