Utumishi wa Umma Mithili ya Tanga Ndugu

Adeladius Makwega-MBAGALA

Kwa wale wasomaji wa Mwanakwetu ambao siyo wenyeji wa pwani, naomba siku ya leo nieleze kidogo maana ya neno tanga:

“Tanga ni aina ya kitambaa kikubwa kigumu kisichoweza kuchanika kwa urahisi , kisichopitisha hewa, kisichoharibika kwa maji baridi au maji chumvi kwa urahisi, kisichoharibika kwa jua kali kwa urahisi, hakiozi kwa haraka , kinachopokea upepo na kuwambika vizuri, hivyo kuwezesha chombo cha majini kusukumwa na kusafiri majini kutoka eneo moja kwenda lingine kwa nguvu ya upepo tu bila ya kutumia nishati yoyote ile. Katika mazingira ya Pwani ya Tanzania hasa maeneo ya Mbagala, Kilindoni, Mikindani, Kisiju Pwani na maeneo mengine kando ya Bahari ya Hindi zipo aina kadhaa za vitambaa madhubuti vya kutengeneza tanga ambavyo ni PAMBA NENE ambayo ndiyo inatumika tangu enzi kama tanga katika majahazi, pia hata kitambaa cha Polista na mwisho hata vitambaa vya Nailoni.”

Katika mazingira haya haya ya Pwani ya Tanzania kila kunapokuwa na jambo kubwa la kifamilia, jamii hizi huwa na utaratibu wake wa kukaa pamoja kujadili jambo hilo na namna wanavyolitatua iwe harusi au msiba huku jamii kando ikishiriki kwa asilimia zote. Hapa ukiitazma misiba mingi ya Kiafrika inakuwa ni kitu kinachofahamika kama tanga la wote na kisha baada ya mazishi watu wakitawanyika kunakuwa na tanga ndugu. Haya ni mambo ya mswahili na hapa dhana ileile ya  tanga la jahazi ambapo wakati wa msiba ndugu huketi na kukaa juu ya kitambaa kigumu kiwe mkeka , jamvi na hata tanga kuukuu ambalo lina vilaka vingi, halitumiki tena kuwambwa katika jahazi lisije kuleta misiba baharini. Huku sasa tanga chakavu linatumika kama zulia la kukali misibani. Matanga haya chakavu huuzwa sana gulioni kwa bei nafuu yakitumika kama mazulia, vilago na hata vifaa cha kuanikia mazao na nafaka zinginezo.

Msomaji wangu tambua kuwa hapa ndipo dhana ya tanga jamaa na tanga ndugu linaibuka.

Natambua msomaji wangu tangu upo pamoja na Mwanakwetu tangu alipotoka na wewe kutoka katika dhana ya maana ya tanga hadi tanga jamaa na tangu ndugu.

 

Mwanakwetu anakuomba msomaji wake, kwa hisani yako ukumbuke hili:

“Hata siku moja hauwezi kuona tanga jipya linakaliwa msibani, mara zote tanga linalokaliwa msibani lina vilaka vingi sababu ni moja tu gharama ya kununua tanga jipya ni kubwa maana Waswahili Ufukara ni Hadaa, ufukara ni hiari yetu kwa sababu hiki ni kitambaa cha pamba ngumu ambayo inatumika kwa kazi maalumu ikiwamo tanga la jahazi na bei huwa kubwa, huku mita moja kwa mwaka wa 2026 inafika hata dola sita za Kimarekani na ndiyo maana Waswahili wana msemo raha ya jamvi/tanga vilaka.”

Msomaji wangu kwa hisani yako naomba univumilie kidogo sasa twende kwa sote msibani:

“Katika tanga jamaa ndipo unawekwa mustakabali wa mambo yote na mwisho mnazika na mambo yakiwa yamekamilika ndipo tanga ndugu linakaliwa.”

Msomaji wangu nakuomba kwa hisani yako nikutoa katika tanga jamaa na tanga ndugu sasa twende katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambayo ni Wizara kamili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo Katibu wake Mkuu anaitwa Juma Seleiman Mkomi. Msomaji wangu nakuomba kwa hisani yako hapa nikusimulie kisa hiki :

“Kuna wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifanya uteuzi wa ndugu mmoja, akala kiapo na kuelekea kutimiza majukumu yake. Kazi ikafanyika vizuri akiwa kazini kuna wakati kukawa na mapendekezo ya wajumbe wa bodi mojawapo chini yake, majina yakapitia ngazi kadhaa na mwisho mbele ya kiongozi husika kisha kiongozi akamuagiza Mwandishi Mwendesha Ofisi (Karani) ayachape ili yaende hatua ya mwisho ili majina ya bodi yatangazwe.

Karani alipoyapokea majina akayasoma kisha akabaini madhaifu ya mapendekezo haya. Karani akalibeba faili hadi kwa bosi wake na kisha kumwambia bosi wake maneno haya: ’Bosi samahani sana! Kuna kitu naomba niongee na wewe, lakini nitakapo kwambia usinielewe vibaya, shabaha ni kujenga na siyo kubomoa.’ Karani huyu mnyenyekevu mno, karani mzoefu, bosi alitii ombi la karani mnyenyekevu- bosi akasema hakuna neno niambie tu usiwe na shaka. Karani akasema:

‘Katika haya majina, lipo jina la mkeo, hili ni kosa katika Utumishi wa Umma linaweza kuleta maneno na kuharibu jina lako nzuri milele na kazi nzuri unayoifanya isionekane tena, naomba jitahidi waambie waliopendekeza wapendekeze jina lingine na hili jina liondolewe.’ Bosi huyu pale pale aliupokea ushauri huu kwa mikono miwili, ushauri ulimuingia akilini na kuchukua faili na kuandika katika dokezo jina hili liondolewe na pendekezeni jina lingine. Karani alichuku file na kuwapelekwa wahusika kulifanyia kazi mapendekezo mapya yalifanyika.”

Nina hakika msomaji wangu popote ulipo umeuelewa vizuri mfano huo.

 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Kwa sasa utumishi wa Umma wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umekumbwa na shida ya udugu na jamaa tangu ngazi za uwaziri, ubunge hali inaonekana huku wengine wanavuka mipaka hadi bungeni waka zaidi ya mmoja wa mtu mmoja wanatambulishwa. Hii ni kengele ya hatari, vipi katika utumishi wa umma? Wakati vijana wanatafuta fursa za kazi za kuajariwa wakifanya mahojiano ya kazi kwa kusafiri safari ndefu, wakiulizwa maswali ya hesabu wakati wao ni walimu wa lugha kila wakati mahojiano kazi na ajira hakuna.

 

Jamani jamani jamani tuwe na soni na tuwe aibu maana jamii inalia uhaba wa ajira huku familia moja inajilimbikizia ajira tele, hili ni kosa kubwa.

 

Jamani Utumishi wa Umma Mithlli ya Tanga Ndugu? Ebu Mtazameni Julius Nyerere, mkewe huyu Maria Nyerere anatokea eneo linalofahamika kama KOMUGE Kinesi, Wilaya ya Rorya ambayo wakati huo ilikuwa ni Wilaya ya Tarime, Maria Nyerere anatokea familia ya Watanzania wa kawaida kabisa, Julius Nyerere amekula mshahra wake wa urais na binti KOMUGE Maria Nyerere, ebu mimi na wewe tujifunza kitu. Kutokana hili Mwanakwetu anakumbuka maneno ya Julius Nyerere alipokuwa anatatua mgogoro wa Rwanda na Burundi aliyasema maneno haya:

“Kwa mataifa masikini , utumishi wa umma na nafasi za uongozi ni fursa kwa jamii yote, kwa hiyo kama ukilimbikiza utumishi wa umma na vyeo kwa watu wachache unawanyima walio wengi fursa hizo na hili ndilo chanzo cha migogoro mingi ya Afrika.”

Kwa makala haya Mwanakwetu alitamana Katibu Mkuu Ofisi ya Raias Menejimenti ya Utumishi wa Umma ndugu Juma Seleiman Mkomi angekuwa kama karani yule aliyemwambia bosi wake maneno haya:

“…haya majina lipo jina la mkeo, hili ni kosa katika Utumishi wa Umma linaweza kuleta maneno na kuharibu jina lako milele na kazi nzuri unayoifanya isionekane tena, naomba jitahidi waliopendekeza wapendekeze jina lingine…”

Huyu mama karani hakufukuzwa kazi kwa ushauri wake huo na hadi kesho ni mtumishi wa Umma wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mungu atamjalia atastaafu salama mwaka wa 2033.

“Haupewi uongozi ili ujitengenezee fursa wewe mwenyewe na watu walio na nasaba na wewe bali uongozi unapewa ili utoe fursa kwa jamii nzima.”

Kwa hakika viongozi wana ulinzi kila walipo lakini sisi mitaani hawa vijana ambao hawana kazi ni watoto wetu, wanaweza kufanya chochote dhidi ya sisi wazazi wao. Hapa lazima wale wanaonyamazia hali hii tuwaambie hadharani hili ugonjwa huu upate tiba na Mwenyezi Mungu atakapo tuchukua katika maswali na majibu tutajitetea :

“Mimi nilitayarisha makala lakini hawakunisikia.”

Mwanakwetu Upo? Kumbuka:

“Utumishi wa Umma Mithili ya Tanga Ndugu.”

Nakutakia Siku Njema.

 

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 

 

 






















 

 

0/Post a Comment/Comments