Adeladius Makwega-TARIME.
Mkuu wa Wilaya ya Rorya mheshimwa Khalifan Haule amewapongeza wanahabari mkoa wa Mara kwa kufanya kazi vizuri, huku akisema wanatakiwa kuendelea na moyo huo ili kulijenga taifa la Tanzania kwa moyo wote.
“Tunaheshimu, tunathamini mchango wenu katika kazi hii ambapo kwa sasa vyombo vya habari ni muhimili katika kulijenga taifa letu.”
Haya yamesemwa Mei 22, 2026 Wilayani Tarime katika maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Habari mkoa wa Mara huku tukio hili likiwakusanya wanahabari zaidi ya 100 kutoka wilaya zote za mkoa wa Mara.
Awali Mheshimiwa Haule alizindua mfuko wa wanahabari Mkoa wa Mara ambapo kila mwanachama huchangia shilingi 5,000./= kila mwezi ambapo pesa hizi hutumika pale mwanahabari aliyechangia anapopata changamoto.
Akizungumza katika hafla hii fupi ya maadhimisho haya Mwenyekiti wa Kilabu ya waandishi wa Habari Mkoa wa Mara ndugu Jacob Mugini alisema kuwa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo Vya habari Kitaifa yalifanyika mkoani Arusha huku akiwaomba wanahabari mkoa wa Mara kuendelea kuwa na umoja katika kuitumikia taaluma ya habari Tanzania na duniani kote.
Siku ya Uhuru wa Habari husherekewa Mei 3 ya kila mwaka ili kutambua na kuthamini mchango wa wanahabari mbalimbali ulimwenguni namna walivyojitoa katika hii dunia katika mazingira mbalimbali ya hatari huku wengine wakiuwawa na hata kupata vilema vya kudumu wakiwa kazini.
Siku hii ilitambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa mwaka wa 1993 kupitia UNESCO na kuanza kuadhimishwa kila mwaka.
“Katika kipindi cha miaka 10 tangu 2016-2026 takwimu zinadokeza wanahabari na watumishi ndani ya vyombo vya habari 1000 wameuwawa duniani kote wakiwa kazini, huku idadi kubwa ikiwa Mashariki ya Kati, Ukraine na Sudan.”
Wakati haya yakiendelea hapa Mkoani Mara hali ya hewa ya mji wa Tarime ni nyuzi joto 26, unyevunyevu ni wa asilimia 20, ujirani na mvua ukiwa wa asilimia 62 na upepo ukivuma kwa KM 5 kwa saa.
Mwanakwetu upo? Kumbuka:
“Tunathamini Mchango wa Wanahabari.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257
.gif)



.gif)

Post a Comment