David Nkindikwa Aachiwe Huru MARA MOJA




Adeladius Makwega, MBAGALA. 

Aprili 10, mwaka 1993 ilikuwa ni Jumamosi ya kuamkia Sikukuu ya Pasaka ulimwenguni.

 

Mwanakwetu alisalia Ibada ya Misa ya Mkesha katika Kanisa la Mtakatifu Antony wa Padua, Mbagala Misheni, ambapo wakati huo ilikuwa ni Parokia ya Mbagala, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.

 

Misa ilisaliwa vizuri, na kisha watoto na vijana kutoka Koo za Kristo tuliosalia misa hii kutoka Mbagala Sabasaba, Mbagala Makuka na Mbagala Mangaya tukaanza kurudi nyumbani.

 

Wakati huo, Wakristo Wakatoliki wa Mbagala tulikuwa na machaguo mawili ya pa kusali, aidha Parokiani Mbagala Zakhem au kusali kilipo kituo cha kiroho Mbagala, ambapo lipo hili Kanisa dogo la Mtakatifu Antony wa Padua. Kwa hiyo, kituo cha kiroho Mbagala kilikuwa jirani na eneo salama kuliko kusali Mbagala Zakhem, maana palikuwa na msitu eneo lile la kambi la JWTZ na usalama mdogo kutoka kwa wakabaji.

 

Kumbuka msomaji wangu, tumesali sasa tunarudi nyumbani.


Kundi hili linapungua kila mmoja anapofika kwake.

 

Tulipokuwa tunatoka kanisani, wimbo wa mwisho ulioimbwa na Masista wa Shirika la Dada Wadogo wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam ulikuwa na maneno haya:

 

Haleluya, Haleluya, Bwana kafufuka kweli sasa ni mzima, (Haleluya) hafi tena (mara 2).

 

Haleluya, ameshinda mauti, kaburini sasa hayupo (Haleluya), hafi tena, Haleluya.

Haleluya, Haleluya, Bwana kafufuka kweli sasa ni mzima, (Haleluya) hafi tena (mara 2), Haleluya.


Haleluya, ameshinda mauti nasi kweli tumekwisha kombolewa, Haleluya, Haleluya.

Haleluya, Haleluya, Bwana kafufuka kweli sasa ni mzima, (Haleluya) hafi tena (mara 2).

Kaburini ametoka, mautini ameshinda, tufufuke pamonaye (pamoja naye), Haleluya, Haleluya.
Haleluya, Haleluya, Bwana kafufuka kweli sasa ni mzima, (Haleluya) hafi tena (mara 2).”

 

Sasa tunarudi nyumbani, wasichana wanaimba, sisi tunaikitikia huku hapa njiani wengine wanapiga stori ya kuvunjwa mabucha ya nguruwe na namna serikali ilivyolifanyia kazi jambo hili.

 

Kwa wale wanaokumbuka mwaka 1993, Waislamu kupitia Baraza la Kueneza Korani Tanzania kuliibuka kadhia ya mgogoro wa nyama ya nguruwe, na Rais Mwinyi akasema anayetaka kula chochote ni RUKSA (ale), na ndipo wakati huo Rais Ali Hassan Mwinyi alibatizwa jina la Mzee RUKSA.

 

Mkesha wa Pasaka wa Aprili 10, 1993 kulikuwa na wasiwasi wa kutokea vurugu makanisani, hivyo Jeshi la Polisi, nadhani chini ya RPC Mwinyi Dadi Ali, liliwasambaza polisi wengi makanisani na mitaani ili kupambana na vurugu kama Wakristo wangefanyiwa fujo siku hii.

 

Kumbuka hapa tunarudi nyumbani. Tulipofika njiani karibu na makazi ya Mzee Mafko, huku kushoto kwa akina Shempemba na jirani na mabasi ya Chura na Hauna Mbavu, njiani ya kuingia Mbagala Sabasaba Magengeni, wakatuibukia polisi wakatukamata wavulana wote wakubwa, ambapo Mwanakwetu (Adeladius Makwega), Antony (sasa mlokole), Emmanuel Mangaya, Fredrick Mfugale (Black Fish), na kijana mwingine wa Mbagala aliyeitwa Selestine. Polisi wakatufunga mashati kwa hoja mbili:

“Kwani nini mnaimba, mnampigia makelele usiku? Kwanini mnazungumzia kuvunjwa mabucha ya nyama ya nguruwe?”

 

Tukawa tunawajibu sisi tunatoka kanisani na ndiyo maana tunaimba. Hakuna kosa lolote tulilofanya.

 

Polisi wakasema hapana, mnafanya vurugu, wafungwe mashati. Tukaunganishwa na kundi la watu kadhaa waliokamatwa usiku huo na kuelekea Mbagala Kizuiani.

 

Wasichana, vijana wadogo wadogo na watoto tuliokuwa tunatoka nao kanisani wakawa wanalia wakikimbia kuelekea majumbani ili kutoa taarifa kuwa tulikuwa tunatoka kanisani, polisi wamemkamata mjukuu wa Makwega, mjukuu wa Mangaya, mtoto wa Mfugale na wengine wengi wanawapeleka Kituo cha Polisi cha Maturubai. Familia zikauliza wamefanya nini? Tulikuwa tunatoka kanisani tunaimba:

 

“Haleluya, Haleluya, Bwana kafufuka kweli sasa ni mzima, (Haleluya) hafi tena (mara 2).”

 

Wakawakamata tu, tena Fredrick Mfugale na Adeladius Makwega ndiyo waliotumikia kanisani, hawajafanya kosa lolote.

Haya maelezo aliniambia binamu yangu mmoja anaitwa Tulauke Shambani, sasa amefariki, ambaye alikuwepo usiku huu wakati tunatoka kanisani. Yeye alikimbilia nyumbani kwa baba yake mzazi anayeitwa Shabaani Katuna, ambaye alikuwa anaishi nyumba inayotazamana na nyumba ya mmiliki wa mabasi ya Chura Hauna Mbavu.

 

Hawa familia ya akina Shabaani Katuna (Waislamu), ambaye alizaa na binti Makwega, Faustina Makwega, wakawachukua watoto wote na kuwaongoza hadi majumbani kwa familia za Wakristo moja baada ya nyingine kueleza kilichotokea.

Sisi tuliokamatwa tukazunguka kwa mguu, tukakatiza mitaa ya Mbagala Kizuiani na baadaye sana kufika Polisi Maturubai. Kufika Kituo cha Polisi Maturubai, familia zote za Kikristo zilizokuwa zimesali Mbagala Zakhem na zile zilizokuwa zimesali Mbagala Misheni zilijaa polisi, zinauliza kwanini mmewakamata vijana wetu wakati wanatoka kanisani kusali?

 

Hapo sasa wale akina Shabaani Katuna, mama yake na ukoo wake wote waliambatana na familia za Kikristo hadi kituoni, na wale watoto akiwamo Tulauke Shabaani wakawa wanamueleza mkuu wa kituo kilichotokea.

Mkuu wa kituo Maturubai hana majibu maana watu hawajafika. Akasema,

“Jamani subirini kidogo wenzetu waliopo doria wafike ili tutoe majibu.”

Ghafla tukafika hoi bin taabani. Mkuu wa kituo cha Maturubai akasema,

“Akina nani walikuwa wanatoka kanisani?”

Tukanyoosha mkono. Tukafunguliwa mashati, tukakaa pembeni. Hapa sasa kila ukoo ukawa unamtaja jina kijana wake, kila ukoo ukampata kijana wake. Mwanakwetu sasa anajiangalia miguuni, huku kiatu chake kimoja kizuri cha Pasaka kikiwa kimepotea. Tukaachiwa na kuanza kurudi nyuma hoi bin taabani; hiyo sasa ni saa tisa usiku, huku tukiimba wimbo wetu ule ule:

“Haleluya, Haleluya, Bwana kafufuka kweli sasa ni mzima, (Haleluya) hafi tena (mara 2).”

 

Watu majumbani wanajua hao Wakatoliki wanatoka kanisani muda huu, kumbe ibada ya misa ya mkesha ilikwisha mapema mno.

 

Kesho yake ilikuwa Pasaka yenyewe, yaani Aprili 11, 1993. Tulienda kusali kama kawaida. Mchana tukawa tunaongea na vijana wenz wanzetu wakisema: nyinyi mlipata matatizo kwa kuwa hamkuwa na kadi ya CCM mifukoni; muwe makini, muwe mnatembea na kadi za CCM mifukoni. Kadi ya CCM hailali kituo cha polisi; huo ni mwiko mkubwa wa Chama Cha Mapinduzi, chama hiki kina heshima yake.

 

Kweli tulikula Pasaka vizuri na maisha yaliendelea kwa amani tele.

 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

 

Juni 26, 2026 Mwanakwetu amesikitika sana kutokana na kusambaa kwa taarifa za kutekwa kwa David Nkindikwa (kijana mwanamapinduzi) na kada wa CCM. Kutokana na taarifa hiyo ya kutekwa kijana mwanamapinduzi, Mwanakwetu pia aliwakumbukwa wote waliowai kutekwa na wengine hadi kuuwawa akiwamo Ali Mohammed Kibao, Soka n ahata Humphrey Polepole ndiyo maana Mwanakwetu alikumbuka tukio hilo lote alilolisimulia lililotokea miaka 33 iliyopita kijijini Mbagala, namna heshima ya kuwa mwana-CCM ilivyokuwa na imani kwa Watanzania kuwa kadi ya mwana-CCM hailali polisi.

 

Heshima huwa inaanza kwa ndugu zako na watu walio karibu yako, kisha heshima inaambukiza kwa wengine. Lazima heshima ya binadamu iwepo. Kama mtu kafanya kosa, akamatwe mchana kweupe; iweje achukuliwe kwa uficho? Hiyo siyo haki, hiyo si heshima. Matendo ya utekaji yanawanyima amani Watanzania, na wanaofanya hivyo wanajivunjia adabu wao wenyewe na familia zao. Kwa haya mambo, CCM itakuwa mgeni wa nani?

 

Kwa makala haya Mwanakwetu anasema: David Nkindikwa aachiwe huru mara moja.

 

Mwanakwetu upo? Kumbuka:

 

“David Nkindikwa Aachiwe Huru MARA MOJA.”

 

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com
0717649257

 

 

 

0/Post a Comment/Comments