ANATUTAZAMA, KISHA ANATUONEA HURUMA

Adeladius Makwega – Mwisenge MUSOMA TANZANIA.

 

Jumapili, Juni 14, 2026 – Kanisa la Mtakatifu Agustino, Parokia ya Mwisenge, Jimbo Katoliki la Musoma, Tanzania.

Padri Julius Ogolla alimtambulisha Frateli Norbert, mseminari mzaliwa wa Parokia ya Mwisenge, anayehudumu kutoka Shirika la Wajesuiti, mwenye taaluma ya sheria. Frateli Norbert alitoa tafakari ya Dominika hii.

 

“Hivi mnakumbuka Yesu alipofika Hekaluni na kuwakuta watu wakifanya biashara? Aliwafanyaje? Aliwafukuza? Hapana—aliwakemea kwa nguvu. Msiogope kusema aliwaadhibu. Tatizo ni hili hili la biashara na mali katika nyumba ya Baba yake kugeuzwa kuwa pango la wanyang’anyi.

Hebu Wakristo tutafakari: siku hizi mitaani, likisikika yowe la ‘mwizi! mwizi! mwizi!’, watu hufanyaje? Si wanatoka na kumkimbiza huyo mwizi? Mmoja akiwa na kibiriti, mwingine na dumu la mafuta, mwingine na matairi ya gari. Hakuna anayemuimbia mwizi taarabu au kumnyayulia vidole kwa furaha. Mwizi akiwa salama, ni kwa kukimbia; akishikwa, hukabiliwa na kifo.

Kumbukeni, Yesu alisulubiwa katikati ya wezi. Lakini nyuma ya pazia la maisha ya leo, jamii zetu zina wezi wengine—wanaovaa vizuri, wanaotembea kwa magari, na wanaolindwa. Je, ni nani anayeweza kuwapigia yowe? Nani anawakimbiza? Nani anawabebea dumu la mafuta? Mwizi ni nani? Amefanya nini? Kwa nini mmoja aitwe mwizi na mwingine abaki salama? Kwa nini baadhi ya wezi wanahukumiwa kifo, ilhali wengine wakubwa wanabaki bila kuguswa?

Ndiyo maana Yesu anatutazama, kisha anatuonea huruma.

Watu humchoma moto mwizi wa kuku au mbuzi huku wakishangilia na kujigamba kuwa wamemkomesha, lakini mwizi mwingine hubaki salama.

Kuna wezi ambao hatuthubutu hata kuwataja. Hata ukijaribu kupaza sauti, unaangalia kushoto na kulia—nani anakuona? Mara nyingine kelele hupigwa kupitia akaunti feki za Facebook, Instagram, Twitter na mitandao mingine ya kijamii.

Hapo ndipo tunapoona wazi: Yesu anatutazama, kisha anatuonea huruma.”

 

Mahubiri ya Frateli Norbert yalihusisha ushiriki mkubwa wa waamini, kwa maswali na majibu ya pamoja, yakisindikizwa na vibwagizo vya nyimbo za kanisa.

Kwa upande mwingine, kutoka Vatikani, kupitia Kadinali Luis Antonio Tagle, Mkuu wa Propaganda Fide (Idara ya Uinjilishaji), ilitolewa tafakari ifuatayo:

 

“Tuko katika Jumapili ya 11 ya Kipindi cha Kawaida. Injili ya leo, kulingana na Mtakatifu Mathayo, inatoa mafundisho matatu ya kutusaidia kuishi kipindi hiki cha ukuaji wa kiroho.

Kwanza, tunauona moyo wa Yesu—aliguswa na huruma kwa watu waliokuwa kama kondoo wasio na mchungaji. Bwana anawaona watu wake na anatuonea , huku pia anatuomba tushiriki kwa kuomba watenda kazi katika mavuno yake.

Pili, tunaona wanafunzi kumi na wawili waliopewa mamlaka ya kufukuza pepo na kuponya magonjwa. Wanafunzi hawa walitoka mazingira tofauti, lakini waliitwa kwa utume mmoja.

Tatu, Yesu anatuagiza kutangaza kuwa Ufalme wa Mbinguni umekaribia: kuponya, kufufua, kutakasa na kukomboa. Tumeitwa kuendelea na huduma yake kwa ukarimu—bila kudai malipo.

Bila gharama mmepokea; bila gharama toeni.

 

Je, tunawezaje kumsaidia Yesu katika huduma yake? Tugundue wito na vipawa vyetu katika maisha ya kila siku.”

Kutokana na tafakari hii, Mwanakwetu aliandika shairi lifuatalo:

Ubeti wa Kwanza

Je, mnakumbuka Yesu Hekaluni alipofika,
Akawakuta wafanyabiashara wakivunja patakatifu kabisa,
Nyumba ya Baba ikageuzwa kuwa soko la dhuluma,
Hasira yake ikafichua ukweli wa tamaa na udhalimu.

Ubeti wa Pili

Mitaani leo kelele: “Mwizi! Mwizi!” zasikika,
Watu hukimbia kwa hasira, huruma haionekani kabisa,
Mmoja na moto, mwingine mafuta, hukimbiza bila woga,
Lakini haki iko wapi, au hasira tu imetuteka?

Ubeti wa Tatu

Wapo wezi wa wazi, huadhibiwa mbele ya jamii,
Lakini wengine hujificha, wakilindwa na mali,
Wavalia suti, wapita kwa magari kwa nguvu na hila,
Ni nani atasimama kusema kweli bila hofu wala mila?

Ubeti wa Nne

Ndiyo maana Yesu hututazama kwa huruma,
Akiuona unafiki wetu na ukimya wa dhuluma,
Tukimwonea mdogo huku mkubwa tukimwacha huru,
Anatuita tuishi kweli kwa haki na nuru.

 

 

Baada ya ibada, Mwanakwetu alipokuwa anarudi nyumbani, alikutana na matukio mawili ya kutafakari:

 

Kwanza, ilipita pikipiki dereva alimsalimu kana kwamba wanajuana. Dereva huyo alisimama kuzungumza na wanawake wawili waliokuwa wamevaa rozari. Mmoja alisema:


“Yule wameuawa kwa wivu wa kazi yake nzuri. Kama mwenzako anafanya vizuri, jifunze kwake—usimdhuru.”

 

Baadaye, Mwanakwetu alikutana na kijana akizungumza kwa simu:

 

“Kuzaliwa katika ukoo mkubwa kuna faida, lakini pia hasara—hasa misiba mingi. Unaporudia kuomba ruhusa kazini, unaonekana kama mwongo.”

 

Wakati huo, hali ya hewa ya Musoma ilikuwa nyuzi joto 27–28°C, unyevunyevu asilimia 10, uwezekano wa mvua asilimia 47, na upepo wa km 10 kwa saa kutoka Ziwa Victoria.

 

Mwisho, Mwanakwetu anatuacha na ujumbe huu:

“Anatutazama, kisha anatuonea huruma.”

 

Nakutakia siku njema.

Barua pepe:

makwadeladius@gmail.com
Simu: 0717 649 257














 




0/Post a Comment/Comments