HOTUBA YA DKT. NCHIMBI NDOTONI

 


Adeladius Makwega – Musoma MARA TANZANIA

Nilifika nyumbani ninapoishi majira ya saa 10:27 jioni nikiwa nimechoka sana. Nikaingia chumbani kwangu ili nipate usingizi wa muda mfupi wa kunipunguzia uchovu wa siku nzima. Kitanda changu cha telemka tukaze nilikikimbilia mithili ya mtoto mchanga anayelikimbilia nyonyo la mama yake baada ya kutengana naye siku nzima. Mama ametoka kazini, amerudi nyumbani, na mtoto amebaki na njaa tele; hivyo hukimbilia kifua cha mama yake kwa shauku kubwa. Ndivyo nilivyokikimbilia kitanda changu.

Nilijitupa kitandani na kulala kwa muda mfupi. Nikiwa usingizini, ghafla niliamshwa na mlio wa simu yangu ya mkononi. Nilizungumza na ndugu mmoja, kisha nikapokea simu ya pili kutoka kwa ndugu mwingine na kuzungumza naye pia. Ndugu hao wawili walitambua mara moja kwamba Mwanakwetu alikuwa amelala, kwa sababu maneno yalikuwa hayatamkwi vizuri kutokana na usingizi.Baada ya mazungumzo hayo, nikarejea tena kitandani na kuendelea na usingizi wangu.

 


Nikiwa nimelala, katika wakati ambao siwezi kuuelezea vizuri, nikaota kwamba nimepewa jukumu la kuandaa hotuba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Emmanuel Nchimbi, kwa ajili ya kuisoma katika shughuli fulani muhimu. Aliyenipa jukumu hilo sikumfahamu. Hata hivyo, alinipa vidokezo kadhaa vyenye muktadha wa kidini na kisha kuniachia kazi hiyo, akisisitiza kuwa alikuwa anaihitaji baada ya saa mbili tu.

Ndani ya ndoto hiyo, Mwanakwetu nikajiuliza:

“Mbona siku nyingi sijandika risala wala hotuba? Kweli nitaweza?”

Nikajitia moyo na kuanza kazi mara moja. Nikaiandika hotuba hiyo kwa umakini mkubwa kuanzia mwanzo hadi mwisho. Baada ya kuikamilisha, nikaifanyia uhariri wa awali na kisha nikawasiliana na mhariri maarufu, Simon Mkina, ili aipitie kwa mara ya mwisho kabla ya kumkabidhi Makamu wa Rais. Mhariri Simon Mkina alitumia dakika chache kuikagua na kuikamilisha kazi hiyo, kisha akanirejeshea rasimu iliyoboreshwa. Nami nikaanza kuisoma kwa mara ya mwisho kabla ya kuiwasilisha.

 



Msomaji wangu, kumbuka kwamba Mwanakwetu bado yupo ndotoni na anaota haya yote. Mkononi mwake ameshika karatasi kadhaa zenye hotuba aliyoiandaa kwa ajili ya kukabidhiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Emmanuel Nchimbi, ili aisome katika shughuli moja muhimu.

Mwanakwetu akaanza kuipitia kazi hiyo kwa mara ya mwisho. Hotuba hiyo ilikuwa na maudhui yafuatayo:

 

 “Ndugu Wananchi,

Nawasalimu kwa heshima kubwa.

Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na kauli mbalimbali zilizotolewa katika mijadala ya kisiasa, zikiwemo kauli zinazohusisha majina na mifano yenye asili ya kidini. Baadhi ya kauli hizo zimeelekezwa kwangu moja kwa moja au kwa namna ambayo wananchi wengi wamezitafsiri kuwa zinanihusu.

Kama kiongozi wa umma, nimejifunza kwamba si kila kauli inahitaji kujibiwa kwa ukali, na si kila tuhuma inahitaji kujibiwa kwa hasira. Wakati mwingine, hekima kubwa zaidi ni kuzungumza kwa utulivu, kueleza ukweli kwa staha na kuacha wananchi waamue kwa kutumia busara zao.

Ndugu Wananchi,

Nimesikia nikihusishwa na jina la “Yuda” na madai ya usaliti. Kwa kuwa jina hilo lina asili ya kidini na lina maana nzito katika historia ya imani za watu wengi, ni muhimu kulitafakari kwa kina kabla ya kulitumia katika mjadala wa kisiasa.

Katika Agano Jipya kuna watu zaidi ya mmoja walioitwa Yuda. Wapo Yuda Iskariote, Yuda mwana wa Yakobo (Luka 6:16), na Yuda anayetajwa katika Yohane 14:22. Hata hivyo, Yuda Iskariote ndiye aliyebaki katika historia ya Ukristo kama alama ya usaliti.

Kwa mujibu wa simulizi za Injili, Yuda Iskariote alikubali kuwasaidia viongozi wa dini kumkamata Yesu Kristo kwa malipo ya vipande thelathini vya fedha (Mathayo 26:14–16). Alimtambulisha Yesu kwa busu wakati wa kukamatwa kwake (Mathayo 26:47–50). Aidha, katika baadhi ya maandiko ya Kikristo, anahusishwa na kupenda fedha kupita kiasi na kutokuwa mwaminifu katika usimamizi wa hazina ya wanafunzi wa Yesu (Yohane 12:4–6).

Baada ya kuona matokeo ya kitendo chake, alijuta na kurudisha fedha alizokuwa amepokea. Hata hivyo, alikata tamaa na kushindwa kutafuta msamaha wa Mungu.

Kwa Wakristo wengi, Yuda Iskariote si alama ya usaliti pekee, bali pia ni mfano wa kushindwa kusimama katika ukweli, kupoteza mwelekeo wa maadili na kukata tamaa badala ya kutubu.

Ndiyo maana najiuliza kwa utulivu kabisa: mtu anapomwita mwenzake “Yuda”, anakusudia maana ipi hasa? Je, anamaanisha usaliti wa kisiasa, au anamaanisha pia maana zote za kidini na kimaadili zinazobebwa na jina hilo?

Haya ni maswali ambayo kila mmoja anaweza kuyatafakari kwa dhamiri yake mwenyewe.

Ndugu Wananchi,

Mimi naamini kwamba historia ya mtu haipaswi kuhukumiwa kwa maneno ya hasira, bali kwa matendo yake. Maisha ya uongozi hupimwa kwa uaminifu, uwajibikaji, utumishi kwa wananchi na mchango wake kwa Taifa.

Mafundisho ya dini zetu yanatupa mwongozo mzuri kuhusu namna ya kushughulikia tofauti za maoni.

Miongoni mwa hadithi maarufu za Mtume Muhammad (SAW), iliyopokelewa na Abu Huraira na kuandikwa katika Sahih al-Bukhari na Sahih Muslim, inasema:

"Mwenye nguvu si yule anayewashinda watu kwa mieleka, bali mwenye nguvu ni yule anayejizuia wakati wa hasira."

Mafundisho haya yanaelekeza kwamba nguvu ya kweli haipatikani katika uwezo wa kumshinda mwingine, bali katika uwezo wa kujitawala nafsi wakati wa hisia kali.

Leo hii ningeweza kujibu kwa maneno makali. Ningeweza kurudisha mashambulizi kwa mashambulizi. Lakini ninachagua njia nyingine; njia ya subira, njia ya staha na njia ya busara.

Hadithi nyingine iliyopokelewa kutoka kwa Shaddad ibn Aws katika Jami' al-Tirmidhi inasema:

"Mwenye akili ni yule anayejihesabu nafsi yake na kufanya kazi kwa ajili ya maisha ya Akhera; na asiye na busara ni yule anayefuata matamanio yake kisha akatarajia mema kutoka kwa Mwenyezi Mungu."

Katika mafundisho haya, busara inahusishwa na kujitathmini, kuwajibika na kufikiri kabla ya kutenda.

Qurani Tukufu nayo inasisitiza umuhimu wa busara na ukweli. Katika Surah Al-Baqarah 2:13 inasema:

"Na wanapoambiwa: Aminini kama walivyoamini watu wengine, husema: Je, tuamini kama walivyoamini wapumbavu? Hakika wao ndio wapumbavu, lakini hawajui."

Aya nyingine, zikiwemo Surah Al-Baqarah 2:130 na Surah An-Nisa 4:5, zinaunganisha upumbavu na kukosa busara katika maamuzi na wajibu wa maisha.

Ndugu Wananchi,

Siasa ni eneo la mijadala, ushindani wa hoja na utofauti wa mawazo. Lakini siasa zisipokuwa na mipaka ya maadili na staha zinaweza kuwa chanzo cha mgawanyiko badala ya maendeleo.

Ni wajibu wetu kama viongozi kupima athari za maneno yetu kabla ya kuyatoa hadharani. Tunapotumia mifano, majina au alama zenye uzito mkubwa wa kidini, tunapaswa kufanya hivyo kwa tahadhari kubwa kwa sababu jamii yetu inaishi kwa misingi ya imani, maadili na kuheshimiana.

Mimi nitabaki kuamini kwamba Tanzania ni kubwa kuliko tofauti zetu za kisiasa. Nitabaki kuamini kwamba maridhiano ni bora kuliko matusi, hoja ni bora kuliko shutuma, na umoja ni bora kuliko migawanyiko.

Kwa hiyo, kwa wale wanaonikosoa, nasema ahsanteni. Ukosoaji ni sehemu ya demokrasia. Kwa wale wanaonishambulia, nasema nawaheshimu. Na kwa wale wanaotafuta ukweli, nawaomba waendelee kuhukumu viongozi kwa matendo yao na mchango wao kwa Taifa.

Namalizia kwa kurejea somo kubwa la dini ambalo linafaa katika siasa na katika maisha ya kila siku:

"Mwenye nguvu si yule anayewashinda watu kwa mieleka, bali mwenye nguvu ni yule anayejizuia wakati wa hasira."

Mungu aibariki Tanzania.

Asanteni sana kwa kunisikiliza.”

 

Mwanakwetu akiwa ndotoni akamtumia mhusika hotuba yake, kisha akajiuliza:

"Je, Simai Mohammed Said atakuwa na uwezo wa kujibu?"

Mwanakwetu akajijibu mwenyewe:

"Hapa tumempiga Simai Mohammed Said na kitu kizito sana. Hawezi kutamka hata neno moja. Hapa ndugu Simai Mohammed Said ameshakuwa mufilisi wa hoja."

Wakati akiendelea kuwaza hayo ndani ya ndoto yake, ghafla akahisi kama mvua kubwa ilikuwa ikinyesha. Ndani ya ndoto hiyo hiyo, akakumbuka kuwa nje ya nyumba yake alikuwa ameanika nguo kadhaa. Hivyo akaona hana budi kuamka haraka ili akazisitiri zisilowane.

Akiwa bado katika mchanganyiko wa ndoto na uhalisia, simu yake ikaanza kuita. Mlio huo ukamwamsha usingizini kabisa.Alipofumbua macho, akagundua jambo la kushangaza sana. Kweli nje kulikuwa na mvua kubwa ikinyesha! Tukio hilo likamstaajabisha mno. Akapokea simu hiyo huku moyoni akimlaumu kidogo mpigaji wa simu hii, kwa sababu alikuwa amemtoa katika ndoto nzito na ya kuvutia aliyokuwa akiota.

 

Baada ya kuzungumza na ndugu huyo, akatoka nje haraka ili kuokoa nguo zake. Lakini alikuta tayari zimekwisha lowanishwa na mvua. Aliporejea ndani, akaangalia saa yake. Ilikuwa saa 3:00 usiku wa tarehe 4 Juni, 2026.

Kwa muda mrefu, Mwanakwetu alitafakari mambo yote aliyoyaona katika ndoto hiyo. Alitafakari hotuba, maudhui yake, watu waliokuwamo ndani ya ndoto hiyo na hata tukio la mvua ambalo lilionekana kana kwamba lilikuwa limetabiriwa na ndoto yenyewe. Baada ya kutafakari kwa kina, akaamua kuwasha kompyuta yake na kuanza kuyaandika yote aliyoyaota.

Ndivyo makala haya yalivyozaliwa.

Lakini sasa linabaki swali moja muhimu:

Je, makala haya yaitwe:

"Simai Mohammed Said Amepigwa na Kitu Kizito?,

Sasa Amekuwa Mufilisi? Au labda: Hotuba ya Dkt. Nchimbi Ndotoni?"

Baada ya kutafakari kwa muda, Mwanakwetu akafanya uamuzi wake.

Akachagua jina:

HOTUBA YA DKT. NCHIMBI NDOTONI

Mwanakwetu upo?

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 

 

 

 

 

 

 

0/Post a Comment/Comments