.gif)
Adeladius Makwega -Musoma
“Tunasherehekea kupaa kwa Bwana. Neno la milele la Mungu, aliyefanyika mwanadamu katika Yesu, alihubiri, akafa, na kufufuka ili tupate wokovu. Sasa yuko katika uwepo wa milele wa Baba lakini kabla ya kupaa kwa Bwana mbinguni, alikaa siku arobaini hapa duniani. Alikutana na wanafunzi wake na kuwafundisha tena. Wakati uliopangwa ulipofika, alirudi kwa Mungu huku akiwaagiza wanafunzi wake kwenda katika utume. Aliwaambia wanafunzi wake:
‘Mamlaka yote mbinguni na duniani nimepewa. Basi, enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu, na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru. Nanyi tazameni, mimi nipo pamoja nanyi siku zote hata mwisho wa nyakati.’
Leo sisi pia tumetumwa kumshuhudia Kristo popote tuendapo, tukiwa na uhakika na faraja ya ahadi ya Yesu kwamba atakuwa pamoja nasi siku zote hadi mwisho wa nyakati.”
Haya ni sehemu fupi ya mahubiri ya Kadinal Luis Antonie Tagle Jumapili ya Mei 17, 2026 ambaye ni Kiranja wa Propaganda Fide ya Kanisa Katoliki inayoshugulika na Uinjilishaji wa watu Ulimwenguni yenye makao yake makuu pale Vatikani.
Msomaji wangu kuipamba dominika hii Mwanakwetu ameandaa utenzi wa Kupaa kwa Bwana:
Tunasherehekea
leo, kupaa kwa Bwana wetu,
Neno la Mungu milele, lamfanyika mwanadamu,
Kwa Yesu alihubiri, akafa akafufuka,
Tupate wokovu wote, kwa pendo lake kuu.
Sasa
yuko mbinguni, kwa Baba wa milele,
Katika utukufu mkuu, wa enzi isiyokwisha,
Ametukuka kwa haki, mshindi wa mauti,
Ametufungulia njia, ya uzima wa kweli.
Kabla
hajapaa juu, alikaa nasi hapa,
Arobaini za siku, akiwafundisha tena,
Aliwakusanya wote, wanafunzi wake wapendwa,
Akiwapa mafundisho, ya imani iliyo hai.
Wakati
ulipotimia, akarudi kwa Baba,
Lakini hakutuacha, bila kazi ya kufanya,
Aliwatuma wafuasi, kwenda ulimwenguni kote,
Kuwaita watu wote, waingie wokovuni.
“Mamlaka
nimepewa, mbinguni na duniani,
Enendeni mkafundishe, mataifa yote pia,
Wabatizeni kwa jina, la Baba na la Mwana,
Na Roho Mtakatifu, mkawafundishe yote.”
Nasi
leo twatumwa, kumshuhudia Kristo,
Popote tuendapo, kwa matendo na maneno,
Yeye yu pamoja nasi, hata mwisho wa dahari,
Ahadi yake ya kweli, hututia moyo daima.
Msomaji wangu haya ni kutok ndani ya kuta za Kanisa Katoliki Ulimwenguni kwa waamini wake.
Wakati Mwanakwetu anayatayarisha makala haya katikati ya Mji wa Musoma hali ya hewa ilikuwa ni nyuzi joto 25, unyevunyevu ni wa asilimia 10, ujirani na mvua ni wa asilimia 72, huku upepo ukivuma kwa KM 3 kwa saa,
Mwanakwetu upo? Kumbuka:
“Tunatumwa Kuishi Utume wa Kristo Aliyepaa.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257






.gif)

Post a Comment