Vyombo Vya Habari Muhimili Geresha

Adeladius Makwega-MBAGALA

Jumapili ya Mei 3, 2026, Mwanakwetu aliamka na kisha kuangalia katika shajala yake na kubaini kuwa ilikuwa ni siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Dunia. Kutokana na umuhimu wa siku hii Mwanakwetu kama MWANAHABARI akasema ngoja aandike makala kupamba siku hii.

Mwanakwetu akawasha kumpyuta yake na kwa bahati mbaya haikuwaka kwa sababu eneo hili majira ya asubuhi halikuwa na umeme. Hivyo basi akasogea kitandani kwake na kuiwasha simu yake, akaongeza sauti kisha akawa anasikiliza muziki. Baada ya dakika kama kumi umeme ulirudi na hivyo aliamka kitandani na kurudi ilipo kompyuta yake ili kuandika makala yake ya Siku ya Uhuru wa Vyombo Vya Habari, gafla umeme ulikatika tena na hata kompyuta yake ilivyowaka haikudumu muda mrefu.

 

Mwanakwetu akarudi tena kitandani akiendelea kusikiliza makala juu ya siku ya uhuru wa habari kwa mwaka wa 2026. Hili lilifanyika kwa muda kiasi lakini baadaye simu yake ikaishiwa chaji na yenyewe kuzima na hili likasababisa Mwanakwetu akalala tena usingizi.

Hapa ndugu huyu akiwa uzingizini akaota ndoto kadhaa:

“Anasoma ujumbe wa ndugu mmoja mwenye namba hii +255782047971 akinukuu makala moja ya Mwanakwetu kupitia kundi moja la WHATSAAP, kwanza huyu ndugu alimsalimu Mwanakwetu kwa maneno Kaka Kwema? Mwanakwetu akajibu Kwema. Kisha huyu ndugu chini ya neno kwema akaandika maneno haya:‘Kuna changamoto yoyote utumishi uwasilishe kwa maandishi ushauri badala ya social media mkuu.’

Mwanakwetu ndotoni akajiuliza, huyu jamaa vipi? Wewe unamuadhibu mtu kisha unatoka huko ulipo unataka kumfundisha mtu alie unavyotaka wewe?Hauna haki hiyo unaweza ukawa na haki ya kuadhibu lakini hauna haki ya kunifundisha namna ya kulia, nitalia nitakavyo.

Mwanakwetu ndotoni ikamjia taswira nyingine ya Balozi Humphrey Polepolem hapa Mwanakwetu akajiuluza huyu Polepole hakutekwa akiwa Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hakutekwa akiwa Balozi ya Tanzania nchini Malawi na hakutekwa akiwa Balozi wa Tanzania kule Kuba lakini alitekwa mara baada ya kuachia ngazi na kuwa kindakindaki katika mitandao ya kijamii wakati akitoa elimu ya uraia juu mambo mbalimbali ambayo ni changamoto ya jamii wa Watanzania.

 

Mwanakwetu ndotoni akawa anajiuliza mbona hatujasikia jaji anatekwa? Mbona hatujasikia mbunge anatekwa/ lakini wote wanaotekwa ni wale wanaojihusisha mitandao ya kijamii hasa wale wanaotoa elimu kwa umma kupitia mitandao ya kijamiii hasa tekinolojia ya habari?

Mwanakwetu katika usingizi ndotoni aliota mambo mengi kadhaa lakini mambo mawili ya mwisho ni haya: Kwanza aliota akiwa anafanya mahojiano ya kazi pale TBC Makao makuu mwaka wa 2009, hapa aliona taswira yupo katika paneli la mahojiano Tido Mhando akiwa mwenyekiti wa mahojiano ya kazi, hapa hapa Tido Mhando anasema:

“Wewe ni mwalimu unastashahada ya Ualimu na Shahada ya Kwanza ya Sanaa ya Habari, nimesoma makala zako za magazetini ni nzuri kama ulivyoziambatisha katika barua yako ya maombi ya kazi, sasa kama utapa ajira hapa TBC kama Mtayarishaji Vipindi utapata fursa kubwa ya kuongeza uwanda wa hadhira yako, maana pale unapoelimisha umma, maana mwalimu anafundisha darasa lake la wanafunzi katika ya 40, 80, 100 hawa ni wachache kwa wakati mmoja lakini ukiwa hapa katika redio yetu TBC Taifa(RTD zamani) inasikika nchini nzima kwa hiyo unakuwa na nafasi kubwa ya kuelimisha umma mkubwa kuliko kubaki katika ualimu na kwa hakika huo ndiyo Uandishi wa Habari , hii ndiyo taaluma yenye uwanda mkubwa wa kutoa elimu kuliko taaluma yoyote duniani.”

Mwanakwetu ndotoni akawa anatafakari kubwa kwa nini aliacha kazi ualimu ambapo ni kazi aliyoifanya vizuri na bila ya kusumbuliwa na mtu yoyote yule wala kutumiwa ujumbe wa vitisho vyoyote vile kwa miaka karibu 10 aliyofundisha shule ya msingi na sekondari za binafsi na umma nchini Tanzania? Lakini uandishi wa habari umekuwa kazimbaya kwake mara kufuta kazi , mara kukamatwa, mara kuitwa polisi, mara kulala mahabusu mara barua, mara kutishiwa hiki na kile? Huku sasa watu kadhaa wakitekwa na hawajulikani walipo?

Kwanini mie nife huku ndugu zangu wanisalie ibada ya mazishi kwa mashaka mashaka, ndugu yetu atarudi leo atarudi kesho? Kisa ni kujikita katika taaluma niliyosomea kwa hiari yangu? Maana Vyombo Vya Habari hasa mitandao ya kijamii inapata changamoto. Ati nyuma ya pazia wanahabari wapakwa mafuta kwa mgongo wa chupa nyinyi ni muhimili wa nne baada ya Serikali, Bunge na Mahakama? Ebo kama Vyombo Vya Habari vina adhi sawa na hao wengine mbona Majaji wapo salama? Mbona wabunge wako salama? Mbona viongozi wako salama? Mwanakwetu akahoji ndotoni au huku ni kunakotazamwa kama muhimili wan ne Kisingizio? Dangaya toto kula kunde mbichi.? Vyombo Vya Habari Muhimili Kisingizio. 

 

Msomaji wangu kumbuka Mwanakwetu alikuwa amelala usingizini kitandani na haya yote anayoota tu, gafla muziki ukaanza kucheza tena na hili likamshitua Mwanakwetu na kweli alipoamka alibaini kuwa umeme umerudi, akawasha kompyuta yake ndipo akaamua kutayarisha makala haya kama yalivyo tangu umeme ulivyokuwa unakatika na ndoto alizoziota.

 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Uhuru wa vyombo vya habari ni haki ya wanahabari na vyombo vya habari (magazeti, redio, televisheni, mitandao) kukusanya, kuchapisha, na kusambaza taarifa bila kuingiliwa, kudhibitiwa, au kuogopa adhabu kutoka kwa serikali au mamlaka nyingine yoyote ile. Uhuru huu ni nguzo muhimu ya demokrasia inayowezesha wananchi kupata taarifa sahihi na kuwawajibisha viongozi wao. Waandishi Wasio na Mipaka (RSF) hutoa orodha ya kila mwaka tangu 2002 ikiorodhesha nchi 180 kulingana na kiwango cha uhuru wa habari kila Mei 3 ya kila mwaka ambayo ni Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, iliyoanzishwa na UNESCO mnamo mwaka 1991. Uhuru wa habari mara nyingi hukabiliwa na vikwazo, kutoka serikali, vyombo vya ulinzi na hata wamiliki wa vyombo hivyo kwa maslahi yao binafsi, vitisho kwa waandishi, na udhibiti wa maudhui, hali inayoendelea kujadiliwa duniani kote.”

Msomaji wangu hii ni siku ya wanahabari ulimwenguni, ebu fikiria Mwanakwetu kalala kidogo kupumzika anaotoa juu ya matukio ya kweli juu yake yeye mwenyewe kama mwanahabari. Unaweza kudhani uhuru huu anayekandamizwa ni yule mwanahabari pekee yake hili hapana inayokandamiza zaidi ni jamii ili inayolengwa na habari hiyo isijue ukweli wa jambo linalojadiliwa.

 

Yakumbuke haya maelezo ya Tido Mhando mwaka wa 2009 pale Studio ya Morise Nyunyusa wakati wa mahojiano ya kazi:

“…utapata fursa kubwa ya kuongeza uwanda wa hadhira yako, maana pale unapoelimisha umma, maana mwalimu anafundisha darasa lake la wanafunzi katika ya 40, 80, 100 hawa ni wachache kwa wakati mmoja lakini ukiwa hapa katika redio yetu TBC Taifa(RTD zamani) inasikika nchini nzima kwa hiyo unakuwa na nafasi kubwa ya kuelimisha umma mkubwa kuliko kubaki katika ualimu na kwa hakika huo ndiyo Uandishi wa Habari , hii ndiyo taaluma yenye uwanda mkubwa wa kutoa elimu kuliko taaluma yoyote…”

Ebu fikiria ujumbe wa ndugu huyu mwenye namba hii+255782047971 hoja ilikuwa ni makala ya Mwanakwetu juu ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma ambapo Katibu wake mkuu ndugu Juma Seleiman Mkomi kuomba trioni 1.4 katika bajeti yake ya 2026/2027 kama pesa matumizi ya kawaida ya wizara hii . Makala ya Mwanakwetu ilijenga hoja kuwa pesa hizi ni nyingi maana unajenga madaraja ya Bugogo Busisi Mawili, Daraja ya Tanzanite la Dar es Salaam 6, sasa iweje pesa hii iende katika matumzi ya kawaida? Lazima pesa hii iende katika miradi ya maendeleo na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma haipaswi kupewa pesa hiyo ingekuwa kwa miradi ya maendeleo sawa, hapa Mwanakwetu harudi nyuma. Huu ni ushauri maana Ofisi wa Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma inafahamika hata majukumu yake hii ni ofis yetu maana utumishi wa umma ni mali yetu.

 

Kama hali hii ya changamoto zote zinapoendelea, hatupaswi kuvihusisha vyombo vya habari  na mihimili hiyomitatu  maana huko ni kuvifanya vyombo vya habari kama muhimili geresha.

Msomaji wangu leo nilitaka nitafakari na wewe juu ya umuhimu wa vyombo vya habari na kwa hakika haya niliyayaeleza yalinijia ndotoni, kwa moyo wangu mweupe nakula kiapo sijakata tamaa nitaendelea kuifanya kazi hii kwa moyo wote na kwa nguvu zake zote nitakazojaliwa na Mungu Baba Mwenyeenzi.

Mwanakwetu Upo? Kumbuka:

“Vyombo Vya Habari Muhimili Geresha.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 

 

 

 

 
























 



0/Post a Comment/Comments