Ukiiuza Musoma Utakaa Wapi?

 

Adeladius Makwega-MBAGALA.

Jumamosi ya Mei 9, 2026, Mwanakwetu alitembelea ukurasa mmoja wa mitandao ya kijamii wabinti wa Kitanzania anayejulikana kana Viola Mtetezi ambaye hutoa mada kadhaa za kijamii kulingana na muktadha wa hali ya taifa la Tanzania ulivyo kwa wakati huo, ukurasa wake siku hii aliweka video fupi ya nyimbo kadhaa za makabila ya Kitanzania na huku akicheza katika ukanda mfupi kwa madaha mno.

Kwa ukweli wa Mungu na uwonga dhambi, Mwanakwetu alipotazama ukanda huu wa Viola Mtetezi udenda ulimtoka na kama kungekuwa na watu wengi kando yake lo salale Mwanakwetu angeficha wapi fedhea hii?Angeficha wapi sura yake! Mungu bahati Mwanakwetu alikuwa mwenyewe, alijifuta udenda huo kwa leso yake kuukuu na kuendelea kumpekua Viola Mtetezi, leo Mwanakwetu mpekuzi.

Mwanakwetu alizitazama video zote moja baada nyingine, huku akivutiwa mara dufu na video moja iliyosindikizwa na wimbo uliyokuwa na maneno haya:

“Ati mwenzenu naiuza Bunda, mwenzenu nauza Musoma, mwenzenu naiuza Majita, Nauza Kiabakari, Nauza Tarime, Nauza Nyamongo...”

Mwanakwetu akajiuliza huyu Viola Mtetezi anapeleka sokoni nini? Viola Mtetezi kawa dalali! Huku chini ya video hii kuna ndugu mmoja akaandika akisema dada yangu kipenzi kama ukiiuza Musoma, ukaipeleka sokoni Tarime alafu Bunda na Kiabakari wewe utakaa wapi? Hapa Mwanakwetu akacheka hahahaha…! Kisha aliirudia mno video hiyo mithili yupo katika ukumbi wa muziki na akimwambia disk joka rudia tena, once more, akisema kwa sauti ya juu. Msomaji wangu kumbe Mwanakwetu alikuwa mwenyewe akiitazama video hii. Kwa chonjo Mwanakwetu alikutana na maoni yaliyo katika swali kutoka kwa Twaha Kabajemi yeye alisema Kumbe Musoma kuna Warembo? Mwanakwetu akajibu moyoni Twaha Kabajemi kalagha bao(baki hivyo hivyo):

“Wewe unasema Musoma tu? ndugu yangu bado kuna Tarime, Butiama, Bunda, Serengeti na Rorya huku mambo ni hatari. Kuna warembo hatari, ukitaka kuijua mbunga yenye wanyama wakali itembelee. Kama unawapenda weusi wa asili ndugu yangu wamejaa tele na kama unapenda weupe kama Wamanga Koko wapo Musoma mjini masalia ya Wahindi na Waarabu wa tangu mwaka wa 1880 chaguo lako, warembo wamenona kwa kula samaki za Ziwa Victoria.”

Mwanakwetu akayasoma maoni haya huku video hii ikichezwa, mara akakutana na jina la Kiraka Kakwaya yeye akasema- jamaini nyumbani ni nyumbani, ringa na asili yako ulikotokea. Mwanakwetu hakuwa na hakika kama Viola Mtetezi ni mzaliwa wa Mkoa wa Mara lakini siku akikutana naye atamuuliza.

 

Baadaye Mwanakwetu ndipo alipoamua kuyatayarisha makala haya unayoyasoma.Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Viola Mtetezi alicheza kipande cha wimbo kama ngoma ya Wakurya ya Litungu na Isubane lakini wimbo huu ulikuwa wa maadhi ya kisasa, ukiwa ni wimbo wenye jina Nauza Bunda, Musoma na Tarime wa msanii anayefahamika kama Chief Maker ambapo kwa uchambuzi wa kimaantiki wa ujumbe wa mwanamuziki huyu katika wimbo huu anamaanisha haya:

“Yeye ni msanii wa muziki wa Bongo fleva ya Tanzania na kutokana na uwezo wake katika Sanaa anasema muziki wake (Sanaa yake) anauza Bunda, Musoma, Tarime, Kiabakari na Nyamongo na ndiyo maana mwishoni mwa wimbo huo anawapongeza sana disko joka wanaoucheza muziki wake.

Pia kama hili la kwanza halitoshi maneno jamani mimi nauza Musoma, Nauza Tarime yakiwa Kibwagizo tu ndani ya wimbo huu. Huku maeneo haya yaliyotajwa ni miji kadhaa maarufu ndani ya Mkoa wa Mara.”

Huku Mkoa wa Mara ni eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lenye makabila yenye ngoma za kibabe kama vile Litungu ambazo kwa utafiti wa Mwanakwetu ni ngoma zilizopitia changamoato kubwa sana ya kisanaa ambapo mara nyingi ngoma hizi za kibabe huwa hazipewi nafasi katika matukio kadhaa kitaifa. Changamoto ya ngoma hizi ni kuchezwa kwa kutumia nguvu na wakati mwingine huchezwa kwa kutumia marungu, upinde, mikuki kama zilivyo ngoma za Kimasai na Wanyamwezi na Wasukuma .

 

Ukitaka kupima hili angalia aina za ngoma zinazopewa nafasi katika matukio ya kitaifa ngoma utabaini ngoma za kibabe zinakuwa kando huku ngoma kama ile Mganda kutoka mkoani Ruvuma ikipewa kipao mbele.

Kama wewe ni mtu makini hali hii haikuanza leo hata tangu uhuru yaani ile Disemba 9, 1961 Viwanja wa Uhuru siku hii Tanganyika Broadcasting Cooperation walirusha matanganzo ya moja kwa moja na yalitangazwa watangazaji wawili maarufu mno wakati huo marehemu Godfrey Mgodo na marehemu David Wakati . Wakati Davidi Wakati anaaga uwanjani aliyasema maneno haya…

“Wasikilizaji tupo hapa uwanjani tangu mapema sana, mmesikiliza burudani ya ngoma zetu za asili za Tanganyika na hotubu kutoka kwa watukufu kadhaa, sasa tunawarudisha studioni, sisi hapa uwanjani hadi njaa zinauma sana, mwezangu ni Godfrey Mgodi mimi ni Davidi Wakati.’

Kwa wale wanaokumbuka au wale waliosikiliza matangazo haya ya moja kwa moja ya Siku ya Uhuru wa Iliyokuwa Tanganyika Disemba 9, 1961 watakumbuka hakukuchezwa hata ngoma moja asili ya kibabe zaidi ya ngoma ya Mganda na ile ya Tarumbeta Bini Mazumari.Hoja ni hii uteuzi wa ngoma hizo na kuziweka kando ngoma za kibabe ulifanyika kwa matakwa kadhaa na umeendelea hadi kesho. Hali hii ya kuzinyima fursa ngoma za kibabe imeendelea miaka nenda miaka rudi na jamii zinazocheza ngoma hizi ni jamii hasa za wafugaji. Jamani tuambiane ukweli hizi ngoma za asili zenye kuchezwa kibabe na kiukakamavu zina umuhimu mkubwa kwa jamii ya sasa n ahata baadaye maana kwa sasa hata kupambana na mambo ya kipuuzi kama vile ushoga maana vijana katika ngoma za kibabe wanajivunza kuwa iwe mwanaume au mwanamke lazima uwe unajitambua na uwe mkakamavu na huo ndiyo Uafrika wenyewe.

 

Msomaji wangu najua tupo pamoja na yote haya yanakufikia hapo ulipo kwa heshima ya Viola Mtetezi.

Mwanakwetu upo? Kumbuka:

“Ukiiuza Musoma Utakaa Wapi?”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 

 














 

 

0/Post a Comment/Comments