Adeladius Makwega – Musoma, Mara, Tanzania
Tafakari ya Dominika ya 12 ya Mwaka A wa Kanisa, iliyofanywa na Padri Paschal Ighondo, inatuhimiza waamini kutokuwa na woga. Inatukumbusha kuwa utume wa kumtangaza Kristo una changamoto zake, lakini Mungu yupo nasi daima, na thamani yetu ni kubwa mbele zake.
Tafakari hii iliyotolewa na Redio Vatikani inatoa dondoo muhimu tatu: Kutokata tamaa, Ushuhuda wa kweli, na Thamani yetu.
Padri Ighondo anasema somo la kwanza la Nabii Yeremia linatufunza jinsi wajumbe wa Mungu wanavyopitia mateso na shutuma. Licha ya hayo, wanapaswa kubaki waaminifu, kwani Mungu ni mtetezi wao. Hili ni dondoo la kwanza—kutokata tamaa.
Katika Injili, Yesu anawaambia wanafunzi wake: “Msiogope. Hakuna siri isiyofunuliwa.” Hivyo, tunapaswa kusimama kidete na kuishuhudia imani yetu bila woga, hata pale tunapokabiliwa na changamoto. Hili ni dondoo la pili—ushuhuda wa kweli.
Mungu anatujua na kutujali sana. Nywele zetu zote zinahesabiwa, jambo linalothibitisha kuwa tunathaminiwa mno mbele za Mungu. Hili ni dondoo la tatu na la mwisho—thamani yetu.
Kama haya ya Padri Ighondo hayatoshi, Kadinali Luis Antonio Tagle, Mkuu wa Propaganda Fide ya Kanisa Katoliki duniani inayosimamia uinjilishaji wa watu, alisisitiza haya:
“Tupo katika Jumapili ya kumi na mbili ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa. Katika Injili ya leo, Yesu anawapa wanafunzi wake mtazamo juu ya mateso na dhiki watakazoweza kukumbana nazo wanapomfuata. Anawaambia: ‘Msiogope mtu yeyote. Semeni waziwazi, na tangazeni juu ya paa yale niliyowafundisha—Habari Njema na ukweli.’
Basi, kwa nini wanafunzi wa Yesu wanatakiwa kufanya hivyo bila hofu? Kwa sababu Baba anawajua na anawajali. Wao wana thamani kuliko mashomoro wengi, ambao Mwenyezi Mungu huwalisha na kuwalinda. Tena, waweza kuweka tumaini lao kwa Yesu aliyesema: ‘Kila anayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele ya Baba yangu aliye mbinguni.’
Huu ndio moyo wa kutia nguvu na yakini tulio nao sisi pia, enyi ndugu zangu, tunapomfuata Yesu leo. Ufuasi wetu utajaribiwa na kutishiwa, lakini Mwenyezi Mungu ni mkuu kuliko majaribu yote.”
Haya ni kutoka Vatikani, katika Idara ya Propaganda Fide ya Kanisa hili ulimwenguni.
Kutokana na tafakari hizi mbili, Mwanakwetu ameandaa beti hizi tatu za ushairi:
(1) Kutokata Tamaa
Yeremia alilia, akazongwa na dhiki,
Shutuma zikamjia, akabaki thabiti,
Mungu mtetezi wake, hakumwacha hatarini,
Asikate tamaa kamwe, kwani Bwana yu karibu.
(2) Ushuhuda wa Kweli
Yesu asema wazi: “Msiogope kamwe,”
Siri zote hufunuliwa, kweli haisitiriki,
Ndugu, simama kidete, ushuhudie bila woga,
Imani iwe taa yako, gizani iking’ara.
(3) Thamani Yetu
Mungu atujua sote, hata nywele zahesabiwa,
Upendo wake mkuu haupimwi wala kupungua,
Thamani yetu kwake si haba wala ya dunia,
Sisi ni wake daima, mikononi mwake salama.
Mwanakwetu haishii katika beti hizo tatu za shairi, bali siku ya Juni 21, 2026, alikutana na simulizi hii njiani:
“Nilitoka nyumba ninayoishi kwenda dukani kununua mboga niliyoitamani kula Jumapili hii, hivyo nilianza safari kidogo. Njiani nilikutana na kijana anayeuza nguo huku akinadi maneno haya: ‘Chinga Boy hapa kutoka Mwisenge! Chinga Boy wa Mwisenge, njoo ununue nguo!’ Watu wakawa wanatoka na kumsimamisha; wapo wanaonunua nguo hizo, wengine wanatazama tu kwa macho.
Chinga Boy wa Mwisenge, akiwa na furushi la nguo mgongoni mithili ya mtoto, aliendelea kutembea. Alipofika sehemu, alisimama karibu na kundi la bodaboda. Mimi nilikuwa nyuma yake.
Jamaa mmoja mtu mzima alifika katika kijiwe cha bodaboda na kumchagua dereva mmoja ili ampeleke anapokwenda. Alipokuwa akitaka kupanda, akatokea mama mmoja mtu mzima wa rika sawa naye, akasema: ‘Naomba tupande pamoja ili nipunguze gharama za nauli.’
Yule jamaa alisita kupanda bodaboda hiyo pamoja na mama huyo, akamwambia: ‘Mama, panda wewe; mimi nitapanda bodaboda nyingine.’ Akaanza kumwita dereva mwingine.
Dereva wa bodaboda, mtu mzima, alianza kumwambia yule mama kwa Kijaluo maneno ambayo sikuyaelewa.
Yule jamaa aliyekuwa anataka kupanda alisema kwa mshangao: ‘Jamani, kweli nipande pikipiki huku nimempakata huyu mama?Au huyu mama amenipakata mimi? Kweli mnanitakia mema?’ Kisha akasema: ‘Mama, panda; mimi nitakuongezea hiyo pesa iliyopungua uende na huyu bodaboda.’
Mama huyo akaanza kutoa maneno makali sana kwa hasira. Mwishowe, yule baba hakupanda ile bodaboda; aliondoka kwa miguu akisema: ‘Hapa bwawa limeshaingia ruba.’”
Mwanakwetu aliendelea na safari yake pamoja na Chinga Boy wa Mwisenge, huku kijana huyo akiendelea kunadi:
“Chinga Boy wa Mwisenge, njoo upate nguo safi!”
Baadaye akasema:
“Kupanda bodaboda na mwanamke ambaye si mkeo ni hatari; linaweza kutokea jambo baya usilolitegemea. Lakini pia, yule mama alionyesha shida, hata alipoambiwa alipiwe, hakuchangamkia fursa hiyo; badala yake akakasirika.”
Mwanakwetu aliendelea na safari, akanunua mboga, kisha akarudi nyumbani kwake.
Je, kisa hiki cha barabarani kinahusiana vipi na tafakari ya Dominika hii?
Mwanakwetu aliwaza hivi:
“Hiki kisa kinaweza kuhusishwa vizuri na tafakari ya Dominika hii kwa kuangalia dondoo tatu: kutokata tamaa, ushuhuda wa kweli, na thamani yetu.
Kuhusu kutokata tamaa: yule mama alipokutana na kukataliwa kupanda pamoja na yule baba, alikumbana na hali ya kudharauliwa na kukosa msaada. Hii ni sawa na mateso na shutuma aliyopitia Nabii Yeremia. Kama Yeremia hakukata tamaa licha ya upinzani, vivyo hivyo katika maisha ya kila siku watu hukutana na kukataliwa au kudharauliwa; lakini mwaliko ni kubaki na moyo thabiti bila kuvunjika moyo.
Kuhusu ushuhuda wa kweli: yule baba aliyekataa kumpakata mama alionyesha yaliyo moyoni mwake waziwazi. Ingawa njia yake haikuwa ya huruma sana, alitoa msimamo wake hadharani. Yesu anasema ‘msiogope’—tusimame kidete katika ukweli. Hata hivyo, Injili inatukumbusha kuwa ushuhuda wa kweli unapaswa kuwa wa upendo na heshima, si wa kumdhalilisha mwingine.
Kuhusu thamani yetu: yule mama alikasirika kwa sababu alijihisi kudharauliwa. Lakini Injili inatufundisha kuwa kila mtu ana thamani kubwa mbele za Mungu. Hata kama watu wanatuona kwa namna fulani, Mungu anatujua na kututhamini.
Tukio hili linaonesha jinsi binadamu tunavyoweza kushindwa kuona thamani ya wengine, lakini Mungu haoni hivyo.
Kisa hiki kinatufundisha kuwa: tusikate tamaa tunapokutana na dharau au changamoto; tushuhudie ukweli kwa upendo na hekima; na tukumbuke kuwa kila mtu ana thamani mbele za Mungu, hivyo tuheshimu kila mmoja.”
Kwa ufupi, maisha ya kila siku—kama tukio hili la barabarani—yanatukumbusha jinsi Injili inavyoishi ndani ya maisha ya mwanadamu.
Wakati makala haya yanakamilika kutayarishwa, hali ya hewa Musoma Mjini ni nyuzi joto 26, uwezekano wa mvua ni asilimia 63, na upepo unavuma kwa kasi ya kilomita 19 kwa saa.
Mwanakwetu upo? Kumbuka:
“Hakuna siri isiyofunuliwa.”
Nakutakia siku njema.
Barua pepe: makwadeladius@gmail.com
Simu: 0717 649 257
.gif)








.gif)
Post a Comment