.gif)
Adeladius Makwega-MBAGALA
Mei 20, 2026 Mwanakwetu alitembelea Idara ya Mifugo ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, hapa alipokelewa vizuri na ndugu Mathias Mathew Lusheleja ambaye ni Afisa Mshauri wa Mifugo wa Mkoa huu.
Mwanakwetu akiwa hapa alitaka kujua kipi kinaendelea katika Ofisi hii ya Umma? Ndugu Lusheleja aliyasema haya:
“Mpaka sasa tulikuwa tunamalizia zoezi ya utambuzi wa mifugo kwa upachikaji wa heleni na chanjo ya awamu ya kwanza, mara baada ya Mkoa wa Mara kupokea shilingi milioni 175,612,000 na tumeweza kuchanja ng’ombe 561,597, mbuzi 127,373, kondoo 104,015 na kuku 1,467,901.”
Akizungumzia hoja hii ya chanjo alisema kuwa chanjo ya mifugo hiyo ya awamu ya kwanza ilianza Januari 15, 2026 na mara baada ya kuchanja kinachofuata ni kuangalia je mifugo iliyochanjwa imepokeaje chanjo hiyo?
“Unajua Julai 2026 tunaingia awamu ya pili ya chanjo lakini sasa tunaangalia seli ya mnyama aliyepata chanjo je imeonesha kuna kuongezeka kwa kinga ? Hoja siyo kuchanja tu maana baadhi ya wanyama kinga zao zinaweza kuwa chini hata baada ya chanjo, hivyo basi wenzetu wanaoshugulika na seli za wanyama kutoka Maabara ya Mifugo huja kufanya utafiti huo kwa sampuli watakazochagua sisi mkoa tunakuwa wapokezi wao tu.”
Mwanakwetu pia alitaka kujua changamoto katika zoezi hili la awamu ya kwanza zilikuwa zipi ?
“Ukosefu wa fedha za kutosha ikiwamo kwa kupokea fedha pungufu ambapo kwa awamu ya kwanza tuliomba milioni 250 ambapo mapokezi ya milioni 175 na ushehe ikiwa sawa na asilimia 70, huku upungufu huu unaibua kukosekana kwa vitendea kazi muhimu katika zoezi, pia kuna tatizo la ushiriki hafifu wa wadau ikiwamo wafugaji, Imani potofu kwa wafugaji kwamba akichanja mifugo yake itakufa, pia maafisa mifugo katika baadhi ya maeneo kupangiwa majukumu mengine na kuweka kando kazi yao ya msingi na hata udhaifu wa mitandao ambapo wakati mwingine zoezi lilisimama baada ya mfumo kutofanya kazi vizuri.”
Ndugu Lusheleja alisema changamoto hizi zinatajwa siyo kumsonta kidole mtu yoyote bali ili kila mdau wa sekta ya mifugo atimize wajibu na hili litasaidia mno awamu ya pili ikifika zoezi hili liweze kufanikiwa vizuri.
Baada ya mazungumzo haya Mwanakwetu aliagana na ndugu Lusheleja na kwenda kuyaandika makala haya.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kulingana na Afisa Takwimu Mkoa wa Mara Ndugu Issa Rajabu Mbombwe alisema kuwa hadi Aprili 2026 mkoa wa Mara unakadiliwa kuwa na watu 2,372,015 na kama utawagawa watu hao katika kaya kwa wastani watu watano kila kaya utapata kaya 474,403 na kulingana na kulingana na Afisa Ushauri wa Mifugo Mkoa wa Mara ndugu Lusheleja hadi Aptili 2026 mkoa wa Mara una ng’ombe 1,428,292, kondoo 579,131, mbuzi 661,793 na kuku 2,148,309.
“Kwa takwimu hizo za idadi ya watu mkoa wa Mara na zile kaya 474,403 inaonekana wazi kuwa kaya moja ya mkoa wa Mara inafuga kondoo mmoja, kaya moja mkoa wa Mara inafuga mbuzi mmoja na nusu, kaya moja mkoa wa Mara inafuga ng’ombe watatu na mwisho kaya moja ya mkoa wa mara inafuga kuku watano.”
Hoja hii ni kulingana na takwimu zilivyo na kulingana na uchambuzi wa Mwanakwetu kwa makala haya nah ii inatoa jawabu la Ng’ombe Watatu, Kondoo Mmoja, Mbuzi Mmoja na Nusu na Kuku watano yaani Ng’ombe 3,Kondoo 1,Mbuzi 1.5 na Kuku 5, haya ni mambo ua hesabu na uchambuzi wa Mwanakwetu.
“Mkoa wa Mara unaweza kujiwekea malengo ya kuongeza Ng’ombe 7 kwa kila kaya, kondoo 9 kila kaya, Mbuzi 8.5 kwa kaya na kuku 5 kila kaya ili kufikia shabaha ya Ng’ombe , Kondoo, Mbuzi na Kuku kumi kumi kwa kila kaya ili kuongeza tija iwe kwa chakula(Protini) na pia kwa kipatoh na hapa majibu yake yatakuwa yameubadilsiha kabisa mkoa wa Mara katika ufugaji , kwa chakula na kipato.”
Sasa msomaji wangu hapa tunaweza kuweka malengo hata ya miaka miwili ili kuipifika shabaha ya wanyama hao kumi kumi kwa kaya.
Hii siyo kwa mkoa wa Mara tu bali hata eneo lolote hapa nchini Tanzania ikiwamo mkoa wa Singida unaongozwa na dada wa Mwanakwetu Halima Binti Omari Dendego
Mwanakwetu upo? Kumbuka:
“Wadau wa Mifugo Timizeni Wajibu.”
Afisa Mifugo Mkoa wa Mara anapatikana kwa simu namba 0783-38-93-35
Nakutakia Siku njema
0717649257





.gif)
Post a Comment