Adeladius Makwega – MBAGALA
Kati ya mwaka 1983 na mwaka 1985 yapo matukio kadhaa ambayo Mwanakwetu anayakumbuka sana, iwe ndani ya familia yake au kwa kuyahusisha na matukio ya kitaifa, japokuwa wakati huo alikuwa bado mdogo.
Mwaka 1983, Mwanakwetu alisajiliwa kuwa mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Kimanzichana. Mwaka 1984 alikuwa darasa la pili, akiwa na rafiki yake mkubwa Mohammed Kidundusi (Mohammed Mfupi).
Januari 30, 1984, Ali Hassan Mwinyi alichaguliwa kushika nafasi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Aprili 12, 1984, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati huo, Edward Moringe Sokoine, alifariki dunia katika ajali ya gari. Wakati huo Mwanakwetu alikuwa darasa la pili, muhula wa kwanza, katika Shule ya Msingi Kimanzichana.
Mara baada ya Ali Hassan Mwinyi kuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Kwanza wa Rais, kiongozi huyo alifanya ziara katika mikoa ya Pwani ya Tanzania, ambako ndipo yalikuwa makazi yake ya asili.
Mwanakwetu akiwa darasa la pili, kama nilivyodokeza, shuleni kwao walishiriki tukio moja kubwa la kitaifa.
Anakumbuka tukio hilo hivi:
“Mgeni mkubwa wa kitaifa alifika Kijiji cha Kimanzichana, kando ya njia ya kwenda vijiji vya Mkerezange na Mkamba. Kulifanyika mkutano mkubwa ambapo mama yangu mzazi, Mwalimu Doroth Mlemeta, alisoma risala ya wanakijiji hicho. Wakati huo alikuwa amevaa gauni la rangi ya njano lenye maua. Walimu wa Shule ya Msingi Kimanzichana walifanya shughuli mbalimbali, ikiwamo kuwapikia chakula viongozi kadhaa tangu ugeni huo ulipoingia hadi ulipoondoka siku iliyofuata.
Miongoni mwa wageni hao alikuwa Bi Sophia Kawawa. Sikumbuki kama alikuwa na cheo gani wakati huo, iwe ndani ya CCM, UWT au serikalini. Ninachokumbuka ni kwamba baada ya ugeni huo kuondoka, simulizi za walimu shuleni hapo zilihusu namna baadhi ya viongozi waliokuwa wakipiga vinyo walivyopepesuka baada ya kulewa, vituko vyao na maneno yao. Aliyesimuliwa sana alikuwa marehemu Bi Sophia Kawawa, mke wa Rashidi Kawawa na Mwenyekiti wa UWT Taifa.”
Walimu walisema mengi kuhusu Sophia Kawawa na mambo mbalimbali aliyoyafanya wakati wa ziara hiyo.Mwanakwetu anayakumbuka yote haya kupitia wazazi wake, ambao walishuhudia matukio hayo kwa macho yao.Leo anayasimulia kama alivyoyapokea kutoka kwa Francis Makwega na Doroth Mlemeta, wazazi wake.
Baada ya ugeni huo, nadhani kati ya miezi miwili au mitatu baadaye, familia yao ilihamia Kijiji cha Mkuranga. Hapo Mwanakwetu aliondoka huku akisikitika kumuacha rafiki yake Mohammed Kidundusi. Kwa bahati nzuri, alipofika Mkuranga alipata marafiki wengine, akiwamo Deogratias Msukuma, Shaha Uwanga na Hamisi Issa. Mwanakwetu hakuwa maskini wa marafiki.
Kwa hiyo, aliagana na Mohammed Kidundusi na kwenda kupata marafiki wapya akiwamo Hamisi Issa na wenzake.
Katika kipindi hicho kulikuwa na matukio kadhaa makubwa: kuchaguliwa kwa Ali Hassan Mwinyi kuwa Rais wa Zanzibar (Januari 30, 1984), kifo cha Edward Sokoine (Aprili 12, 1984), pamoja na ziara ya Ali Hassan Mwinyi katika Kijiji cha Kimanzichana.
Haya yote huwezi kuyaona katika nyaraka za serikali, magazeti au vyombo vya habari. Hata hivyo, kwa mashuhuda walioshuhudia matukio hayo ndipo unaweza kuyasikia kupitia simulizi zao, kwa sababu kila mmoja husimulia jambo kwa mtazamo wake.
Mei 31, 2026, Mwanakwetu aliambatana na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, aliposhiriki harambee katika Kanisa la Bikira Maria wa Fatima, Songe, Jimbo Katoliki la Musoma. Katika ziara hiyo, Mwanakwetu alikuwepo kama mwanahabari kutoka Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.
Miongoni mwa mambo aliyoyasema Kanali Mtambi ni haya:“Ukienda Galilaya watakufundisha njia hiyo, lakini katika Biblia haimo. Siku Yesu alipovunja na kupindua meza za wafanyabiashara Hekaluni, wale jamaa walifanya nini? Watu hao walichukizwa, wakasimama na kutaka kumpiga Bwana Yesu. Yesu alipoona hali imekuwa tete, aliondoka. Wale wafanyabiashara wakamkimbiza huku naye akielekea mlimani hadi kileleni mwa Mlima Kana. Hawakukata tamaa; walimfuata hadi kileleni ambako kulikuwa na ukingo mrefu. Yesu alipofika ukingoni alisimama. Wale jamaa wakaongeza kasi, lakini walipofika kileleni hawakumuona Yesu. Wakashangaa sana. Badala yake walimuona akiwa umbali wa kama kilomita kumi kutoka pale kileleni.”
Kwa hakika, kisa cha Yesu kuwafukuza wafanyabiashara Hekaluni kinasimuliwa katika Injili za Mathayo 21:12–13, Marko 11:15–17 na Luka 19:45–46. Hata hivyo, maelezo ya Kanali Mtambi yanatokana na mapokeo, kama vile Mwanakwetu alivyopokea simulizi kuhusu Sophia Kawawa katika ziara ya Ali Hassan Mwinyi mwaka 1984.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Katika makala haya, Mwanakwetu amejenga simulizi mbili: simulizi zake mwenyewe, za wazazi wake, walimu wake na wanakijiji wa Kimanzichana kuhusu matukio ya kitaifa; na simulizi ya Kanali Mtambi kuhusu mapokeo yanayomhusu Yesu Kristo baada ya kupindua meza za wafanyabiashara Hekaluni.
Kwa hakika, hapa unakutana na sentensi kama hii:
“Tukamkimbiza hadi kileleni ili tumkamate, lakini tulipofika kileleni tulishangaa kumuona akiwa umbali wa kilomita kumi kutoka pale kileleni. Na huo ulikuwa muujiza wake wa kwanza.”
Msomaji wangu, unaposoma kisa hiki katika Injili za Mathayo, Marko na Luka, pamoja na simulizi za mapokeo ya watu walioishi wakati wa Yesu Kristo kama ilivyosimuliwa na Kanali Mtambi, unaona wazi kuwa Yesu anabaki kuwa mshindi.
Swali la kujiuliza ni moja tu:
Wewe na mimi, katika maisha yetu hapa duniani, watu wakiyapiga picha maisha yetu, iwe kwa mapokeo taarifa rasmi tutabaki kuwa washindi au tutakuwa wale waliofilisika?
Msomaji wangu, naomba ujipige picha kisha ujipatie jibu.
Mwanakwetu upo?
Kumbuka:
“Anabaki Kuwa Mshindi.”
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717 649 257
.gif)
















.gif)
Post a Comment