KITI ANAKONDA

Eh eh… sikiliza sasa…
Pwani yasema… ukweli huu…

Ahh Mwanangu Gershoni
Mtangazaji wa  zamani wa SHIUTA, unayemnenepesha shetani,
Kiti anakonda, kiti anakonda,
Unawalisha pepo, watu wako wanateseka,
Kiti anakonda, kweli anakonda.

Ahh Mwanangu Gershoni

Mtangazaji wa zamani wa SHIUTA, amka uone sasa,
Haki iko wapi, watu wanalia,
Usimnenepeshe shetani kwa mali ya wengine,
Kiti anakonda, kiti anakonda.

Pwani ya Afrika Mashariki, mila zimeenea,
Matambiko gizani, sauti zasikika,
Pango na miti mikubwa, au vyumba vilivyofichwa,
Kuna kiti cha ajabu, kimepambwa kwa siri.
Sauti zatoka pale, zikitoa maagizo,
“Kuku mwekundu lete, mbuzi mweusi pia,”
Watu wanaamini, wakifuata bila shaka,
Lakini hawajui, wanapotea njia.

Ahh Mwanagu Gershoni

Mtangazaji wa  zamani wa SHIUTA, unayemnenepesha shetani,
Kiti anakonda, kiti anakonda,
Unawalisha pepo, watu wako wanateseka,
Kiti anakonda, kweli anakonda.

Waswahili wakasema, kwa hekima ya zamani,
“Unamnenepesha shetani, kiti anakonda,”
Maana mali inaenda, kwa njia zisizo haki,
Na nyumbani kwako, njaa inaongezeka.
Watoto wanalia, familia zinateseka,
Wengine wanatafuta, msaada wa gizani,
Badala ya mwanga, wanazidi kupotea,
Hii siyo njia njema, rudini kwenye kweli.

Ahh Mwanangu Gershoni
Mtangazaji wa Zamani wa SHIUTA, unayemnenepesha shetani,
Kiti anakonda, kiti anakonda,
Unawalisha pepo, watu wako wanateseka,
Kiti anakonda, kweli anakonda.

Amka ewe ndugu, angalia maisha yako,
Usitoe sadaka, kwa giza lisilo na faida,
Heshima huanza nyumbani, kwa walio karibu,
Sio kwa sauti za siri, zisizo na mwanga.
Tafuta njia ya haki, iliyo wazi mchana,
Usikimbilie gizani, kwa ahadi za uongo,
Maana mwisho wake, ni majuto na maumivu,
Rudi kwenye nuru, ndipo utapata amani.

Kiti anakonda… (eeh eeh)
Kiti anakonda… (eeh eeh)
Usimnenepeshe shetani…
Rudi kwenye mwanga…

 

Jioni ya Juni 28, 2026, MwAnAkWeTu aliusikiliza wimbo Kiti Anakonda, uliotungwa kutoka Mbagala, ambao unamzungumzia mhusika mwenye jina la Gershoni na hekaheka zake.

Dhana iliyotumika ni safari za mhusika huyu kwenda kwa Shetani na kutoa sadaka kadhaa za wanyama kama vile kuku, mbuzi, na wanyama wengine wa rangi mbalimbali. Kwa bahati nzuri, mtunzi hakutaja kama huko binadamu wanatolewa kafara.

 

Dhana hii imejengwa katika mandhari ya kwa mganga, ambapo kuna kiti kilichopambwa vizuri. Kisha, kuna sauti inayotoka kwa Shetani ambayo hutoa maagizo kadhaa:

 

“Leta mbuzi mweupe, leta kuku wa rangi hii na ile, leta ngamia jike, leta beberu mweusi.”

Ahh, Shetani—hongera kwa kuagiza vinono!

 

Haya ni mandhari ya ushirikina katika dhana ya maisha ya Waswahili na watu wa Afrika Mashariki.

 

Mtunzi wa wimbo huu anamwambia mwanawe, Gershoni,

 

“Mbona unamfaidisha Shetani tu, wakati kiti hakipati kitu?”

Kama kazi inafanywa na Shetani na Kiti, basi wote wafaidike na kazi hiyo ya ushirikina.

 

Mtunzi wa wimbo huu anaonekana kukionea huruma Kiti, na pia kumwonea huruma mwanawe Gershoni kwa kupoteza rasilimali na nguvu zake kumfaidisha Shetani.

 

Kwa faida ya msomaji wa MwAnAkWeTu, leo hii ameamua kuuweka wimbo huu ili wasomaji wake wausome.

 

Je, wewe msomaji wangu umejifunza nini?

 

Kumbuka:


“KITI ANAKONDA.”

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com
0717649257

 











0/Post a Comment/Comments