Wafanyabiashara Waache Mara Moja Kuhihodhi CCM

Adeladius Makwega-MBAGALA.

Kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko ya ndani ya CCM kuwa nafasi za uongozi kupitia chama hiki zinapotangazwa ni ngumu sana mtu masikini asiye na pesa na fukara kupenya maana penya yoyote kupitia CCM silaha yake ni pesa kwa kuhonga wajumbe na viongozi tangu ngazi ya Mwenyekiti wa Kijiji, Diwani, Mbunge, hata wajumbe wa Halmashuri Kuu ya CCM Taifa na hata wajumbe wa Kamati Kuu, hali hii ipo hata katika kukalia nafasi za Wilaya na Mikoa maana penye uzia wewe penyeza rupia.

Wapo masikini huwa wanapenya lakini kwa ufadhili wa matajiri fulani fulani hauwezi kupenya masikini bila pesa mkono mtupu haulambwi.

“Ndugu wewe gombea uwenyekiti wa Wilaya, wewe gombea uwenyekiti wa Mkoa mimi nitakupa pesa za kuwahongo wajumbe lakini naomba ukishinda unilinde naamini 2025 nitagombea ubunge/naomba unilinde katika biashara zangu.”

Haya ndiyo mambo yanavyofanyika kwa miaka mingi na hata kuzungumzia rushwa ndani ya CCM wewe unayezungumzia unaweza kuonekana punguani, hauna kifua na unatoa siri za chama.

 

Kwa sasa wafanyabiashara ni wengi kuliko idadi ya wakulima na wafanyakazi kwa sababu mfanyakazi na mkulima hawa ni fukara ambapo hawezi kumuhonga mjumbe pesa ili wampigie kura lakini wafanyabiashara wanaweza kuinunua kura moja moja kati ya shilingi 10,000 -5,000,000 kulingana na mazingira ya vikao na nafasi inayogombewa, hapa hakuna siri.Wajumbe wamezoea rushwa hivyo akija mgombea asiye honga wanachukia wanasema kila mmoja afe na chake sisi tunakupa kura wewe unapata cheo kisha kila mmoja anayafanya mambo yake tukutane uchaguzi ujao.

Sasa tatizo la wafanyabishara wapo katika siasa kusoma ramani za biashara zao na siyo kuifanyika kazi jamii ya Watanzania.

“Mfanyabiashara yupo siasani ili kufanikisha kushamiri kwa biashara na miradi yake tu hakuna kingine.”

Ukweli huu ndivyo unavyoonekana baina ya mgogoro wa Mr Kepu mwana CCM  kutoka Ilala Dar es Salaam ambaye alitumia fedha zake za mkopo kuifanya kazi ya CCM ya vifaa vya kampeni na kuweka rehani jengo lake huku Chama cha Mapinduzi hakikulipa deni hili kwa wakati na baadaye jengo la Mr Kepu lililokuwa rehani kupigwa mnada na benki huku ikidaiwa mnunuzi ni mjumbe wa Hamalshauri Kuu ya CCM Taifa.

“Heri jengo hili angenunua mtu mwingine kwa nini anunue mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa?”

Mwanakwetu watu wapo CCM kusoma ramani na huku vita vya kibiashara vinafanikiwa kwa urahisi mno.

 

Kwa bahati nzuri Mwanakwetu anamfahamu Mr Kepu miaka mingi sana tangu akiwa kijana, huyu ni ndugu yake Mwanakwetu, hili lazima lisemwe wazi bila ya kuficha na kwa kuwa wanaolalamikiwa ni watu watatu , Chama cha Mapinduzi Taifa kwa kushindwa kulipa deni kwa wakati, Benki kwa kupiga mnada dhamana (Jengo la Ndugu Kepu) na tatu mnunuzi ambaye ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.

Mwanakwetu anasema wazi kuwa jambo hili lazima lifanyiwe maamuzi haraka maana linakitia aibu kubwa Chama Cha Mapinduzi katika umma wa Watanzania na huku ni ni Kusalua(kuvuliwa nguo) Nguo Hadharani.

 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Mwanakwetu anashauri CCM taifa kwanza ilipe deni inayodaiwa na Mr Kepu mara moja.

Pili Mr Kepu akishalipwa pesa zake amalize deni analodaiwa na Benki husika na hata kama lina riba na tatu Mr Kepu arudishwe jengo lake mara moja.

Nne CCM iwe makini katika nafasi zake za uongozi zigawanywe kwanza kwa wakulima , pili wafanyakazi na tatu wafanyabiashara katika mgau huu kundi la wafanyabiashara limekuwa kubwa kwa sasa na kuhodhi nafasi ndani ya CCM na hili linahodhi hata nafasi ya maamuzi ya chama na serikali. Hii hali ifike ukomo wake kinyume chake wakulima na wafanyakazi watakisusia hiki chama kwa kuona siyo chama chao tena bali chama cha mabwenyenye ambao wako chamani kusoma ramani za biashara zao tu.

Mwanakwetu upo? Kumbuka:

“Wafanyabiashara Waache Mara Moja Kuhihodhi Chama cha Mapinduzi.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257














 

 

0/Post a Comment/Comments